Tuesday, July 31, 2012

MAKUMBUSHO YA BUJORA,MOJA YA VIVUTI VILIVYOSAHAULIKA LICHA YA KUTOA FURSA YA AJIRA KWA WASANII.
Charles Madatta,kwa niaba ya Fabian Mhoja ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Makumbusho hayo akionyesha nyumba walizokuwa wakiishi enzi hizo,na wasukuma.


Moja ya nyumba ambazo zilikuwa zikitumia na wafalme wa Kisukuma kwa ajili ya kukutana na kucheza ngoma za asili ya  kisukuma.



Makumbusho ya tamaduni za kabila la kisukuma yaliyopo Kijiji cha Kisesa Jijini Mwanza yameelezwa kuendelea kuwa kivutuo kikubwa afrika Mashariki na kuwavutia watalii kutoka nchi mbalimbali za jumuiya ya Ulayana  kuchangia katika kuliingizia taifa fedha za kigeni.

Akizungumza na blog hii,Charles Madatta,kwa niaba ya Fabian Mhoja ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji  wa Makumbusho hayo alisema kuwa uwepo wa makumbusho hayo,licha ya kusaidia kutunza mila za kisukuma,lakini pia yametoa ajira kwa wananchi wanaozunguka makumbusho.

Alisema kuwa makumbusho hayo yametoa ajira kwa zaidi ya watu 100  kwenye idara mbalimbali, Miongoni mwa ajira inayotolewa na bujora ni pamoja na wasanii wa ngoma za asili ya kisukuma  kujipatia kipato kupitia sanaa yao,kwa kualikwa ndani na nje ya nchi kama Dernmark,Marekani,Ufaransa.
Alisema kuwa vipo vikundi vya ngoma zaidi ya 2000 ambavyo hualikwa kwa ajili ya kufanya maonyesho ya ngoma hizo,ambapo kwa mwaka vikundi zaidi ya 30 huweza kwenda nje ya nchi,na kutoa mchango wa kodi pamoja na wao wenyewe kunufaika na safari hizo.
Jamii inayozunguka makumbusho ya Bujora wanasema kuwa makumbosho hayo yameweza kuwa mkombozi mkubwa hususani wajasiriamali wadogo wadogo,wakiwemo mama ntilie,dereva wa bodaboda na wananchi wengine ambao hupata nafasi ya kufanya kazi kama nlivyokwishaeleza hapo awali
.
Hata hivyo kwa upande wa vikundi ambavyo vinacheza ngoma za kisukuma vimekuwa vikilipwa zaidi ya 150,000 hadi 200,000 pamoja na usafiri wanapoalikwa kutumbuiza sehemu mbalimbali za Jiji la Mwanza.
Miongoni mwa makumbusho Makumbusho nayopatikana bujora ni pamoja na historia ya kabila la kisukuma,picha ambazo zinaonyesha matukio ya asili,bidhaa za kazi za mikono, historia ya uchifu, uhusiano wa kijamii, teknolojia ya uhunzi, sayansi ya uganga wa kijadi na mifumo ya kuhesabu na majina ambayo yanafuata mfumo wa kijinsia na umri wa watu wanaohesabu namba.



Monday, July 30, 2012

SERIKALI YALIFUNGIA GAZETI LA MWANAHALISI. 



Serikali ya Tanzania imetangaza kulifungia gazeti la MWANAHALISI kwa muda usiojulikana kutokana na kuandika habari na makala za uchochezi, uhasama na uzushi likiwa na nia ya kusababisha wananchi kukosa imani na vyombo vya dola.Taarifa iliyotumwa kwenye vyombo vya habari na ofisi ya msajili wa Magazeti Wizara ya habari, Vijana, Utamaduni na michezo imesema katika matoleo ya hivi karibuni, gazeti hilo limekua likichapicha habari na makala zenye kueneza na kujenga hofu kwa wananchi.
Taarifa imesema kabla ya uamuzi wa kulifungia Mwanahalisi, mhariri wa gazeti hilo aliitwa na kuonywa mara nyingi lakini hakuwa tayari kukiri kuwa maudhui ya makala zake hayakua na tija kwa jamii na zilikua hazifati madili ya uandishi wa habari japo amekua akinukuu kifungu cha 18 cha katiba ya Uhuru wa kutoa maoni ambapo hii ni mara ya pili kufungiwa, kabla liliwahi kufungiwa kwa miezi mitatu.





Friday, July 27, 2012


 MFANYABIASHARA AUAWA KWA WIVU WA MAPENZI.

Kamanda wa mkoa wa kipolisi Tarime na Rorya  Justus Kamugisha
 
MFANYABIASHARA mmoja katika kitongoji cha Nyangoto kataya Matongo
wilayani Tarime Mgaya NyamhangaSindo(28)ameuawa kwa kuchomwa visu
sehemu tano maeneo  mbalimbali ya mwili kutokana na wivu wa mapenzi.
Tukio hilo limetokea julai 24,majira ya kati ya saa 1.45 na saa 2:00
mwaka huu  usiku nyumbani kwa Marwa Machugu katika mtaa huo alipokuwa
ameenda kununua mawe yanayodaiwa ya dhahabu limethibitishwa na
polisi,na kiongozi wa mtaa huo.
Mwenyekiti wa kitongoji hicho Chacha Kichere alimtaja mtuhumiwa wa
tukio hilo kuwa ni Ngewa Masicho Magau (39)ambaye anashikiliwa na
polisi  chanzo kikiwa ni ujumbe wa simu unaodaiwa kutumwa na Sindo
kwenye simu ya mkewe Otaigo Ngewa Masicho .
Alimchoma visu sehemu tano ikiwemo tumboni mara mbili,kifuani,jichoni
na mgongoni na kuanguka chini akiwa amepoteza fahamu.
“Ujumbe uliokutwa kwenye simu ya mke wa mtuhumiwa unaodai mbona
hatukukutana  unipe ule mzigo”alifafanua na kuongeza kuwa”kulikuwa na
hisia za kuwa anauhusiano wa kimapenzi na mke wa mtuhumiwa na hata
ndoa yao ilikuwa na mgogoro”alisema Mwenyekiti.
Kabla ya tukio hilo alidai Sindo alipigiwa simu na rafiki yake Marwa
Machugu wakanunue mawe ya dhahabu “wakiwa nyumbani kwa Machugu ghafla
mtuhumiwa alitokea na kuanza kumshambulia kwa kisu huku rafiki yake
akiwa hatoi msaada’alisema.
Hata hivyo alidai Machugu ambaye alimpigia simu anahusishwa na mpango
huo na kuwa ndiye alimpigia simu na kumkuta mtuhumiwa eneo hilo,na
hata hayo madini hayakuwepo.
Alibainisha kuwa majilani ndio walitoa msaada wa kutaka kumwokoa ,hata
hivyo alifia njiani wakati wanampeleka kituo cha afya cha Goldwill
Foundation kituo cha Nyangoto na kulazimika kupeleka mwili wa marehemu
kituo cha afyua cha Sungusungu ambacho ni cha serikali.
Hata hivyo alisema mtuhumiwa baada ya kuona wananchi wamejitokeza kwa
wingi alikimbilia kituo cha polisi akiwa na kisu chake  na
kujisalimisha na  anashikiliwa kuhusiana na tuhuma hizo.
Mmoja wa majilani wa mtuhumiwa jina tunalo aliliambia gazeti hili kuwa
mtuhumiwa siku ya tukio kwa nyakati tofauti alisikika akidai ataua mtu
bila kumtaja mtu mwenyewe.
Kamanda wa mkoa wa kipolisi Tarime na Rorya  Justus Kamugisha alisema
mtuhumiwa natarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote,huku mke wa
mtuhumiwa akisaidia polisi kutokana na kuhusishwa na tukio hilo.
Wakati huo huo alisema Waitara Sebuti Masiane(42)mkazi wa kijiji cha
Nyantira kata ya Nyansincha amekufa baada ya kunywa pombe aina ya
gongo ambayo inadaiwa ilikuwa na sumu na mtuhumiwa Mirama Nyangira
anashikiliwa kwenye kituo kidogo cha Nyamongo.
Mwisho.

Monday, July 9, 2012

UMOJA WA MATAIFA WATOA BILL 11KUWEZESHA KIWANDA CHA MADAWA ARUSHA. 


Umoja wa nchi za Ulaya umetoa kiasi cha Sh bilioni 11 kwa ajili ya kukiwezesha  kiwanda ch kutengeneza madawa ya binadamu cha TPI kilichopo njiro Mkoani Arusha, ambapo kitaanza kutengeneza dawa za kurefusha maisha kwa waathirika kwa ugonjwa wa ukimwi .

Hayo yalisemwa  na Balozi wa Nchi za Umoja wa Ulaya, Timoth Clarke wakati alipokuwa akielezea nchi za umoja wa ulaya zinavyojitahidi kutoa misaada mbalimbali ya kimaendeleo hususan katika sekta ya afya, elimu ,vifo vya kinamama na watoto .

Alisema katika kiwanda hicho kumeanzishwa kitengo cha kutengeneza dawa za kurefusha maisha kwa waathirika wa   VVU na kwamba kiwanda hicho kama hakitafunguliwa ,Taifa linaweza kupoteza nguvu kazi ambazo zinatokana na wale wagonjwa waliokumbwa na maambukizi hayo na kuongeza kuwa kupatikana kwa dawa hizo nchini kutawezesha wale walioathirika na ugonjwa huo kuendelea na shughuli mbalimbali za kijamii ambazo zinaweza kuinua uchumi wan chi.

Alisema si busara kwa nchi kuwatenga waathirika wa ukimwi sehemu mbalimbali bali jamii inatakiwa kuwapa TANZANIA ni nchi mojawapo inayojitahidi kutokomeza maambukizi ya Virusi vya Ukimwi kwa kutumia kampeni mbalimbali ikiwemo kupunguza vifo vya kinamama na watoto vinavyotokana na ugonjwa huo.

WATUHUMIWA WALIOKAMATWA KWA KUTAKA KUMUUA ALBONO WAACHIWA HURU

 MTOTO Mlemavu wa Ngozi (Albino) Adam Robert (13) wakati akiwa amelazwa hospitalini baada ya kujeruhiwa na kwa kukatwa mkono na kisha kunyofolewa Vidole sita vya mikono yote miwili,picha hii ilipigwa siku moja tu baada ya kufikishwa katika hospitali ya wilaya ya Geita,Picha hii ilipigwa Oktoba 14 mwaska 2011.
 HUYU ndiye baba mzazi wa Adam ambaye alidaiwa kuhusika katika tukio la kujeruhi mwanaye ambaye ni Albino,ambaye anadaiwa alikuwa umbali wa hatua 3 kutoka alipokuwa akikatwa mwanaye lakini hakufanya jitihada zozote za kumuokoa,hapa akiwa na pingu chini ya ulinzi mara baada ya kutiwa mbaroni.

MLEMAVU wa ngozi Mtoto Adam akiwa hospitalini baada ya kupona majeraha yake aliyokatwa na kujeruhiwa vibaya.(Picha zote na David Azaria Geita yetu).

WATUHUMIWA watatu waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya kujaribu kumuua Mtoto Mlemavu wa Ngozi Albino Adam Robaert (13) katika mahakama ya wilaya ya Geita, wameachiwa huru na sasa wamerejea nyumbani wakiendelea na maisha yao ya kawaida. 
Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na Mwandishi wa Gazeti hili watuhumiwa hao wakiwemo wazazi wa Mtoto huyo Robert Tangawizi, waliachiwa huru tangu Mei 30 mwaka huu majira ya saa 4 asubuhi kutokana na amri kutoka kwa Mwendesha mashitaka mkuu wa serikali Elieza Feleshi. 
 
Watuhumiwa walioachiwa huru kwa amri hiyo ya Mwendesha Mashitaka Mkuu wa serikali ni pamoja na Baba wa Mlemavu huyo Robert Tangawizi,Mama wa Kambo Agnes Majala,pamoja na mtu mmoja anayedaiwa kuwa ni mganga wa kienyeji Machibya Alphonce wote wakazi wa kijiji cha Nyaruguguna kata Tarafa na Wilaya ya Nyang’hwale Mkoani Geita. 
 
Washitakiwa hao kwa pamoja walikuwa wakikabiliwa na mashitaka mawili kila mmoja katika mahakama hiyo ya wilaya,ambayo ni pamoja na Kujaribu kuua,pamoja na kula njama ya kutaka kuua,ambapo walikamatwa  Oktoba mwaka 2011 na baada ya mahojiano na polisi walifikishwa katika mahakama hiyo ya wilaya. 
Inadaiwa kuwa kukamatwa kwa watuhumkiwa hao kulitokana na maelezo ya mtoto mmelavu aliyejeruhiwa ambaye alidai kuwa siku ya tukio baba yake mzazi alimkaribisha mtuhumiwa anayedaiwa kumkata na kumjeruhi pamoja na kwamba mtoto huyo tayari alikuwa amekwishatoa taarifa za mtuhumiwa huyo kwamba alikuwa akimfuatilia machungani na kumdanganyadanganya. 
Alieleza kuwa hata baada ya kukataa kula mtuhumiwa huyo na kuamua kwenda kuulala ndani ya nyumba baba yake aliendelea kumuita na kumtaka kubebea chakula kupeleka ndani na wakati akiwa njiani kupeleka chakula ndipo alipovamiwa na kuanza kukatwa mapanga huku baba yake akishuhudia kwa macho,na wakati huo mama yake wa kambo alikuwa akimmulika kwa tochi. 
Uchunguzi umebaini kuwa serikali kupitia Mwendesha Mashitaka wake Mkuu imeonesha nia ya kutoendelea na mashitaka dhidi ya watuhumiwa hao (NOLLE-PROSECUI), ambayo hutolewa kwa mujibu wa Kifungu cha 91 kifungu kidogo cha kwanza cha Sheria ya Mwenendo wa Mashitaka ya jinai sura ya 20 ya mwaka 2000. 
Kwa mujibu wa kifungu hicho Mwendesha mashitaka Mkuu wa serikali (DPP) anayo mamlaka ya kutoa maamuzi ya kumuachia huru mshitakiwa yeyote na kwa wakati wowote, endapo ataona kuna haja ya kufanya hivyo bila kuhojiwa na mtu yeyote. 
Uchunguzi zaidi umebaini kuwa Barua ya kuachiwa kwa watuhumiwa hao (Nolle Prosecui) ilisainiwa Aprili 28 mwaka huu na T. Vitalis ambaye ni Mwanasheria wa Serikali mkuu, na kusomwa katika mahakama hiyo ya wilaya Mei 30 mwaka huu na siku hiyo hiyo washitakiwa hao waliachiwa majira ya saa 4 asubuhi. 
Kwa mujibu wa maelezo ya awali ya Mwendesha mashitaka wa polisi katika mahakama hiyo ambayo ilianza kusomwa katika mahakama hiyo Oktoba 24 mwaka 2011 katika mahakama ya wilaya ya Geita mbele ya hakimu Mwandamizi wa mahakama hiyo Zablon Kesase, ambayo haikuwahi kusikilizwa kwa kipindi chote cha miezi minane kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji. 
Kwa mujibu wa maelezo hayo ya awali katika mahakama hiyo watuhumiwa hao wanadaiwa kutenda kosa hilo Oktoba 14 mwaka jana majira ya saa 1:30 katika kijiji cha Nyaruguguna Kata ya Nyang’hwale,ambapo walimkata mkono Mtoto Adam na kisha kumnyofoa vidole sita vya mikono yote miwili. 
Kwa mujibu wa Mwendesha mashitaka wa polisi Thomas Mboya watuhumiwa hao walidaiwa kuhusika katika tukio la kumjeruhi Mlemavu huyo kwa lengo la kukata na kunyofoa baadhi ya viungo vyake na kutoweka navyo na kumsababishia kilema cha maisha. 
Mlemavu huyo alilazwa katika hospitali ya wilaya ya Geita kwa miezi miwili na baada ya kupona alikataa kutoka katika hospitali hiyo ya wilaya kwa ajili ya kurejea nyumbani kwao kijijini kwa hofu ya kuuawa na watu waliomkata na kumnyofoa vidole vyake. 
Hali hiyo ilimfanya Mlemavu huyo kukaa katika hospitali hiyo kwa miezi miwili kabla ya kujitokeza wasamaria wema waliomchukua na kwenda kuishi naye Jijini Dar es Salaam, na hiyo ni baada ya Gazeti hili la Habari Leo kuandika habari nyingi pamoja na makala zilizohusu Madhila ya Mlemavu huyo. 
 
Baadhi ya wananchi pamoja na wapigania haki za binadamu wameonesha kustushwa na kuachiwa na watuhumiwa hao,kwa madai kuwa hatua iliyochukuliwa na Mwendesha mahitaka Mkuu wa Serikali ya kutia sahihi kwa niaba ya Jamhuri kutokuwa na nia ya kuendelea na Mashitaka jalada la watuhumiwa imekuwa ya haraka tofauti na matarajio ya wengi. 
 
Walidai kutokana na vitendo vya mauaji na kujeruhiwa kwa watu wenye ulemavu wa Ngozi (Albino) kuonekana kurejea kwa mara nyingine tena nchini,hakukuwa na sababu zozote za msingi za kuwaachia watuhumiwa hao kwa haraka,hali ambayo walidai inachochoea mauaji dhidi ya walemavu hao kutokana na sheria kutokuwa na makali. 
Paulina Alex ni mmoja wa wanaharakati wa haki za binadamu ambaye pia ni Mkurugenzi wa shirika la NELICO ambalo ni miongoni mwa mashirika yanayojihusisha na utoaji wa mafunzo kuhusiana na haki za binadamu, unyanyapaa, huku akiishi na baadhi ya walemavu wa ngozi wasiokuwa na wazazi pamoja na wala wanaoishi katika mazingira magumu, anasema ni lazima serikali iwe na sheria kali kuhusiana na watu wanaojihusisha na mauaji ya Albino.
 
Akizungumzia kuachiwa kwa watuhumiwa hao Hakimu Mfawidhi wa wilaya ya Geita Desdery Kamugisha alisema wao kama mahakama hawana mamlaka ya kulazimisha kuendelea kusikiliza kesi ambayo Mwendesha mashitaka mkuu wa Serikali (DPP) asmeamuaru kufutwa ama kuachiwa kwa watuhumiwa.
 
“Mwendesha mashitaka Mkuu wa Serikali (DPP) kwa niaba ya Jamhuri anayo mamlaka ya kutoa maamuzi ya kumuachia mshitakiwa yeyote Yule ambaye anakabiliwa na mashitaka ya aina yoyote,na anatoa maamuzi hayo chini ya kifungu 91(1) cha sheria ya mwenendo wa mashitaka ya jinai sura ya 20 ya mwaka 2000,na katika hilo hairuhusiwi mtu yeyote,na anayo mamlakaa ya kutotoa sababu za kufanya hivyo…….kwa hiyo sisi hatuna mamlaka tena ya kuhoji hilo na ndiyo maana tumetekeleza amri na kuwachia…..’’ alifafanua Hakimu Kamugisha. 
 
Hata hivyo kifungu hicho kinachotumiwa na Mwendesha mashitaka Mkuu wa serikali (DPP) na kuwaachia watuhumiwa kimekuwa kikilalamikiwa kwa muda mrefu na wadau wa haki za binadamu kwa madai kuwa kimekuwa kikisababisha hata watu wenye mahitaka stahili kuachiwa na hivyo kuaondoa dhana ya Utawala Bora,lakini hakuna hatua zozote zambazo zimekwishachukuliwa katika kurekebisha ama kujadili kifungu hicho na kukifanyia marekebisho. 
Habari na  David Azaria, wa Geita yetu

Sunday, July 1, 2012

HOTUBA YA RAISI WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA JAKAYA MRISHO KIKWETE.













Ndugu Wananchi,

          Kama ilivyo ada naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehma, kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha kumaliza nusu ya kwanza ya mwaka 2012 salama.  Kwa kutumia utaratibu wetu wa kuzungumza nanyi kila mwisho wa mwezi, leo napenda kuzungumzia mambo mawili. Jambo la kwanza ni suala la usafirishaji haramu wa binadamu nchini na la pili ni la mgomo wa madaktari. 
Usafirishaji Haramu wa Binadamu Nchini

Ndugu Wananchi;
          Bila ya shaka mtakuwa mmezisikia taarifa za tukio la kushtusha na kuhuzunisha la kukutwa maiti 43 za watu wasiojulikana, zilizotupwa katika kichaka kilichopo kijiji cha Chitego, Wilayani Kongwa, Mkoa wa Dodoma tarehe 26 Juni, 2012.  Pamoja na maiti hao, walipatikana watu 84wakiwa hai lakini wote wakiwa wamedhoofu na baadhi yao wakiwa mahututi.  Hatua za haraka zilichukuliwa kuwasafirisha watu hao hadi Dodoma ambapo wale waliokuwa mahututi walifikishwa Hospitali Kuu ya Mkoa wa Dodoma kwa matibabu na wengine walihifadhiwa katika Kituo cha Kati cha Polisi, Dodoma.  Maiti 22 zilipelekwa Dodoma na 21zilipelekwa Morogoro kuhifadhiwa.
Taarifa zilizopatikana kutoka kwa wale walionusurika zimebainisha kuwa watu hao ni raia wa Ethiopia ambao walikuwa safarini kwenda Malawi na baadaye Afrika ya Kusini ambako wangetengenezewa utaratibu wa kwenda kuishi Marekani na Ulaya.  Kwa mujibu wa maelezo yao, safari yao ilianza miezi mitano iliyopita.  Mwezi mmoja waliutumia Ethiopia na miezi minne waliitumia Kenya kabla ya kuletwa Arusha ambako walipakiwa kwenye lori na kuanza safari ya kuelekea Malawi lakini ikaishia Chitego.  Lori walilopanda lilikuwa limezibwa kabisa na hivyo kusababisha vifo kwa kukosa hewa.
Tukio la Chitego, Dodoma la wahamiaji haramu kukamatwa na wengine kukutwa wamekufa si la kwanza kutokea hapa nchini.  Kwa jumla, katika kipindi cha takriban miaka 10 sasa kumekuwepo na tatizo kubwa la wahamiaji haramu kuingia nchini.  Kwa mfano, kati ya mwaka 2005 na hivi sasa jumla ya wahamiaji haramu 19,683 wamekamatwa.  Karibu wote wameshaondoshwa nchini na hivi sasa wapo karibu watu 1,500 tu magerezani wanaotumikia adhabu na kusubiri kurejeshwa makwao.  Wengi wa watu hao wanatoka Ethiopia na Somalia na baadhi kutoka Pakistan na Bangladesh.
Wahamiaji haramu wamekuwa wanaingia nchini kwa kupitia njia zisizo rasmi.  Wapo wanaotumia nchi kavu hasa kupitia mikoa ya Mara, Arusha, Kilimanjaro na Tanga.  Na, wapo wanaopitia baharini kwa kutumia fukwe za Pemba, Unguja na za mikoa ya ukanda wa Pwani ya Tanzania Bara yaani Tanga, Pwani, Lindi na Mtwara.
Ndugu Wananchi;
Kwa mujibu wa kauli zao, watu hao wamekuwa wanaeleza kuwa hawaji nchini kuhamia bali wao ni wapita njia tu.  Wanaelekea Afrika ya Kusini ambako wameahidiwa kuwa watatengenezewa mipango ya kuhamia Marekani na Ulaya.  Watu hao pia wamethibitisha kuwepo kwa watu maalum wanaojihusisha na usafiri wao tangu nchi watokako na zote wanazopitia mpaka kule waendako.  Aidha, wamesema kuwa wao wanawalipa watu hao ili wawasafirishe na hakika si kiwango kidogo.  Kwa jumla ni kwamba hili si suala la uhamiaji haramu bali ni la biashara haramu ya kusafirisha binadamu.
Ndugu Wananchi;
Kufuatia vyombo vyetu vya usalama kuwa makini na watu wengi kukamatwa ndipo wasafirishaji walipobuni njia za kuwasafirisha kama mizigo.  Makontena, malori yaliyofunikwa nyuma na matenki ya mafuta na ya maji yamekuwa yanatumika kwa ajili hiyo.  Usafiri wa aina hiyo ndiyo uliosababisha vifo vilivyotokea Dodoma tarehe 26 Juni, 2012 na vya watu 21 vilivyotokea mwezi Desemba, 2011 Mkoani Morogoro, na vile vya watu 12 vilivyotokea katika matukio mawili ya Mkoa wa Mbeya, mwezi Mei, 2012.
Ndugu Wananchi;
Tarehe 27 Juni, 2012 nilikutana na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama nchini kuzungumzia tukio la Chitego na suala zima la biashara hii haramu na hasa mbinu mpya inayotumiwa na wasafarishaji.  Nilitoa pongezi kwa vyombo vya dola kwa kazi nzuri waifanyayo kudhibiti shughuli za biashara hii haramu hapa nchini.  Tulielewana kuwa waendelee kuimarisha udhibiti huo kwa lengo la kukomesha kabisa biashara hii.
 Niliagiza pia kwamba kikundi kazi nilichokiunda mwaka 2006 kushughulikia ujambazi sasa kielekeze sehemu ya nguvu zake kukabili tatizo hili. Aidha, kwa pamoja tulikubaliana kuwa nchi yetu ishirikiane na wenzetu wa Ethiopia, Kenya, Malawi, Msumbiji na Afrika ya Kusini kutambua mawakala na kuwabana kwa mujibu wa sheria.  Tayari nimeshaanza kufanya mawasiliano na baadhi ya Wakuu wa Nchi hizo kuhusu ushirikiano huo.  Nashukuru wote wameafiki nchi zetu zishirikiane kwa pamoja kuvunja mtandao huu mchafu na kutokomeza biashara hii haramu na inayodhalilisha utu wa mwanadamu.
Ndugu Wananchi;
Napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru wenzetu, wakazi wa vijiji vya Chitego na Mkoka kwa kazi nzuri walioifanya. Kwa kweli, wenzetu wameonesha uzalendo wa hali ya juu kwa kutoa taarifa mapema juu ya jambo lenyewe, lakini pia wameonesha utu kwa kuwajali wageni waliokumbwa na janga hili. Naushukuru pia uongozi wa Mkoa wa Dodoma na Morogoro ikiwa ni pamoja na vyombo vya ulinzi  na usalama kwa kulishughulikia tatizo hilo kwa umakini mkubwa.   Nimefurahishwa sana na ushirikiano ulioonyeshwa na vyombo na taasisi mbalimbali za Serikali katika kushughulikia suala hili.
Mgomo wa Madaktari
Ndugu Wananchi;
          Jambo la pili ni kuhusu mgomo wa Madaktari unaoendelea nchini hivi sasa.  Nilipozungumza na Wazee wa Dar es Salaam katika Ukumbi wa Diamond Jubilee tarehe 12 Machi, 2012, kuhusu mgomo wa Madaktari uliokuwa unaendelea wakati ule pamoja na kuelezea chimbuko la mgomo na hatua iliyokuwa imefikiwa, nilielezea mazungumzo yangu na viongozi wa Chama cha Madakari wakiwemo pia viongozi wa Jumuiya ya Madaktari.  Nilitoa taarifa kuwa tumeelewana kuwa watasitisha mgomo na watarudi kwenye meza ya majadiliano na Serikali.  Siku ile pia nilielezea matumaini yangu kuwa mgomo ule utakuwa wa mwisho katika nchi yetu.  Bahati mbaya matumaini yangu hayo hayakuwa na hivi sasa tunashuhudia tena wagonjwa wakiteseka, kuhangaika na wengine kufa kwa sababu ya kukosa huduma wanazostahili kwa vile madaktari wao wamegoma tena.
Ndugu Wananchi;
Kama walivyoniahidi, madaktari waliacha kugoma na viongozi wao walirudi kwenye mazungumzo na Serikali.  Kama ilivyoagizwa na Mahakama Kuu, Kitengo cha Kazi tarehe 8 Machi, 2012, kwa mujibu wa Sheria ya Mahusiano Kazini, Namba 6 ya mwaka 2004.   Chama cha Madaktari na Serikali walifika katika Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (Commission for Mediation and Arbitration) kwa ajili ya majadiliano.  Kwa pamoja na kwa ridhaa yao wote, pande hizo mbili ziliiomba Tume hiyo iwape fursa ya kuzungumza wao wenyewe na wakimaliza mazungumzo wataenda kusajili makubaliano yao.  Tume ikawakubalia.  Ni vizuri ikakumbukwa kuwa siku ile ya tarehe 8 Machi, 2012 Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi, ilitoa zuio la mgomo pamoja na kuagiza kuwepo mazungumzo baina ya pande mbili.
Ndugu Wananchi;
Kati ya tarehe 10 Aprili, 2012 na tarehe 30 Mei, 2012, vilifanyika vikao sita vya majadiliano kati ya Serikali na Chama cha Madaktari.  Katika mazungumzo hayo hoja au madai 12 ya madaktari yalizungumzwa.  Mambo hayo ni haya yafuatayo:
1.    Posho ya kuitwa kazini (on call allowance) iwe asilimia 10 ya mshahara.
2.    Posho ya kufanya kazi katika mazingira hatarishi (Risk allowance) iwe asilimia 30 ya mshahara.
3.    Madaktari wapatiwe nyumba grade A au posho ya makazi ambayo iwe asilimia 30ya mshahara.
4.    Posho ya kufanya kazi katika mazingira magumu iwe asilimia 40 ya mshahara.
5.    Madaktari walipwe posho ya usafiri ya asilimia 10 ya mshahara au wakopeshwe magari.
6.    Madaktari wanaoanza kazi walipwe mshahara wa shilingi 3,500,00/= kwa mwezi.
7.    Madaktari wapatiwe Green Card za Bima ya afya.
8.    Hatua za kinidhamu zichukuliwe dhidi ya Watendaji Wakuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
9.    Viongozi wa Kisiasa kulazimisha kupewa rufaa nje.
10.           Madaktari waliofukuzwa warudishwe kazini.
11.           Huduma za afya ziboreshwe nchini.
12.           Posho ya uchunguzi wa maiti iongezwe.

Ndugu Wananchi;
          Katika mambo hayo 12 pande zote mbili zilifikia muafaka na kukubaliana wa pamoja kwa mambo saba.  La kwanza, ni kuhusu usafiri wa kwenda na kurudi kazini.  Serikali ilieleza kuwa upo utaratibu kwa mujibu wa Waraka wa Utumishi wa Serikali Na. 3 wa mwaka 2011 wa kuwakopesha wafanyakazi wa Serikali fedha za kununulia magari au pikipiki, samani na matengenezo ya magari.  Ilikubaliwa kuwa madaktari waitumie fursa hiyo.
          Jambo la pili, ni kuhusu madaktari kupatiwa Green Card za Bima ya Afya.  Jambo hili lilikubaliwa na Serikali na Wizara ya Afya imekwishachukua hatua za utekelezaji wake.
          Jambo la tatu, ni kuhusu hatua za kinidhamu kuchukuliwa dhidi ya Watendaji Wakuu wa Wizara ya Afya.  Kwa pamoja walikubaliana kuwa suala hilo liko nje ya mamlaka ya Kamati yao ya pamoja, waziachie mamlaka husika za uteuzi.  Uongozi wa juu wa Wizara umebadilishwa na sasa kuna uongozi mpya.  Lakini, jambo la kustaajanisha hata Waziri mpya wa Afya alipowataka waonane kuzungumzia hoja walikataa kumuona.  Kwanza walisema hawaoni sababu kwa vile wameyazungumza na Kamati yake kwa miezi mitatu bila ya mafanikio
          Jambo la nne walilokubaliana ni kuhusu viongozi kulazimisha kupewa rufaa ya kutibiwa nje.  Walikubaliana mambo mawili.  Kwanza,kwamba maelekezo ya Waziri Mkuu, Mhe. Mizengo Pinda kuwa madaktari wazingatie maadili ya kazi zao na kukataa kutoa rufaa kwa mtu asiyestahili awe kiongozi au asiwe kiongozi. Pili, walikubaliana kuwa hospitali zilizopo ziboreshwe ili viongozi watibiwe hapa nchini.  Ukweli ni kwamba kufanya hivyo ndiyo sera ya Serikali.  Nililieleza hili mwezi Desemba 30, 2005 katika hotuba yangu ya kuzindua Bunge baada ya kuchaguliwa kwa mara ya kwanza kuongoza nchi yetu. 
Tumeiongeza sana bajeti ya sekta ya afya kutoka shilingi bilioni 300 2005/2006 hadi shilingi trilioni 1.2 mwaka 2011/12 na imekuwa ya tatu baada ya miundombinu na elimu.  Tumeziimarisha hospitali za Mikoa kwa vifaa tiba na wataalamu wa afya.  Kazi inaendelea katika hospitali za Wilaya. Tumewekeza katika Hospitali ya Muhimbili.  Hospitali hiyo ilivyo leo sivyo ilivyokuwa miaka sita nyuma.  Na kazi inaendelea hasa katika maeneo ambayo tunapeleka wagonjwa nje.  Matunda yake yanaanza kuonekana kwa upande wa figo, moyo, kinywa na mipango inaendelea kwa upande wa ubongo na mishipa ya fahamu.  Tunaendelea kuimarisha mafunzo ya  madaktari na madaktari bingwa, yote kwa nia hiyo hiyo.  Hivi sasa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba,Muhimbili kinachukua wanafunzi wengi zaidi ya ilivyokuwa siku za nyuma na makazi mapya ya chuo yanaendelea kuandaliwa ili kuchukua wanafunzi wengi zaid.    Mwaka 2005 tulikuwa na madaktari bingwa 46 mwaka huu tunao 520.
Ndugu Wananchi;
          Jambo la tano ambalo pande zote mbili zilikubaliana ni kuhusu madaktari waliofukuzwa.  Hawa ni wale Interns waliokuwa wamerudishwa Wizarani kutoka Muhimbili na kupangiwa hospitali za Temeke, Ilala, Mwananyamala na Lugalo.  Hili ni jambo ambalo lilikuwa limemalizika kitambo na wote walikuwa wamerudi Muhimbili.
          Jambo la sita ni kuhusu mapendekezo mbalimbali yaliyotolewa na madaktari kuhusu kuboresha huduma ya afya.  Mapendekezo hayo yalihusu kutathmini sera na mpango wa afya ya msingi, bajeti ya afya kuwa asilimia 15 ya bajeti ya Serikali, kuwepo na utaratibu mzuri wa kuajiri madaktari na kuboresha viwango vya ubora wa madaktari na kadhalika.  Serikali imeyaafiki mapendekezo hayo na yatafanyiwa kazi.
          Jambo la saba, ambalo pande zote walilokubaliana ni kuhusu kuongeza posho ya uchunguzi wa maiti.  Hili ni jambo jipya halikuwepo mwazoni.  Hata hivyo, Serikali imelikubali na posho hiyo imeongezwa kutoka shilingi 10,000/= hadi kufikia shilingi 100,000/= kwa daktari na shilingi 50,000/= kwa wasaidizi wake.
Ndugu Wananchi;
          Kuna masuala matatu ambayo yamekuwa na muafaka kwa kiasi fulani na kutoafikiana kwa baadhi ya mambo.  La kwanza ni suala la kufanya kazi katika mazingira hatarishi.  Serikali imekubali hoja ya kuchukua hatua ya kuwalinda madaktari wanaofanya kazi katika mazingira hatarishi.  Serikali iliwaeleza kuwa watumishi wa kada zote za afya watapatiwa chanjo dhidi ya maambukizi ya Hepatitis B na fedha zimetengwa katika bajeti ya 2012/13.
Aidha, Serikali imeeleza dhamira ya kurudisha posho ya mazingira hatarishi kwa watumishi wa umma wanaostahili.  Utekelezaji wake utafanyika baada ya uchambuzi wa kina wa kubainisha mazingira hatarishi ni yepi, viwango stahiki viwe vipi na nani hasa wahusike.  Madaktari wamekataa hili la kufanya uchambuzi, wanataka kiwango kiwe kama wanavyotaka wao, yaani asilimia 30 ya mshahara na kianze mara moja.
          Jambo la pili ambalo wamekubaliana nusu nusu ni kuhusu nyumba za kuishi.  Serikali imekiri wajibu wake wa kuwapatia madakari nyumba za kuishi.  Aidha, imeeleza mpango ulioanza wa kujenga nyumba 700 za madaktari kote nchini na kwamba hivi sasa ujenzi wa nyumba 90 unaendelea, 50 katika mkoa wa Mtwara na 40 katika mkoa wa Rukwa.
 Kwa maeneo ambayo madaktari wanalipwa posho ya pango Serikali imesema waajiri wataendelea kufanya hivyo kwa mujibu wa taratibu zilizopo kwa watumishi wa umma wenye stahili ya kupewa nyumba.  Jambo hilo limekataliwa na Madakari na kutaka lazima walipwe asilimia 30 ya mshahara kama posho ya nyumba.  Serikali kwa upande wake imeona vigumu kufanya hivyo na kuwasihi wakubali wanayotendewa wafanyakazi wengine wote wa umma.
          Jambo lingine ambalo lilikuwa na makubaliano ya nusu nusu ni kuhusu posho ya kufanya kazi katika mazingira magumu.  Pande zote mbili ziliafikiana kuwa yapo baadhi ya maeneo nchini yanayo mazingira magumu kwa watumishi wa umma  hivyo hatua zichukuliwe kuwasaidia watumishi hao. Serikali imekubali wajibu wa kuweka utaratibu wa kuboresha maisha ya watumishi katika maeneo hayo.  Kwa ajili hiyo, Serikali itatoa mwongozo kwa mamlaka za ajira kuhusu namna ya kuwasaidia watumishi hao kupunguza makali ya maisha katika kila eneo badala ya kutegemea posho peke yake.
  Kuhusu posho, Serikali imeeleza kuafiki kuwepo posho ya aina hiyo ila itatekelezwa baada ya kufanya uchambuzi wa kuainisha mazingira husika, kutambua watumishi waliopo na gharama zake.
          Madaktari hawajakubali kusubiri zoezi la uchambuzi lifanyike, wanataka Serikali ilipe posho hiyo sasa.  Tofauti hapa si posho hiyo kuwepo, bali ni rai ya Serikali ya kubaini maeneo yenyewe na kupanga aina ya hatua na viwango vya posho kulingana na mazingira halisi ya maeneo.  Madaktari hawaoni haja ya kufanya hayo.
Ndugu Wananchi;
          Mambo mawili hayakuwa na muafaka kabisa kati ya pande zetu mbili.  Jambo la kwanza ni posho ya kuitwa kazini (on call allowance).  Kwanza sina budi kueleza kuwa Serikali imekubali kuongeza posho hiyo.  Tangu Februari, 2012 posho iliongezwa kutoka shilingi 10,000/= hadi shilingi 25,000/=kwa daktari bingwa (Specialist), shilingi 20,000/= kwa dakari mwenye usajili wa kudumu (Registrars) na shilingi 15,000/= kwa madaktari waliohitimu ambao wapo katika kipindi cha mafunzo kazini (Interns).  Viwango hivyo vya posho vinatumika hivi sasa. 
  Madaktari kwa upande wao hawakukubali uamuzi huo wa Serikali na kusisitiza walipwe asilimia 10 ya mshahara.  Ugumu wa kukubali pendekezo la madakari ni kuwa sharti la malipo haya ni mtu kuitwa kazini.  Ukitaka ilipwe kiwango cha mshahara ina maana kuwa hata kama daktari hakupangwa kuitwa au alipangwa na hakutokea aendelee kulipwa.  Hili haliwezi kuwa sahihi kufanya.  Linaweza kuwafanya baadhi ya madaktari kutokutimiza wajibu wao kwa vile wana hakika mwisho wa mwezi malipo yako pale pale.
Ndugu Wananchi;
Jambo la pili ambalo muafaka haukufikiwa baina ya Serikali na madaktari ni kuhusu mshahara wa kuanzia kazi wa daktari.  Madaktari wanataka uwe shilingi 3,500,000/= wakati Serikali inasema kiasi hicho hatukiwezi.  Serikali imeeleza utayari wake wa kuongeza mshahara kwa kati ya asilimia 15 mpaka 20 kama ambavyo itafanya kwa watumishi wote wa umma katika mwaka huu wa fedha.  Kwa kiwango cha sasa cha mshahara wao, daktari ataanzia kati ya shilingi 1,100,000/=na 1,200,000/= kutegemea kiwango kipi hatimaye kitaamuliwa.  Madaktari wamekataa katakata na wameng’ang’ania shilingi 3,500,000/=.
Ndugu Wananchi;
Huo ndiyo mlolongo wa mambo yaliyozungumzwa na pande zote mbili na matokeo ya mazungumzo yenyewe.  Katika kikao cha sita kilichofanyika tarehe 30 Mei, 2012, upande wa Chama cha Madaktari ulisema kuwa kwa vile hoja ya nyongeza ya mshahara haina mabadiliko hawakuona haja ya kuendelea na majadiliano mpaka watakapowasiliana na wenzao.  Waliahidi kutoa taarifa ndani ya wiki mbili.  Tarehe 12 Juni, 2012, Rais wa MAT aliandika barua kwa Katibu Mkuu Utumishi ambaye ndiye kiongozi wa majadiliano kwa upande wa Serikali, kuwa Madaktari wameikataa taarifa na ufafanuzi waliopewa kutoka Serikalini kwa ujumla wake.
Ndugu Wananchi;
 Baada ya majibu yale ya madaktari, tarehe 19 Juni, 2012, Serikali na Madaktari walikwenda kwa Msuluhishi (CMA) kutoa taarifa kuwa mgogoro umekosa usuluhishi kama sheria inavyotaka.  Kwa pamoja pande zote mbili zilikubaliana suala hilo lifikishwe Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi.  Wakati pande zote zinasuburi mgogoro huu kufikishwa ngazi hiyo ya juu, upande wa Madaktari ukatangaza kuwepo kwa mgomo kuanzia saa sita ya usiku tarehe 23 Juni, 2012.  Hatua hiyo haikustahili kwani suala lenyewe halijafika mwisho wa kushughulikiwa kwa mujibu wa Sheria za Mahusiano ya Kazi nchini.
Ndugu Wananchi;
Tarehe 22 Juni, 2012, Mwanasheria Mkuu wa Serikali akaenda Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi kulifikisha suala la tishio la mgomo na kuomba zuio la muda kufanywa.   Mahakama Kuu ilikubali ombi hilo na kuagiza kuwa mgomo usitishwe.  Juhudi za kumtafuta Rais wa MAT, Dkt. Namala Mkopi na viongozi wengine wa MAT hazikufanikiwa, Ofisi ya MAT ilikuwa imefungwa na simu zote za viongozi wa MAT zilikuwa zimezimwa.  Hatimaye tarehe 25 Juni, 2012, alipatikana na kupewa amri hiyo ya Mahakama.  Tarehe 26 Juni, 2012, Dkt. Mkopi alifika Mahakamani ambapo alikana kuwa yeye hahusiki na kuitisha huo mgomo lakini hakumtaja aliyehusika.  Pamoja na rai hiyo, Jaji alimuamuru Rais wa MAT akawatangazie wanachama wake kusitisha mgomo.   Dkt. Namala Mkopi hajafanya hivyo hadi leo na mgomo umekuwa unaendelea kinyume cha Sheria.
Ndugu Wananchi;
Wagonjwa wanateseka na wengine kupoteza maisha kwa mgomo huu usiokuwa halali kisheria ambao pia haustahili kuwepo hata kwa mujibu wa maadili ya udaktari.  Viongozi wa  MAT na wenzao wanawaingiza Madaktari katika mgogoro na Mahakama na waajiri wao isivyostahili.  Ni vyema viongozi wa Madaktari na madaktari wakatambua kuwa wanashiriki katika mgomo usiokuwa halali ambao pia kiongozi wao mkuu amekana Mahakamani kuwa hahusiki nao.  Madaktari lazima watambue pia kwamba ajira zao wanaziweka hatarini.  Mfanyakazi ana kinga ya kutofukuzwa kazi na mwajiri kwa kushiriki mgomo unaokubalika kisheria.  Huu siyo.  Watapoteza ajira, hawana pa kukimbilia, hawana cha kiwalinda.  Kwa madaktari interns, wanahatarisha maisha yao kwani hawatapata cheti cha kudumu wakishiriki mgomo usiokuwa halali.   Lazima watafakari sana kwa hayo wafanyayo. 
Ndugu Wananchi;
          Napenda kurudia maneno niliyoyasema tarehe 12 Machi, 2012, kuwa kuboresha mishahara na maslahi ya wafanyakazi ni Sera ya Serikali yetu kwa maelekezo ya Ilani ya Chama Tawala (CCM).  Tumeitekeleza kwa vitendo sera hiyo, hata hivyo ni ukweli ulio wazi kuwa nia yangu njema tu pekee haitoshi, lazima uwezo wa kufanya hivyo uwepo.  Kwa kulingana na uwezo uliopo, tumeendelea kuboresha mishahara na maslahi ya wafanyakazi hatua kwa hatua tangu tuingie madarakani.  Tumefanya hivyo kwa jumla kwa wafanyakazi wote na kwa kada mbalimbali za watumishi wa umma.
Miongoni mwa wafanyakazi wa umma walionufaika na hatua hizo za Serikali ni madaktari na watumishi wa kada nyingine za huduma ya afya.  Tena nadiriki kusema madaktari tumewapa upendeleo mkubwa kuliko watumishi wengine wa umma.  Upendeleo upo kwenye mafunzo ambapo wanafunzi wa udaktari wanagharimiwa na Serikali kwa asilimia mia moja wakati wanafunzi wenzao wa taaluma nyingine hawako hivyo.
Ndugu Wananchi;
Mwaka 2004/2005, mshahara wa kuanzia wa daktari ulikuwa shilingi 178,700/=, mwaka 2005/ 2006 tuliupandisha na kuwa shilingi 403,120/=. Tuliendelea kuupandisha mwaka hadi mwaka mpaka kufikia shilingi 957,700/=wanazolipwa sasa.  Kiasi hicho ni mara mbili ya mishahara ya watumishi wa taaluma nyingine wenye shahada ya kwanza wanaoanza kazi ambao kwa wastani hupata shilingi 446,100/=.
Tunafanya hivyo kwa kutambua na kuthamini nafasi maalum ya madaktari katika jamii na ukweli kwamba bado tunayo safari ndefu ya kuziba pengo la madaktari nchini.  Lakini inaonekana juhudi zetu zote hizo hazithaminiwi.
Ndugu Wananchi;
Sina budi kusisitiza  kwamba tunapofanya hivyo tunaongozwa na uwezo tulio nao wa kulipa.   Kwa sasa hatuwezi kuwaahidi kuwa tunao uwezo wa kuwalipa mshahara wa kuanzia wa shilingi 3,500,000/= na posho zote zile. Tukifanya hivyo malipo ya daktari anayeanza kazi yatakuwa shilingi 7,700,000/=.  Kwa hakika kiasi hicho hatutakiweza. Si vyema kutoa ahadi hewa kwa watu tunaowaheshimu na kuwathamini kama walivyo madaktari.
Kutokana na ukweli huo basi kama daktari anayeona kuwa hawezi kufanya kazi Serikalini bila ya kulipwa mshahara huo awe huru kuacha kazi na kwenda kwa muajiri anayeweza kumlipa kiasi hicho.  Nasi tutamtakia kila la heri.  Hana sababu ya kugoma ili ashinikize kulipwa mshahara huo. Asisumbuke, hatalipwa mshahara huo.  Isitoshe, hana sababu ya kuendelea kuwa na mgogoro na mwajiri ambaye hana uwezo wa kumlipa anachokitaka.  Huna sababu ya kumpa usumbufu mwajiri wa kukuandikia barua ya kujieleza au kukuachisha kazi.  Kwa nini upate usumbufu wa kupata barua hizo na kuzijibu. Kwa nini upate usumbufu wa kuachishwa kazi na kutakiwa kuondoka kwenye nyumba ya Serikali ndani ya saa 24.  Jiepushe na yote hayo kwa kujiondoa mwenyewe.  Usipofanya hivyo, mwajiri anakuwa hana jinsi bali kukuondoa kazini maana unakwenda kinyume na sheria za kazi na maadili ya kazi ya udaktari.
  Mamlaka za ajira zimeanza kuchukua hatua hizo na wataendelea kufanya hivyo kwa wote wanaoendelea kugoma.   Najua baada ya hatua hizo kuchukuliwa kuna manun’guniko ya kuonewa. Hivyo, mlitegemea mwajiri afanyeje? Ni bora kufanya hivyo ili ajue hana daktari aweze kufanya utaratibu wa kuziba hilo pengo na huyo ajae awe na mahali pa kuishi. Vinginevyo atakuwa anajidanganya kuwa anae daktari ambae hayupo kazini na wala hataki kufanya kazi.
Ndugu Wananchi;
Napenda kuwathibitishia kwamba dhamira ya Serikali ya kuboresha maslahi ya watumishi wa umma wakiwemo  madaktari iko wazi.  Tumekuwa tunafanya hivyo, na tutaendelea kufanya hivyo kulingana na uwezo wa kibajeti.  Ni vyema watumishi wa umma wakatambua kuwa hatuwezi kutumia fedha zote au kiasi kikubwa mno cha pesa za umma kulipana mishahara.  Tukifanya hivyo, Serikali itashindwa kutoa huduma muhimu kwa wananchi ambao ndiyo wengi na wanastahili kuhudumiwa.  Hata hizo huduma za afya tunazosema ni duni tuziboreshe, hatutaweza kuziboresha kama tutatumia sehemu kubwa ya pesa za Serikali kuwalipa mishahara wafanyakazi. 
Hivi sasa matumizi ya mishahara ni asilimia 48 ya bajeti ya Serikali.  Kiwango hicho ni kikubwa mno.  Uwiano mzuri ni kuwa na matumizi ya mishahara yasiyozidi asilimia 35 ya bajeti na asilimia 65zitumike kugharimia huduma na shughuli nyingine za maendeleo ya wananchi na taifa.  Sisi tumezidi kwa asilimia 13.  Hivyo, hatuna budi tukubali kujinyima kwa manufaa ya walio wengi. 
Suala la Dkt. Steven Ulimboka
Ndugu Wananchi;
Kabla ya kumaliza hotuba yangu, napenda kuungana na Watanzania wenzangu wote kuelezea masikitiko yangu makubwa na kuhuzunishwa kwangu na kitendo cha kinyama alichofanyiwa Dkt. Steven Ulimboka usiku wa tarehe 26 Juni, 2012. Kitendo hicho ni kinyume kabisa na mila na desturi zetu. Watanzania hatujayazoea mambo hayo. Nimeelekeza vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi wa kina ili ukweli ujulikane.  Nimesema kuwa ningependa ukweli huo ujulikane mapema ili tuondoe wingu baya la kutiliana shaka na kulaumiana kunakoendelea hivi sasa.
Natambua kuwa Serikali nayo inatajwa katika orodha ya wanaotiliwa shaka.  Mimi nimeshangazwa sana na hisia hizo kwani siioni sababu ya Serikali kufanya hivyo.  Dkt. Ulimboka alikuwa mmoja wa kiungo muhimu katika mazungumzo baina ya Serikali na Madkatari.  Ni kweli kwamba yeye si mtumishi wa Serikali, hivyo hakustahili kuwa sehemu ya majadiliano haya.  Kulikuwa na rai ya kutaka asiwepo, lakini nilisema wamuache maadam Madaktari wanamuamini kuwa anaweza kuwasemea vizuri zaidi kuliko wao wenyewe walioajiriwa na Serikali.
Ndugu Wananchi;
Kama nilivyoeleza, mazungumzo yalienda vizuri na mafanikio makubwa yamepatikana.  Yapo maeneo machache na hasa eneo la mshahara ambalo hatukuweza kukubaliana.  Hapo tulipofikia si pabaya na tulikubaliana sote kurudi kwenye mkondo wa Sheria kusaidiwa.  Kwa nini Serikali imdhuru Dkt. Ulimboka? Na, kuhusu mgomo, Mahakama Kuu imekwishatoa amri ya kusitisha mgomo.  Anayekaidi amri ya Mahakama ananunua ugomvi na mhimili huo wa dola ambao wenyewe una mamlaka ya kumtia adabu mtu huyo.  Hivi baada ya kufika hapo Serikali iwe na ugomvi na Dkt. Steven Ulimboka kwa sababu ipi na jambo lipi hata iamue kumdhuru?  Kama kuna mtu wa Serikali kafanya, itakuwa kwa sababu zake binafsi na siyo za Serikali au kwa kutumwa na Serikali.
Ndugu Wananchi;  
Kwa niaba yangu na kwa niaba ya Serikali natoa mkono wa pole kwa Dkt. Steven Ulimboka na kumuombea apone haraka ili aungane na familia yake na Watanzania wenzake katika ujenzi wa taifa.  Kwa namna ya pekee namshukuru na kumpongeza Bwana Juma Mgaza, kwa moyo wake wa huruma na upendo na kwa hatua alizochukua za kumsaidia Dkt. Ulimboka.
Naomba kumaliza kwa kuwasihi madaktari kuacha mgomo na kurejea kazini.  Watanzania wenzenu wanateseka na kupoteza maisha.  Muwe na moyo wa huruma na upendo na msaada kwa wagonjwa kama kiapo chenu kinavyowataka.

Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!

Asanteni kwa Kunisikiliza.