Monday, October 22, 2012


*Kupungua kwa samaki pamoja na kufungwa kwa shughuli za uvuvi bwawa la Nyumba ya Mungu kwatishia maisha ya wananchi wanaozunguka bwawa hilo kiuchumi.

                                                           


                                                          Rodrick Mushi.
Kupungua kwa samaki katika bwawa la nyumba ya Mungu kumefanya maisha ya wakazi hao kuwa magumu,kutokana na kutegemea bwawa hilo kujiingizia kipato ambacho kinawasaidia kujikimu kimaisha.
Mkazi wa Kijiji cha Njia Panda Wilayani Mwanga  Peter Msangi anasema kuwa wakazi wa Vijiji vinavyozunguka bwawa hilo vya Kiti cha Mungu,Nyabinda,Kagongo na Langata Bora wote wanategemea kuendesha maisha yao kwa kutumia bwawa hilo.
Anaeleza kuwa wananchi hao hawana njia nyingine mbadala ya kuweza kujipatia kipato tofauti na biashara hiyo ya uvuvi,hivyo ikitokea bwawa hilo kutoweka na wao hawataweza kuishi.
Msangi anasema wakazi wa maeneo yanayozunguka eneo la bwawa kwa ujumla hawana ardhi kwa ajili ya kulima,na iliyopo kidogo ina mawe ambayo haifai kwa kilimo.
Wakazi wengi wanasema kuwa licha ya Serikali kukataza wavuvi kuvua kwa kutumia nyavu zenye matundu chini ya nchi tatu lakini wamekiri kushindwa kufanya hivyo kwani wakitumia matundu makubwa watakuwa hawaambulii kitu.
Mvuvi mwingine aliyejitambulisha kwa jina moja la James anasema kuwa kuvuliwa kwa muda mrefu kwa samaki kwenye bwawa hilo kwa kutumia nyavu ndogo maarufu kama kokoro kumechangia kutoweka kwa samaki wakubwa hali inayochangiwa na kutokuwa na muda wa kuacha samaki hao wakue.
“Wakazi wote tunaozunguka bwawa hili hatuna sehemu nyingine ya kutegemea kupata kipato,hata sisi hatupendi kutumia makokoro, lakini hatuna njia nyingine ya kuishi. Sisi tufanyaje?Alisema James.
Anasema kuwa shughuli za uvuvi kwenye bwawa hilo walianza tangu mwaka 1980,kipindi ambacho hali ya samaki katika bwawa hilo ilikuwa nzuri,kwa upatikanaji wa samaki wakubwa na maji ya kutosha.
Wapo wananchi wanaotupia lawama Serikali kwa kushindwa kudhibiti uvuvi huu haramu,kwa mamlaka husika kusimamia vyema sheria ya uvuvi,kutokana na uvuvi haramu kuendelea kushamiri kila kukicha.
Bwawa la nyumba ya Mungu linazungukwa na Wilaya za Moshi na Mwanga kwa Mkoa wa Kilimanjaro,na Wilaya ya Simanjiro kwa Mkoa wa Manyara,ambapo takribani vijiji 11 vinazunguka bwawa hilo kutoka kwenye Wilaya hizo.
Hitaji la wananchi ni kubwa kwani vijiji vyote nilivyotaja hapo juu vinategemea bwabwa hilo kwa ajili ya kujikimu na wanavua samaki mchana na usiku kama njia ya kujipatia kipato.
Hivyo utaona jitihada za Serikali katika kuokoa kutoweka kabisa kwa samaki kwenye bwawa hili zinahitajika ili kunusuru maisha ya wakazi wanaotegema bwawa hili kwa hapo baadae.
Kilichochangia kupungua kwa samaki
Wananchi wanaozunguka bwawa la nyumba ya mungu wanakiri kuwa wanashiriki katika uvuvi haramu,hi ni kutokana na kutokuwa na njia nyingine mbadala ya kujiingizia kipato.
Daudi Hamisi ambaye ni mvuvi wa muda mrefu anasema kuwa madhara yaliyopatikana kutokana na wao kuendelea kuvua kwa kutumia makokoro ni pamoja na bwawa hilo kutokuwa na samaki wakubwa kama kipindi cha nyuma.
 “Wananchi wanaozunguka bwawa hili wanaendelea kuvua,wapo wanaotoka maeneo mengine nao wanavua,hadi hali sasa imekuwa mbaya kwani wanachovua ni dagaa siyo samaki tena”Alisema.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na taasisi  ya Uvuvi Tanzania(TAFIRI)kwenye bwawa hilo walibaini kuwa endapo wavuvi wangeweza kutumia nyavu zenye macho makubwa kuanzia nchi tatu samaki hao wangepata muda wa kukua.
Utafiti huo unasema kuwa hali hiyo imechangia kupungua kwa samaki waliovunwa na kurekodiwa katika vitabu vya maafisa uvuvi kufika wastani wa tani 1,770,kwa mwaka badala ya tani 5,173.
Hali hiyo inadhihirisha kuwa uvuvi haramu ulivyochangia kupungua kwa samaki kwenye bwawa hilo,ambapo jitihada za makusudi zisipofanywa na Serikali ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa wakazi wanaozunguka bwawa kuwaelimisha umuhimu wa kuachana na uvuvi huo huenda samaki zikatoweka kabisa.
Sheria za uvuvi,zinaeleza wazi juu ya utaratibu uliowekwa wa usajili wa vyombo vya kuvulia na kupewa leseni kwa ajili ya kulipa ushuru pamoja na kupatiwa vibali.
Kwenye bwawa hilo kuna vyombo zaidi ya 921 vinavyofanya kazi ya uvuvi,lakini vyombo 329 ndio vimesajiliwa huku vyombo 592 vikifanya kazi hiyo bila kufuata taratibu ikiwemo uvuvi haramu.
Wavuvi wanaojishughulisha na uvuvi kwenye bwawa la nyumba ya Mungu 654 pekee ndio waliosajiliwa kati ya wavuvi 2800 hivyo utaona kuwa wavuvi 2146 wanafanya shughuliza za uvuvi pasipo kusajiliwa na moja kwa moja wao ndio wamekuwa wakishiriki kwenye uvuvi haramu.
Hivyo kwa namna moja ama nyingine kutokufuatwa kwa sheria kwa wavuvi pamoja na Serikali kulegalega kwa mamlaka zilizopewa rungu la kusimamia sheria za uvuvi nao wanachangia kuendelea kuwepo kwa uvuvi haramu kwenye bwawa hilo.
Adhari za kupungua kwa samaki.
Kilio kikubwa cha wananchi wanaozunguka bwawa la nyumba ya Mungu ni kukosa njia nyingine mbadala ya kujipatia kipato ukiondoa shughuli za uvuvi.
Wanasema kuwa kufungwa kwa bwawa hilo pamoja na kupungua kwa samaki kumekuwa pigo kubwa kwao,kwani uvuvi ndio unaowezesha wao kuwasomesha watoto na majukumu mengine muhimu ya kifamilia.
Mnale Qamang(45) ambaye ni baba wa familia ya watoto watatu anasema kuwa maendeleo aliyonayo yanatokana na biashara hiyo ya uvuvi ambayo ameweza kulea familia pamoja na kuwasomesha watoto.
Anasema kuwa hali sasa imebadilika,wapo wananchi ambao wanaona maisha yamegeuka machungu baada ya samaki kupungua kwenye bwawa la nyumba ya Mungu kutokana na kuwa msaada mkubwa kwao.
Anasema kuwa yeye alikuwa anaweza kupata shilingi 40,000 hadi 60,000 kutokana na shughuli za  uvuvi ambapo baada ya kufungwa kwa bwawa hilo pamoja na uvivu haramu hali imebadilika kwa kiasi kikubwa.
“Kwa kweli sisi wavuvi hatuna tabia ya kuhifadhi fedha ukipata 50,000 au 80,000 unaitumia yote kwa siku moja au mbili kutokana na bwawa unaliona hapa kila siku lakini kwa kweli hali imebadilika sana na maisha yetu yameanza kuwa magumu”Alisema
Qamang anasema kuwa wameshakutana na viongozi mbalimbali wa Serikali baada ya hali ya uvuvu  kuwa mbaya wakiwaeleza vilio vyao lengo likiwa ni jinsi gani wanaweza kuwasaidia kusajili vikundi vyao na kuanzisha miradiu mbalimbali .
Anasema kuwa licha ya wavuvi kuvua kwa siri baada ya shughuli za uvuvi kufungwa lakini wanachoambulia ni dagaa yaani watoto wa samaki kutokana na kuwepo kwa uvuvi haramu kwa muda mrefu pamoja na uvuvu uliopitiliza.
Je Serikali imeshindwa kudhibiiti uvuvi haramu?
Wataalamu mbalimbali kutoka Mikoa ya Arusha,Manyara,na Kilimanjaro walioketi agosti 09 mwaka jana walipendekeza kufungwa kwa shughuli za uvuvi kwenye bwawa hilo kutokana na hali mbaya inayolikabili.
Kikao hicho ambacho kiliwahusiha  maafisa uvuvi kutoka Mkoa wa Kilimanjaro Mgalula Lyoba,Emanuel Mao Manyara na Maria Kalinga pamoja na wataalamu wengine walipitisha kwa pamoja rasimu ya kupendekeza kufungwa kwa bwawa na kusimamishwa kwa shughuli zozote zile.
Wataalamu hao wanapendekeza kuwa,kwa kipindi chote ambacho bwawa hilo litakapokuwa limefungwa kutatakiwa kufanyika kwa ulinzi wa kutosha kwa kushrikisha maafisa uvuvi kufanya doria za majini na nchi kavu kwa muda wote bwawa hilo litakuwa limefungwa.
Kufunga kwa bwawa hilo kunaelezwa kuwa kutasaidia kutoa nafasi kwa samaki wanaopatikana kwa sasa kuweza kukua,na kuzaliana ili kusaidia kkuongezeka kwa idadi ya samaki.
Mkuu wa Wilaya ya Mwanga,Shaibu Ndemanga anasema kuwa bwala hilo lilifungwa tangu mwezi machi mwaka huu kutokana na hali mbaya inayosababishwa na uvuvi haramu.
Anasema amekwishapokea malalamiko kutoka kwa wananchi kutokana na kutegemea bwawa hilo kujipatia kipato,pamoja na wao kutokuwa na njia nyingine ya kuwaingizia  kipato.
Ndemanga anasema mahitaji ya uvuvi ni makubwa,(fish pressure)na hayaendani na samaki wanaopatikana bwawa hilo hadi walipoamua kulifunga kwa muda.
Anasema kuwa kutokana na uvuvi haramu uliokuwa unaendelea kwa kasi kwenye bwawa hilo,Serikali iliamua kulifunga ili kutoa fursa kwa samaki waliopo kuweza kuzaliana na kukua.
Licha ya kufungwa kwa bwawa hilo lakini utafiti uliofanywa na mwandishi wa makala hii ulibaini kuendelea kuwepo kwa uvuvi haramu,kutokana na kutokuwepo kwa ulinzi wa kutosha.
Uchunguzi huo umebaini kuwa,wavuvi zaidi ya 100-120 waendelea kuvua kwa kuvuka hadi kwenye Wilaya za Simanjiro kwenye vijiji vya ngorika,nyumba ya Mungu na magadini,na kuvua samaki wachanga ambao huwauzia wafanyabishara samaki wanazovua.
Mkuu wa Wilaya anakiri kupokea taarifa za uvuvi huo unaoendelea,ambapo samaki zinazovuliwa zinanunuliwa na wafanyabishara na kuuzwa kwenye masoko ya mbalimbali ya Kilimanjaro na Arusha.
Naye Mbunge Mbunge wa Jimbo la Mwanga,Jumanne Magembe,anasema kuwa uvuvi haramu ndio umechangia kwa kiasi kikubwa,kuendelea kutoweka kwa samaki kwenye bwawa hilo.
Magembe ambaye ni Waziri wa Maji anasema kuwa kinachochangia  kuendelea kuwepo kwa  uvuvi haramu ni kutokana na kutokuwepo kwa nguvu ya kutosha kulinda bwawa hilo kwa kipindi ambacho litakuwa limefungwa ili kuruhusu kukua kwa samaki.
Anasema kuwa yeye hakubaliani na wananchi wanaodai hawawezi kusitisha shughuli hizo za uvuvi kwa miezi michache litakapokuwa linafungwa,kwani wapo wakulima wanaolima kwa msimu na wanaendelea kuishi.
“Kufungwa kwa mabwawa na maziwa ni taratibu zilizopo na zinajulikana kwa sababu zinasaidia mfano ni kwamba samaki anaweza kukua kwa gramu 400 kwa siku 90,hivyo kusimamishwa kwa shughuli za uvuvi kutasaidia kama kukiwepo ulinzi wa kutosha”Alisema Magembe.
Bwawa la Nyumba ya Mungu lina ukubwa wa kilomita za mraba 140,ambapo shughuli za uvuvi zilianza tangu ,mwaka 1970,ukifanywa na wavuvi wahamiaji baada ya kupungua kwa uvuvi kwenye ziwa jipe.
Mbali na shughuli za uvuvi lakini bwawa la nyumba ya Mungu lilianzishwa likiwa na malengo mahsusi ya kuzalisha umeme(generation of hydro-electric power)tangu mwaka ,1965 ambapo huzalisha hadi megawati 8 kukukiwa na hali nzuri ya upatikanaji wa maji lakini kwa sasa zinazalishwa megawatt 3,kutokana na bwawa hilo kuwa na kina kidogo cha maji.
Mwisho

No comments:

Post a Comment