Saturday, October 27, 2012

                               UTAJIRI WA BARLOW UNATISHA.

                               KAMANDA BARLOW ENZI ZA UHAI WAKE
 SIKU chache baada ya Jeshi la Polisi kutoa taarifa yake ya uchunguzi kuhusu kifo cha aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow, umeibuka utata wa mali alizokuwa akimiliki, huku akidaiwa kumiliki utajiri wa kutisha likiwamo jengo la ghorofa.

Habari za kiuchunguzi zilizopatikana zinaeleza kuwa mbali ya jengo hilo, Kamanda Barlow anadaiwa pia kumiliki magari zaidi ya saba yakiwamo malori mawili aina ya Fuso, malori mawili ya mchanga, gari dogo aina ya Toyota Cresta pamoja na Toyota Hilux Double Cabin.

Magari hayo yanadaiwa kuhifadhiwa eneo la Nyakato mjini Mwanza, yakisimamiwa na mfanyabiashara mmoja kwa niaba yake.

Mbali na magari hayo kamanda hyo anatajwa kumiliki nyumba ya kifahari mkoani Mara, ambayo aliijenga alipokuwa RPC mkoani humo, huku nyumba nyingine ikiwa maeneo ya Capri-Point jirani na Ikulu ndogo mkoani Mwanza, inayoelezwa kuwa aliinunua baada ya Serikali kutangaza uuzaji wa nyumba zake kwa watumishi wake.

Umiliki wa mali hizo umeibua maswali mengi, wengi wakitaka kujua iwapo zinalingana na kipato cha Kamanda Barlow, licha ya kuwa na cheo cha Kamanda wa Polisi wa mkoa.


Jengo la ghorofa
Moja ya mali za Kamanda huyo ambazo zimeanza kuwa gumzo mjini Mwanza ni jengo la ghorofa ambalo ujenzi wale ulikuwa ukiendelea katika kiwanja Namba 173 Block G, eneo la Nyakato Mahina kwa kibali Na. 6400 (Building Permit), kilichotolewa na ofisi ya Mhandisi Jiji la Mwanza kikiruhusu kujenga jengo la ghorofa tatu.

Mhandisi wa Jiji
Mhandisi wa Jiji la Mwanza, Boniface Nyambele alikiri Kamanda Barlow kuomba kibali cha kujenga jengo la ghorofa katika kiwanja hicho na kwamba, hata ujenzi wake walikuwa wakiufuatilia kwa karibu.

“Kibali kilichotolewa hapa kilikuwa ni kwa ajili ya kujenga jengo la ghorofa tatu, alipoanza ujenzi alieleza kuwa anataka kujenga ghorofa tano, lakini baada ya kukagua jengo hili tulikuta foundation yake ikiwa na uwezo wa kuhimili ghorofa tatu tu, tulimzuia,” alisema Nyambele.

Hata hivyo, mmoja wa wasimamizi wa ujenzi wa jengo hilo, ambaye hakutaka kutajwa jina lake alisema kuwa marehemu Kamanda Barlow, aliwasisitiza kujenga ghorofa tano.

Alisema kwamba kila mara kamanda huyo alikuwa akiwaeleza kuwa masuala ya vibali kutoka Jiji wanapaswa kumwachia yeye licha ya wakaguzi kumkatalia.

“Baada ya kuwa tumejenga hapa ,mwezi mmoja kabla ya kufariki alituita na kumweleza fundi wetu mkuu kuwa alikuwa amebadili mawazo ya kujenga jengo la ghorofa tatu na kwamba, mpango wake sasa ulikuwa ni kuongeza ghorofa nyingine mbili juu,” alisema mmoja wa wasimamizi wake wa ujenzi na kuongeza:

“Alipoelezwa kama kisheria haikubaliki, alidai hayo hayamuhusu atasimamia yeye huko kwenye sheria.”
Mwandishi wa habari hizi alifika eneo linapojengwa ghorofa hilo na kushuhudia ubao unaoonyesha kuwa kibali cha ujenzi wa jengo hilo kimetolewa kwa Liberatus Barlow.

Wizi ulikwamisha ujenzi
Hata hivyo, majuma machache kabla ya kifo chake, eneo hilo la ujenzi kulitokea wizi wa nondo za ujenzi, ambapo baada ya tukio hilo mwangalizi wa jengo hilo na baadhi ya mafundi wake walikamatwa na kuwaweka mahabusu kwa siku nne katika Kituo cha Polisi Nyakato Mwatex huku ikielezwa kuwa kamanda huyo aliwatoa baada ya kukubaliana nao kumlipa nondo zilizopotea.

“Siku ya wizi huo ujenzi ulisimama na tulikamatwa na kulazimishwa kulipa nondo 10 alizodai zimeibwa, lakini msimamizi wetu nakumbuka aliamua kulipa yeye badala yetu na kesi iliishi baada ya kuwekwa ndani siku nne. Alilipa nondo 60 badala ya 10 na huo ulikuwa mwisho wake wa kuendelea na kazi pamoja nasi, ” alisema kijana huyo aliyewahi kufanya kazi ya kibarua katika jengo hilo.

Umiliki wa magari na utata

Mali nyingine zinazodaiwa kumilikiwa na Kamanda Barlow ni pamoja na magari, ambapo katika idadi ya magari hayo, gari moja aina ya Toyota Hilux ambalo ndilo alipata nalo ajali limeonekana kuwa na utata katika umiliki wake kutokana na namba hiyo ya usajili kubainika kuwa siyo yake kwa vile ilisajiliwa kwa gari aina ya Nisan Premier inayomilikiwa na wamiliki wawili.

Ingawa umiliki wa magari mengine unadaiwa kusajiliwa kwa majina ya mfanyabiashara maarufu jijini Mwanza, lakini umiliki wa gari ambalo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Evarist Ndikilo, alipotangaza kifo cha kamanda huyo, alilitangaza pia kuwa ni mali ya marehemu, imebainika kuwa alilipata wiki moja kabla ya kifo chake.

Katika uchunguzi wa Mwananchi Jumapili, imebainika kuwa hata bima ya gari hilo iliyoonyesha imekatwa kutoka Kampuni ya Bima ya Zanzibar, ilikuwa haitambuliki.

Kamanda Barlow alilichukua gari hilo kwa mmoja wa wafanyabiashara jijini Mwanza, ambaye bado jeshi hilo la polisi linamsaka kutokana na utata wa umiliki wake, kuonyesha namba hiyo siyo halisi ya gari hilo.

Meneja wa Kampuni ya Bima
Meneja wa Tawi la Kampuni ya Bima Zanzibar Mkoa wa Mwanza, Suzan Masele alipotakiwa kutoa ufafanuzi wa suala hilo, alisema kuwa stika ya bima ya gari hilo alilokuwa nalo Kamanda Barlow, wamefuatilia kwenye mfumo wao wa malipo wakabaini kuwa haipo.

"Tumeangalia katika system (mfumo) yetu hakuna bima ya malipo hayo, kwa hiyo ni feki," alisema.

Aidha, utata wa umiliki wa gari hilo pamoja na bima yake ulithibitishwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Said Mwema, ambaye alisema jijini Mwanza kuwa jeshi lake lilikuwa likiendelea na uchunguzi wa umiliki wa gari hilo, pamoja na bima yake kujua ukweli na jinsi lilivyoingia mikononi kwa marehemu siku kadhaa kabla ya kifo chake.

“Suala la gari alilokuwa akilitumia marehemu mpaka siku mauti yanamkuta, pamoja na bima yake, hatuwezi kulieleza hapa, kwa sasa bado tunachunguza,” alisema IGP, alipoulizwa na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kumaliza kutoa taarifa za awali za uchunguzi wa kifo Kamanda Barlow.
SOURCE: Frederick Katulanda, Mwanza; MWANANCHI JUMAPILI
HIVI NDIVYO ZITO KABWE ALIVYOFUNGA KAMPENI ZA UCHAGUZI KILIMANJARO.

Asema kiama cha  Vigogo walioficha mabilioni Uswisi kinakuja.
Tayari kuwasilisha hoja binafsi mabilion hayo yarejeshwe.
Mgombea Udiwani wa Kata ya Nanjara reha,Frank Salakana akiwa amebebwa na wapiga kura wake wakati wa kufungwa kwa kampeni ambapo uchaguzi unafanyika leo.

Zito Kabwe akitema cheche zake,ambaye ndiye aliyekuja kwa ajili ya kufunga kampeni hizo.

Zito akimnadi Mgombea Udiwani,Frank Salakana.

Zito akimnadi mgomnbea ubunge wa Kata ya Kilema Kusini,Severine wakati wa kufungwa kwa kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani.

Zitto: Vigogo walioficha mabilioni Uswisi kukiona
• Aandaa hoja binafsi bungeni kutaka zirejeshwe

na Rodrick Mushi, Rombo




WAKATI serikali ikishindwa kuwataja vigogo walioficha mabilioni ya fedha nchini Uswisi, Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA), Zitto Kabwe, anatarajia kuwasilisha hoja binafsi katika mkutano wa tisa unaotarajiwa kuanza wiki ijayo mjini Dodoma, kutaka serikali irejeshe fedha hizo.

Zitto ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, amesema tayari hoja hiyo imeshapata baraka za Spika wa Bunge, Anne Makinda.

Mbunge huyo wa CHADEMA alisema hayo jana wakati wa akifunga mkutano wa kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani wa Kata ya Nanjarareha, wilayani Rombo, mkoani Kilimanjaro.

Katika uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika leo, CHADEMA imemsimamisha, Frank Salakana. Alisema sh bilioni 349 zilizofichwa Uswisi na baadhi ya vigogo wa serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM), lazima zirejeshwe nchini, huku akimtaka Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Edward Hosea, kueleza umma barua aliyoituma nchini humo kwa ajili ya kashfa hiyo ilikuwa na lengo gani.

Alisema barua ya Dk. Hosea imesababisha ugumu wa upatikanaji wa taarifa za mabenki ya nchini Uswisi ambayo yameshindwa kutoa ushirikiano kwa kamati inayofuatilia kashfa hiyo.

Huku akishangiliwa na maelfu ya wanachama wa CHADEMA waliofurika kusikiliza mkutano huo, Zitto alisema wizi wa mabilioni hayo umetokana na kuporomoka kwa maadili ya viongozi nchini ambao wengi wanajali zaidi masilahi binafsi badala ya umma.

Mbunge huyo machachari wa CHADEMA, alisema kuna haja kama taifa kurejesha maadili ya uongozi kama enzi za utawala wa Mwalimu Nyerere ili viongozi wachague kitu kimoja, kati ya biashara na siasa.

Alisema CHADEMA imepania kuhakikisha mabilioni hayo yanarejeshwa ili yaweze kutumika kuwasaidia Watanzania katika kujenga na kuboresha miundombinu ya barabara, maji na afya.

Aliwataka viongozi walioficha mabilioni hayo kujitokeza mapema na kueleza jinsi walivyozipata badala ya kusubiri kuumbuliwa.

“Nawataka viongozi waliohusika wajitokeze wenyewe, waeleze walivyozipata na kisha wazirejeshe nchini, vinginevyo patachimbika, kwani nitahakikisha kama chama tunashirikiana na Benki ya Dunia kuhakikisha fedha hizo zinarudi nchini,” alisema Zitto.

Alisema CHADEMA inapigania fedha hizo zirejeshwe kwani zimetokana na wizi wa rasilimali za Watanzania kupitia mikataba mibovu ya mafuta na wizi wa madini na nyingine.

Katika ripoti ya Swiss Central Bank, iliyotolewa hivi karibuni, inaonesha kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi 11 barani Afrika ambazo vigogo wake wa kibiashara, kitawala na kisiasa wameficha kwa siri mabilioni ya fedha katika mabenki ya Uswisi.

Nchini nyingine za Afrika zilizoficha fedha hizo ni Kenya, Uganda, Zimbabwe, Misri, Shelisheli, Afrika Kusini, Rwanda, Sierra Leone, Somalia na Sudan.

Kwa upande wa Tanzania, mapesa ambayo yamefichwa huko ni dola milioni 196.87, sawa na shilingi za Tanzania bilioni 315.5!

Hebu jiulize; mapesa haya tuliyoibiwa yangetusaidia kiasi gani kama yangerejeshwa nchini na kutumbukizwa kwenye miradi ya kuboresha huduma za jamii?

Pia jiulize swali jingine: Je, hata baada ya Benki Kuu ya Uswisi kuturahisishia mambo kwa kututobolea ukweli kwamba tumeibiwa, na kwamba wezi wetu wameficha hizo fedha nchini mwao, watawala wetu wana dhamira ya kuanzisha mchakato ili wahusika wafikishwe mahakamani na fedha hizo zirejeshwe nchini?

Monday, October 22, 2012


MAHAFALI YA KIDATO CHA NNE SEKONDARI YA MAMA CLEMENTINA WAZAZI NA WAPEWA SOMO.


Mwenyekiti wa shirika la mama clementina Foundation akitoa nasaha zake kwenye mahafali hayo.

Mkuu wa Wilaya ya Bahi,Betty Mkwasa akimkabidhi mmoja wa wahitimu zawadi.

                                                                     
                                                 Rodrick Mushi,Moshi.
Kutokana na tatizo la uhaba wa wataalamu wa  fani zinazohitaji masomo ya sayansi nchi jitihada mbali mbali imeelezwa kuwa zinahitaji kuanzia kwa wazazi kushirikiana na waalimu katika kuwashauri wanafunzi kuchagua  michepuo ya kusoma ili kusaidia kuondokana na tatizo hilo.
Akizungumza kwenye mahafali ya kidato cha nne ya shule ya sekondari Mama Clementina Foundation mwenyekiti wa shirika la Mama Clementine Foundatin  Maria Josephine alisema nchi ina tatizo la wataama kama Madaktari,mafamasia,wataalamu wa kilimo,wahasibu,maafisa biashara pamoja na fani nyingin zinazohitaji elimu ya sayansi.
Alisema kuwa wanafunzi wengi wamekuwa wakisoma masomo ambayo inakwua rahisi kwao kuweza kufaulu huku akitolea mfano michepuo kama ya Mahusiano ya Umma,Maendeleo ya Jamii utawala na michepuo mingine huku uhaba ambao umekuwa wa wataalamu ukiendelea kuongezeka.
Maria Alisema kuwa kutokana na tatizo hilo kuwa kubwa mikakati mbalimbali inahitajika ikiwa ni pamoja na kuinua na kuyapa kipaumbelea masomo ya sayansi na biashara,na wazazi kuwa karibu kuwaeleza faida za kuchukua michepuo hiyo ambayo pia imekuwa na nafasi kubwa ya ajira.
“Tatizo linalokabili nchi yetu ni tatizo la uhaba wa wataalamu,na wataalamu wanaohitaji ni muhimu na ili nchi iendelee lazima Nyanja hizo wawepo wataalamu wa kutosha hivyo suala hilo Serikali na wadau wengine kama wazazi na waalimu wanapaswa kushiriana kulimaliza”Alisema
Katika hatua nyingine alisema tatizo hilo linanzia mashuleni kwa wanafunzi kushindwa kufanya vizuri katika masomo ya sanyansi kama phisikia,kemia baologia na hesabu huku idadi ya wanaoshidnwa kufanya vizuri wakiwa ni wasichana,ambapo wanafuzni ambao wamekuwa wakifanya vizuri ni wale wanaosoma shule binafsi.
Kwa upande wake Mgeni rasmi kwenye mahafali hayo Mkuu wa Wilaya ya Bahi Betty Mkwasa alitoa wito kwa wamiliki wa shule binafsi kuwa na tabia ya kujitolea kuwasomesha baadhi ya watoto ambao wazazi hawana uwezo au yatima kama ambavyo shule hiyo ya mama Clementina imekuwa ikifanya.
“Kuna wamiliki wa shule binafsi ambao wamewasahau kabisa watoto maskini lakini ukweli ni kwamba ukimsaidia maskini utapa Baraka kwa Mungu lakini pia umesaidia kujenga taifa kwani motto mmoja unayemsaidia anaweza kuja kuikomboa jamii yake”Alisema Mkwasa.
                                                                         Mwisho


*Kupungua kwa samaki pamoja na kufungwa kwa shughuli za uvuvi bwawa la Nyumba ya Mungu kwatishia maisha ya wananchi wanaozunguka bwawa hilo kiuchumi.

                                                           


                                                          Rodrick Mushi.
Kupungua kwa samaki katika bwawa la nyumba ya Mungu kumefanya maisha ya wakazi hao kuwa magumu,kutokana na kutegemea bwawa hilo kujiingizia kipato ambacho kinawasaidia kujikimu kimaisha.
Mkazi wa Kijiji cha Njia Panda Wilayani Mwanga  Peter Msangi anasema kuwa wakazi wa Vijiji vinavyozunguka bwawa hilo vya Kiti cha Mungu,Nyabinda,Kagongo na Langata Bora wote wanategemea kuendesha maisha yao kwa kutumia bwawa hilo.
Anaeleza kuwa wananchi hao hawana njia nyingine mbadala ya kuweza kujipatia kipato tofauti na biashara hiyo ya uvuvi,hivyo ikitokea bwawa hilo kutoweka na wao hawataweza kuishi.
Msangi anasema wakazi wa maeneo yanayozunguka eneo la bwawa kwa ujumla hawana ardhi kwa ajili ya kulima,na iliyopo kidogo ina mawe ambayo haifai kwa kilimo.
Wakazi wengi wanasema kuwa licha ya Serikali kukataza wavuvi kuvua kwa kutumia nyavu zenye matundu chini ya nchi tatu lakini wamekiri kushindwa kufanya hivyo kwani wakitumia matundu makubwa watakuwa hawaambulii kitu.
Mvuvi mwingine aliyejitambulisha kwa jina moja la James anasema kuwa kuvuliwa kwa muda mrefu kwa samaki kwenye bwawa hilo kwa kutumia nyavu ndogo maarufu kama kokoro kumechangia kutoweka kwa samaki wakubwa hali inayochangiwa na kutokuwa na muda wa kuacha samaki hao wakue.
“Wakazi wote tunaozunguka bwawa hili hatuna sehemu nyingine ya kutegemea kupata kipato,hata sisi hatupendi kutumia makokoro, lakini hatuna njia nyingine ya kuishi. Sisi tufanyaje?Alisema James.
Anasema kuwa shughuli za uvuvi kwenye bwawa hilo walianza tangu mwaka 1980,kipindi ambacho hali ya samaki katika bwawa hilo ilikuwa nzuri,kwa upatikanaji wa samaki wakubwa na maji ya kutosha.
Wapo wananchi wanaotupia lawama Serikali kwa kushindwa kudhibiti uvuvi huu haramu,kwa mamlaka husika kusimamia vyema sheria ya uvuvi,kutokana na uvuvi haramu kuendelea kushamiri kila kukicha.
Bwawa la nyumba ya Mungu linazungukwa na Wilaya za Moshi na Mwanga kwa Mkoa wa Kilimanjaro,na Wilaya ya Simanjiro kwa Mkoa wa Manyara,ambapo takribani vijiji 11 vinazunguka bwawa hilo kutoka kwenye Wilaya hizo.
Hitaji la wananchi ni kubwa kwani vijiji vyote nilivyotaja hapo juu vinategemea bwabwa hilo kwa ajili ya kujikimu na wanavua samaki mchana na usiku kama njia ya kujipatia kipato.
Hivyo utaona jitihada za Serikali katika kuokoa kutoweka kabisa kwa samaki kwenye bwawa hili zinahitajika ili kunusuru maisha ya wakazi wanaotegema bwawa hili kwa hapo baadae.
Kilichochangia kupungua kwa samaki
Wananchi wanaozunguka bwawa la nyumba ya mungu wanakiri kuwa wanashiriki katika uvuvi haramu,hi ni kutokana na kutokuwa na njia nyingine mbadala ya kujiingizia kipato.
Daudi Hamisi ambaye ni mvuvi wa muda mrefu anasema kuwa madhara yaliyopatikana kutokana na wao kuendelea kuvua kwa kutumia makokoro ni pamoja na bwawa hilo kutokuwa na samaki wakubwa kama kipindi cha nyuma.
 “Wananchi wanaozunguka bwawa hili wanaendelea kuvua,wapo wanaotoka maeneo mengine nao wanavua,hadi hali sasa imekuwa mbaya kwani wanachovua ni dagaa siyo samaki tena”Alisema.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na taasisi  ya Uvuvi Tanzania(TAFIRI)kwenye bwawa hilo walibaini kuwa endapo wavuvi wangeweza kutumia nyavu zenye macho makubwa kuanzia nchi tatu samaki hao wangepata muda wa kukua.
Utafiti huo unasema kuwa hali hiyo imechangia kupungua kwa samaki waliovunwa na kurekodiwa katika vitabu vya maafisa uvuvi kufika wastani wa tani 1,770,kwa mwaka badala ya tani 5,173.
Hali hiyo inadhihirisha kuwa uvuvi haramu ulivyochangia kupungua kwa samaki kwenye bwawa hilo,ambapo jitihada za makusudi zisipofanywa na Serikali ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa wakazi wanaozunguka bwawa kuwaelimisha umuhimu wa kuachana na uvuvi huo huenda samaki zikatoweka kabisa.
Sheria za uvuvi,zinaeleza wazi juu ya utaratibu uliowekwa wa usajili wa vyombo vya kuvulia na kupewa leseni kwa ajili ya kulipa ushuru pamoja na kupatiwa vibali.
Kwenye bwawa hilo kuna vyombo zaidi ya 921 vinavyofanya kazi ya uvuvi,lakini vyombo 329 ndio vimesajiliwa huku vyombo 592 vikifanya kazi hiyo bila kufuata taratibu ikiwemo uvuvi haramu.
Wavuvi wanaojishughulisha na uvuvi kwenye bwawa la nyumba ya Mungu 654 pekee ndio waliosajiliwa kati ya wavuvi 2800 hivyo utaona kuwa wavuvi 2146 wanafanya shughuliza za uvuvi pasipo kusajiliwa na moja kwa moja wao ndio wamekuwa wakishiriki kwenye uvuvi haramu.
Hivyo kwa namna moja ama nyingine kutokufuatwa kwa sheria kwa wavuvi pamoja na Serikali kulegalega kwa mamlaka zilizopewa rungu la kusimamia sheria za uvuvi nao wanachangia kuendelea kuwepo kwa uvuvi haramu kwenye bwawa hilo.
Adhari za kupungua kwa samaki.
Kilio kikubwa cha wananchi wanaozunguka bwawa la nyumba ya Mungu ni kukosa njia nyingine mbadala ya kujipatia kipato ukiondoa shughuli za uvuvi.
Wanasema kuwa kufungwa kwa bwawa hilo pamoja na kupungua kwa samaki kumekuwa pigo kubwa kwao,kwani uvuvi ndio unaowezesha wao kuwasomesha watoto na majukumu mengine muhimu ya kifamilia.
Mnale Qamang(45) ambaye ni baba wa familia ya watoto watatu anasema kuwa maendeleo aliyonayo yanatokana na biashara hiyo ya uvuvi ambayo ameweza kulea familia pamoja na kuwasomesha watoto.
Anasema kuwa hali sasa imebadilika,wapo wananchi ambao wanaona maisha yamegeuka machungu baada ya samaki kupungua kwenye bwawa la nyumba ya Mungu kutokana na kuwa msaada mkubwa kwao.
Anasema kuwa yeye alikuwa anaweza kupata shilingi 40,000 hadi 60,000 kutokana na shughuli za  uvuvi ambapo baada ya kufungwa kwa bwawa hilo pamoja na uvivu haramu hali imebadilika kwa kiasi kikubwa.
“Kwa kweli sisi wavuvi hatuna tabia ya kuhifadhi fedha ukipata 50,000 au 80,000 unaitumia yote kwa siku moja au mbili kutokana na bwawa unaliona hapa kila siku lakini kwa kweli hali imebadilika sana na maisha yetu yameanza kuwa magumu”Alisema
Qamang anasema kuwa wameshakutana na viongozi mbalimbali wa Serikali baada ya hali ya uvuvu  kuwa mbaya wakiwaeleza vilio vyao lengo likiwa ni jinsi gani wanaweza kuwasaidia kusajili vikundi vyao na kuanzisha miradiu mbalimbali .
Anasema kuwa licha ya wavuvi kuvua kwa siri baada ya shughuli za uvuvi kufungwa lakini wanachoambulia ni dagaa yaani watoto wa samaki kutokana na kuwepo kwa uvuvi haramu kwa muda mrefu pamoja na uvuvu uliopitiliza.
Je Serikali imeshindwa kudhibiiti uvuvi haramu?
Wataalamu mbalimbali kutoka Mikoa ya Arusha,Manyara,na Kilimanjaro walioketi agosti 09 mwaka jana walipendekeza kufungwa kwa shughuli za uvuvi kwenye bwawa hilo kutokana na hali mbaya inayolikabili.
Kikao hicho ambacho kiliwahusiha  maafisa uvuvi kutoka Mkoa wa Kilimanjaro Mgalula Lyoba,Emanuel Mao Manyara na Maria Kalinga pamoja na wataalamu wengine walipitisha kwa pamoja rasimu ya kupendekeza kufungwa kwa bwawa na kusimamishwa kwa shughuli zozote zile.
Wataalamu hao wanapendekeza kuwa,kwa kipindi chote ambacho bwawa hilo litakapokuwa limefungwa kutatakiwa kufanyika kwa ulinzi wa kutosha kwa kushrikisha maafisa uvuvi kufanya doria za majini na nchi kavu kwa muda wote bwawa hilo litakuwa limefungwa.
Kufunga kwa bwawa hilo kunaelezwa kuwa kutasaidia kutoa nafasi kwa samaki wanaopatikana kwa sasa kuweza kukua,na kuzaliana ili kusaidia kkuongezeka kwa idadi ya samaki.
Mkuu wa Wilaya ya Mwanga,Shaibu Ndemanga anasema kuwa bwala hilo lilifungwa tangu mwezi machi mwaka huu kutokana na hali mbaya inayosababishwa na uvuvi haramu.
Anasema amekwishapokea malalamiko kutoka kwa wananchi kutokana na kutegemea bwawa hilo kujipatia kipato,pamoja na wao kutokuwa na njia nyingine ya kuwaingizia  kipato.
Ndemanga anasema mahitaji ya uvuvi ni makubwa,(fish pressure)na hayaendani na samaki wanaopatikana bwawa hilo hadi walipoamua kulifunga kwa muda.
Anasema kuwa kutokana na uvuvi haramu uliokuwa unaendelea kwa kasi kwenye bwawa hilo,Serikali iliamua kulifunga ili kutoa fursa kwa samaki waliopo kuweza kuzaliana na kukua.
Licha ya kufungwa kwa bwawa hilo lakini utafiti uliofanywa na mwandishi wa makala hii ulibaini kuendelea kuwepo kwa uvuvi haramu,kutokana na kutokuwepo kwa ulinzi wa kutosha.
Uchunguzi huo umebaini kuwa,wavuvi zaidi ya 100-120 waendelea kuvua kwa kuvuka hadi kwenye Wilaya za Simanjiro kwenye vijiji vya ngorika,nyumba ya Mungu na magadini,na kuvua samaki wachanga ambao huwauzia wafanyabishara samaki wanazovua.
Mkuu wa Wilaya anakiri kupokea taarifa za uvuvi huo unaoendelea,ambapo samaki zinazovuliwa zinanunuliwa na wafanyabishara na kuuzwa kwenye masoko ya mbalimbali ya Kilimanjaro na Arusha.
Naye Mbunge Mbunge wa Jimbo la Mwanga,Jumanne Magembe,anasema kuwa uvuvi haramu ndio umechangia kwa kiasi kikubwa,kuendelea kutoweka kwa samaki kwenye bwawa hilo.
Magembe ambaye ni Waziri wa Maji anasema kuwa kinachochangia  kuendelea kuwepo kwa  uvuvi haramu ni kutokana na kutokuwepo kwa nguvu ya kutosha kulinda bwawa hilo kwa kipindi ambacho litakuwa limefungwa ili kuruhusu kukua kwa samaki.
Anasema kuwa yeye hakubaliani na wananchi wanaodai hawawezi kusitisha shughuli hizo za uvuvi kwa miezi michache litakapokuwa linafungwa,kwani wapo wakulima wanaolima kwa msimu na wanaendelea kuishi.
“Kufungwa kwa mabwawa na maziwa ni taratibu zilizopo na zinajulikana kwa sababu zinasaidia mfano ni kwamba samaki anaweza kukua kwa gramu 400 kwa siku 90,hivyo kusimamishwa kwa shughuli za uvuvi kutasaidia kama kukiwepo ulinzi wa kutosha”Alisema Magembe.
Bwawa la Nyumba ya Mungu lina ukubwa wa kilomita za mraba 140,ambapo shughuli za uvuvi zilianza tangu ,mwaka 1970,ukifanywa na wavuvi wahamiaji baada ya kupungua kwa uvuvi kwenye ziwa jipe.
Mbali na shughuli za uvuvi lakini bwawa la nyumba ya Mungu lilianzishwa likiwa na malengo mahsusi ya kuzalisha umeme(generation of hydro-electric power)tangu mwaka ,1965 ambapo huzalisha hadi megawati 8 kukukiwa na hali nzuri ya upatikanaji wa maji lakini kwa sasa zinazalishwa megawatt 3,kutokana na bwawa hilo kuwa na kina kidogo cha maji.
Mwisho

RAIS KIKWETE KATIKA KILELE CHA MKUTANO MKUU WA UWT DODOMA

Mwenyekiti wa CCM Rais Jakaya Mrisho Kikwete akihutubia katika ukumbi wa Chuo cha Mipango mjini Dodoma kufunga mkutano mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT)
Rais Jakaya Kikwete akiwa jukwaa kuu na viongozi mbalimbali wa chama katika mkutano wa UWT mjini Dodoma leo
Wanachama wakongwe wa UWT na CCM wakishangilia
Wanachama wakongwe wa UWT na CCM wakishangilia
Sehemu ya wajumbe wa mkutano mkuu wa UWT wakirushwa na Sizya Mazongela wa kundi la Segere
Mwenyekiti wa CCM Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiongea na Mwenyekiti wa UWT  Sophia Simba na Katibu Mkuu Amina  Makilagi katika ukumbi wa Chuo cha Mipango mjini Dodoma baada ya kufunga mkutano mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT)
Mwenyekiti wa CCM Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwasili katika ukumbi wa Chuo cha Mipango mjini Dodoma kufunga mkutano mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT)
Picha na habari kwa hisani ya John Bukuku blog.