Tuesday, May 29, 2012

WATU 30 WAPANDISHWA KIZIMBANI ZANZIBAR KWA KUDAIWA KUHUSIKA NA VURUGU NA KUHARIBU MALI


Na Juma Mohammed,MAELEZO Zanzibar
Watu 30 wakiwemo wanaosadikiwa kuwa  wafuasi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislam  wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Mwanakwerekwe  wakikabiliwa na makosa mbalimbali ikiwemo kuwashambulia Polisi,kuchoma moto matairi ya Magali barabarani na ukorofi.
Mbali na tuhuma hizo,pia wameshtakiwa kwa kufanya maandamano yasiyokuwa na kibali kinyume na sheria  pamoja na  uzembe na ukorofi wa kuwashambuliya polisi kwa mawe.
Watuhumiwa hao walifikishwa katika mahakama nne tofauti, ikiwemo mahakama ya hakimu Mohammed Ali Mohammed walikofikishwa watuhumiwa wawili, wanne kwa hakimu Janet Nora Sekihola, 11 kwa hakimu Omar Mcha Hamza na 11 waliobakia, wamepandishwa mbele ya hakimu Valentine Andrew Katema.
Kwa nyakati tofauti watuhumiwa hao walishitakiwa kwa makosa ya kufanya mikusanyiko isivyo halali, uzembe na ukorofi pamoja kufanya kitendo kinachoweza kuleta uvunjifu wa amani.
Watuhumiwa hao ni Mbarouk Said Khalfani (45), na Mussa Juma Issa (57) wanaodaiwa kuwa ni viongozi wa Jumuiya hiyo, ambapo walifikishwa mbele ya hakimu Mohammed Ali Mohammed, na kusomewa shitaka la kufanya mkusanyiko isivyo halali kinyume na kifungu cha 55 (1) (2) (3) na kifungu cha 56 cha sheria namba 6/2004 sheria za Zanzibar.
Wengine ni Mbwana Hamadi Juma (50), Massoud Hamadi Mohammed (17), Mohammed Juma Salum (35), Abdulrahman Simai Khatib (19), Hashim Juma Issa (54) Matar Fadhil Issa (54).

No comments:

Post a Comment