*Kupungua kwa
samaki pamoja na kufungwa kwa shughuli za uvuvi bwawa la Nyumba ya Mungu
kwatishia maisha ya wananchi wanaozunguka bwawa hilo kiuchumi.
Rodrick
Mushi.
Kupungua kwa samaki katika bwawa la
nyumba ya Mungu kumefanya maisha ya wakazi hao kuwa magumu,kutokana na
kutegemea bwawa hilo kujiingizia kipato ambacho kinawasaidia kujikimu kimaisha.
Mkazi wa Kijiji cha Njia Panda Wilayani
Mwanga Peter Msangi anasema kuwa wakazi wa Vijiji vinavyozunguka bwawa
hilo vya Kiti cha Mungu,Nyabinda,Kagongo na Langata Bora wote wanategemea
kuendesha maisha yao kwa kutumia bwawa hilo.
Anaeleza kuwa wananchi hao hawana njia
nyingine mbadala ya kuweza kujipatia kipato tofauti na biashara hiyo ya
uvuvi,hivyo ikitokea bwawa hilo kutoweka na wao hawataweza kuishi.
Msangi anasema wakazi wa maeneo
yanayozunguka eneo la bwawa kwa ujumla hawana ardhi kwa ajili ya kulima,na
iliyopo kidogo ina mawe ambayo haifai kwa kilimo.
Wakazi wengi wanasema kuwa licha ya
Serikali kukataza wavuvi kuvua kwa kutumia nyavu zenye matundu chini ya nchi
tatu lakini wamekiri kushindwa kufanya hivyo kwani wakitumia matundu makubwa
watakuwa hawaambulii kitu.
Mvuvi mwingine aliyejitambulisha kwa
jina moja la James anasema kuwa kuvuliwa kwa muda mrefu kwa samaki kwenye bwawa
hilo kwa kutumia nyavu ndogo maarufu kama kokoro kumechangia kutoweka kwa
samaki wakubwa hali inayochangiwa na kutokuwa na muda wa kuacha samaki hao
wakue.
“Wakazi wote tunaozunguka bwawa hili
hatuna sehemu nyingine ya kutegemea kupata kipato,hata sisi hatupendi kutumia
makokoro, lakini hatuna njia nyingine ya kuishi. Sisi tufanyaje?Alisema James.
Anasema kuwa shughuli za uvuvi kwenye
bwawa hilo walianza tangu mwaka 1980,kipindi ambacho hali ya samaki katika
bwawa hilo ilikuwa nzuri,kwa upatikanaji wa samaki wakubwa na maji ya kutosha.
Wapo wananchi wanaotupia lawama
Serikali kwa kushindwa kudhibiti uvuvi huu haramu,kwa mamlaka husika kusimamia
vyema sheria ya uvuvi,kutokana na uvuvi haramu kuendelea kushamiri kila
kukicha.
Bwawa la nyumba ya Mungu linazungukwa
na Wilaya za Moshi na Mwanga kwa Mkoa wa Kilimanjaro,na Wilaya ya Simanjiro kwa
Mkoa wa Manyara,ambapo takribani vijiji 11 vinazunguka bwawa hilo kutoka kwenye
Wilaya hizo.
Hitaji la wananchi ni kubwa kwani
vijiji vyote nilivyotaja hapo juu vinategemea bwabwa hilo kwa ajili ya kujikimu
na wanavua samaki mchana na usiku kama njia ya kujipatia kipato.
Hivyo utaona jitihada za Serikali
katika kuokoa kutoweka kabisa kwa samaki kwenye bwawa hili zinahitajika ili
kunusuru maisha ya wakazi wanaotegema bwawa hili kwa hapo baadae.
Kilichochangia kupungua kwa samaki
Wananchi wanaozunguka bwawa la nyumba
ya mungu wanakiri kuwa wanashiriki katika uvuvi haramu,hi ni kutokana na
kutokuwa na njia nyingine mbadala ya kujiingizia kipato.
Daudi Hamisi ambaye ni mvuvi wa muda
mrefu anasema kuwa madhara yaliyopatikana kutokana na wao kuendelea kuvua kwa
kutumia makokoro ni pamoja na bwawa hilo kutokuwa na samaki wakubwa kama
kipindi cha nyuma.
“Wananchi
wanaozunguka bwawa hili wanaendelea kuvua,wapo wanaotoka maeneo mengine nao
wanavua,hadi hali sasa imekuwa mbaya kwani wanachovua ni dagaa siyo samaki
tena”Alisema.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na
taasisi ya Uvuvi Tanzania(TAFIRI)kwenye bwawa hilo walibaini kuwa endapo
wavuvi wangeweza kutumia nyavu zenye macho makubwa kuanzia nchi tatu samaki hao
wangepata muda wa kukua.
Utafiti huo unasema kuwa hali hiyo
imechangia kupungua kwa samaki waliovunwa na kurekodiwa katika vitabu vya
maafisa uvuvi kufika wastani wa tani 1,770,kwa mwaka badala ya tani 5,173.
Hali hiyo inadhihirisha kuwa uvuvi
haramu ulivyochangia kupungua kwa samaki kwenye bwawa hilo,ambapo jitihada za
makusudi zisipofanywa na Serikali ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa wakazi
wanaozunguka bwawa kuwaelimisha umuhimu wa kuachana na uvuvi huo huenda samaki
zikatoweka kabisa.
Sheria za uvuvi,zinaeleza wazi juu ya utaratibu
uliowekwa wa usajili wa vyombo vya kuvulia na kupewa leseni kwa ajili ya kulipa
ushuru pamoja na kupatiwa vibali.
Kwenye bwawa hilo kuna vyombo zaidi ya
921 vinavyofanya kazi ya uvuvi,lakini vyombo 329 ndio vimesajiliwa huku vyombo
592 vikifanya kazi hiyo bila kufuata taratibu ikiwemo uvuvi haramu.
Wavuvi wanaojishughulisha na uvuvi
kwenye bwawa la nyumba ya Mungu 654 pekee ndio waliosajiliwa kati ya wavuvi
2800 hivyo utaona kuwa wavuvi 2146 wanafanya shughuliza za uvuvi pasipo
kusajiliwa na moja kwa moja wao ndio wamekuwa wakishiriki kwenye uvuvi haramu.
Hivyo kwa namna moja ama nyingine
kutokufuatwa kwa sheria kwa wavuvi pamoja na Serikali kulegalega kwa mamlaka
zilizopewa rungu la kusimamia sheria za uvuvi nao wanachangia kuendelea kuwepo
kwa uvuvi haramu kwenye bwawa hilo.
Adhari za kupungua
kwa samaki.
Kilio kikubwa cha wananchi wanaozunguka
bwawa la nyumba ya Mungu ni kukosa njia nyingine mbadala ya kujipatia kipato ukiondoa
shughuli za uvuvi.
Wanasema kuwa kufungwa kwa bwawa hilo
pamoja na kupungua kwa samaki kumekuwa pigo kubwa kwao,kwani uvuvi ndio
unaowezesha wao kuwasomesha watoto na majukumu mengine muhimu ya kifamilia.
Mnale Qamang(45) ambaye ni baba wa
familia ya watoto watatu anasema kuwa maendeleo aliyonayo yanatokana na biashara
hiyo ya uvuvi ambayo ameweza kulea familia pamoja na kuwasomesha watoto.
Anasema kuwa hali sasa imebadilika,wapo
wananchi ambao wanaona maisha yamegeuka machungu baada ya samaki kupungua
kwenye bwawa la nyumba ya Mungu kutokana na kuwa msaada mkubwa kwao.
Anasema kuwa yeye alikuwa anaweza kupata
shilingi 40,000 hadi 60,000 kutokana na shughuli za uvuvi ambapo baada ya kufungwa kwa bwawa hilo
pamoja na uvivu haramu hali imebadilika kwa kiasi kikubwa.
“Kwa kweli sisi wavuvi hatuna tabia ya
kuhifadhi fedha ukipata 50,000 au 80,000 unaitumia yote kwa siku moja au mbili
kutokana na bwawa unaliona hapa kila siku lakini kwa kweli hali imebadilika
sana na maisha yetu yameanza kuwa magumu”Alisema
Qamang anasema kuwa wameshakutana na viongozi
mbalimbali wa Serikali baada ya hali ya uvuvu kuwa mbaya wakiwaeleza vilio vyao lengo likiwa
ni jinsi gani wanaweza kuwasaidia kusajili vikundi vyao na kuanzisha miradiu
mbalimbali .
Anasema kuwa licha ya wavuvi kuvua kwa
siri baada ya shughuli za uvuvi kufungwa lakini wanachoambulia ni dagaa yaani
watoto wa samaki kutokana na kuwepo kwa uvuvi haramu kwa muda mrefu pamoja na
uvuvu uliopitiliza.
Je Serikali imeshindwa kudhibiiti uvuvi
haramu?
Wataalamu mbalimbali kutoka Mikoa ya
Arusha,Manyara,na Kilimanjaro walioketi agosti 09 mwaka jana walipendekeza
kufungwa kwa shughuli za uvuvi kwenye bwawa hilo kutokana na hali mbaya
inayolikabili.
Kikao hicho ambacho kiliwahusiha
maafisa uvuvi kutoka Mkoa wa Kilimanjaro Mgalula Lyoba,Emanuel Mao Manyara na
Maria Kalinga pamoja na wataalamu wengine walipitisha kwa pamoja rasimu ya
kupendekeza kufungwa kwa bwawa na kusimamishwa kwa shughuli zozote zile.
Wataalamu hao wanapendekeza kuwa,kwa
kipindi chote ambacho bwawa hilo litakapokuwa limefungwa kutatakiwa kufanyika
kwa ulinzi wa kutosha kwa kushrikisha maafisa uvuvi kufanya doria za majini na
nchi kavu kwa muda wote bwawa hilo litakuwa limefungwa.
Kufunga kwa bwawa hilo kunaelezwa kuwa
kutasaidia kutoa nafasi kwa samaki wanaopatikana kwa sasa kuweza kukua,na
kuzaliana ili kusaidia kkuongezeka kwa idadi ya samaki.
Mkuu wa Wilaya ya Mwanga,Shaibu Ndemanga
anasema kuwa bwala hilo lilifungwa tangu mwezi machi mwaka huu kutokana na hali
mbaya inayosababishwa na uvuvi haramu.
Anasema amekwishapokea malalamiko
kutoka kwa wananchi kutokana na kutegemea bwawa hilo kujipatia kipato,pamoja na
wao kutokuwa na njia nyingine ya kuwaingizia kipato.
Ndemanga anasema mahitaji ya uvuvi ni
makubwa,(fish pressure)na hayaendani na samaki wanaopatikana bwawa hilo hadi
walipoamua kulifunga kwa muda.
Anasema kuwa kutokana na uvuvi haramu
uliokuwa unaendelea kwa kasi kwenye bwawa hilo,Serikali iliamua kulifunga ili
kutoa fursa kwa samaki waliopo kuweza kuzaliana na kukua.
Licha ya kufungwa kwa bwawa hilo lakini
utafiti uliofanywa na mwandishi wa makala hii ulibaini kuendelea kuwepo kwa
uvuvi haramu,kutokana na kutokuwepo kwa ulinzi wa kutosha.
Uchunguzi huo umebaini kuwa,wavuvi
zaidi ya 100-120 waendelea kuvua kwa kuvuka hadi kwenye Wilaya za Simanjiro
kwenye vijiji vya ngorika,nyumba ya Mungu na magadini,na kuvua samaki wachanga
ambao huwauzia wafanyabishara samaki wanazovua.
Mkuu wa Wilaya anakiri kupokea taarifa
za uvuvi huo unaoendelea,ambapo samaki zinazovuliwa zinanunuliwa na
wafanyabishara na kuuzwa kwenye masoko ya mbalimbali ya Kilimanjaro na Arusha.
Naye Mbunge Mbunge wa Jimbo la
Mwanga,Jumanne Magembe,anasema kuwa uvuvi haramu ndio umechangia kwa kiasi
kikubwa,kuendelea kutoweka kwa samaki kwenye bwawa hilo.
Magembe ambaye ni Waziri wa Maji
anasema kuwa kinachochangia kuendelea kuwepo kwa uvuvi haramu ni
kutokana na kutokuwepo kwa nguvu ya kutosha kulinda bwawa hilo kwa kipindi
ambacho litakuwa limefungwa ili kuruhusu kukua kwa samaki.
Anasema kuwa yeye hakubaliani na
wananchi wanaodai hawawezi kusitisha shughuli hizo za uvuvi kwa miezi michache
litakapokuwa linafungwa,kwani wapo wakulima wanaolima kwa msimu na wanaendelea
kuishi.
“Kufungwa kwa mabwawa na maziwa ni
taratibu zilizopo na zinajulikana kwa sababu zinasaidia mfano ni kwamba samaki
anaweza kukua kwa gramu 400 kwa siku 90,hivyo kusimamishwa kwa shughuli za
uvuvi kutasaidia kama kukiwepo ulinzi wa kutosha”Alisema Magembe.
Bwawa la Nyumba ya Mungu lina ukubwa wa
kilomita za mraba 140,ambapo shughuli za uvuvi zilianza tangu ,mwaka
1970,ukifanywa na wavuvi wahamiaji baada ya kupungua kwa uvuvi kwenye ziwa
jipe.
Mbali na shughuli za uvuvi lakini bwawa
la nyumba ya Mungu lilianzishwa likiwa na malengo mahsusi ya kuzalisha
umeme(generation of hydro-electric power)tangu mwaka ,1965 ambapo huzalisha
hadi megawati 8 kukukiwa na hali nzuri ya upatikanaji wa maji lakini kwa sasa
zinazalishwa megawatt 3,kutokana na bwawa hilo kuwa na kina kidogo cha maji.
Mwisho
No comments:
Post a Comment