MONDULI WATAKA KATIBA MPYA
MWENYEKITI WA UVCCM, MONDULI, JUILUS KALANGA
WANANCHI wa Monduli wametakiwa kujitokeza kwenye mikutano ya kukusanya
maoni ya katiba mpya ili waweze kutoa mapendekezo yatakayowawezesha
kunufaika na rasilimali zao ikiwemo misitu na mapori yanayotumika kwa
utalii wa kuwinda.
Hayo yalisemwa na mwenyekiti wa Umoja wa vijana wa Chama cha Mapinduzi
(UVCCM) wilayani humo, Julius Kalanga wakati alipokuwa akiwaeleza
waandishi wa habari maazimio ya kikao cha kamati ya utekelezaji
kilichokaa mwishoni mwa wiki .
Alisema kuwa wilaya hiyo ina misitu na vitalu vya uwindaji wa kitalii
lakini wananchi wake hawanufaiki navyo kwani malipo yote hufanyikia
wizarani jambo alilosema kuwa si sahihi kwani wananchi wanaoishi
kuzunguka maeneo hayo ambao huwa walinzi na hupata athari mbalimbali
ikiwemo wanyama kuvamia mashamba na makazi yao hivyo wanapaswa kupata
sehemu ya mapato.
Kalanga ambaye pia ni diwani wa Nyampulukano alisema kuwa tatizo hilo
linaweza kutatuliwa kwa wananchi kujitokeza kwenye mikutano ya kukusanya
maoni ya katiba mpya ambapo alishauri angalau asilimia 25 mpaka 30 ya
mapato ya uwindaji wa kitalii na uvunaji wa miti kwa ajili ya mbao
yakarudishwa kwa jamii zinazoishi kwenye maeneo kuzunguka vitalu vya
uwindaji na mazao ya misitu.
Aidha Mwenyekiti huyo wa UVCCM alisema kuwa wanamshukuru mbunge wao,
Edward lowassa kwa kuamua kuweka wazi msimamo wake wa kutokihama chama
hicho tawala kwani kabla ya hapo kulitokea sintofahamu kubwa miongoni
mwa wanaCCM ambao wengine walitaka kukihama chama hicho wawahi kule
ambapo waliambiwa mbunge wao atahamia.
Pia walimpongeza Lowassa kwa kufanikiwa kutatua kero za ardhi kati ya
wawekezaji na wananchi wa maeneo ya Mto wa Mbu na Meserani kwa kile
alichoeleza kuwa endapo asingefanya haraka kutafutia ufumbuzi
ingesababisha wananchi wengi kukikimbia chama hicho tawala.
“Kama wananchi wakiona hawawezi kupata haki ndani ya chama chao (CCM)
watatafuta mahali pengine kwa kuipata nje ya chama chao hivyo
tunamshukuru Lowassa kwa kuamua kuishughulikia migogoro hiyo ya ardhi na
ufumbuzi alioupatia jambo lililosababisha wananchi kutulia” alisema
kalanga.
KATIBU WA UVCCM MONDULI, EZEKIEL MOLLEL.
Kwa upande wake katibu wa UVCCM wilayani humo, Ezekiel Mollel alisema
kuwa uchaguzi ndani ya chama hicho umeshindwa kukamilika kwenye baadhi
ya maeneo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ile ya baadhi ya
watendaji wa chama kutotoa fomu za kugombea huku kwenye maeneno mengine
akijitokeza mgombea mmoja.
Alisema kuwa hali hiyo imepelekea mashina 497 kati ya 2,106 wilayani
humo kutofanya uchaguzi na matawi nane kati ya 72 kushindwa kufanya
uchaguzi huo ambapo kwa sasa mchakato wa uchaguzi ngazi ya kata
unaendelea kwa wanaCCM kuendea kuchukua fomu.
Habari na Grace Macha.
No comments:
Post a Comment