Thursday, March 22, 2012

KAMATI YA HESABU ZA SERIKALI ZA MITAA(LAAC) YAIOMBA KURUGENZI YA MASKATA NA TAKUKURU KUONGEZA KASI KATIKA UTENDAJI
 
mwenyekiti wa kamati hiyo Bw Augustine Mrema

KAMATI ya bunge ya hesabu za serikali za mitaa(LAAC) imeiomba ofisi ya
mkurugenzi wa mashtaka nchini(DPP) kuharakisha mchakato wa kuandaa
majalada ya kesi dhidi ya watumishi wa halmashauri za wilaya,jiji na
manispaa nchini ili kuwatendea waliosimamishwa kazi.

Pamoja na DPP lakini pia kamati hiyo imeiomba taasisi ya kuzuia na
kupambana na rushwa nchini(TAKUKURU) kuongeza kasi katika uchunguzi
wake dhidi ya watumishi hao ili wale wabadhirifu wachukuliwe hatua
ikiwa ni fundisho kwa wengine.

Akizungumza na viongozi wa halmashauri za Jiji la Arusha, Arusha na
Monduli mkoani humo,mwenyekiti wa kamati hiyo Bw Augustine Mrema
alisema taasisi hizo pamoja na kufanya kazi nzuri kwa maendleo ya
taifa lakini zinatakiwa kuongeza kasi ya utendaji.

“Kwa namna moja au nyingine hiki kitendo cha taasisi hizi kuchelewa
kutoa maamuzi juu ya majalada ya watumishi waliosimamishwa na wengine
kufukuzwa kazi ni kuchangia ucheleweshaji wa kesi dhidi ya watumishi
wabadhirifu”alisema.

Mwenykiti huyo alisema pia kitendo cha baadhi ya halmashauri kuongozwa
na makaimu wakuu wa idara kwa zaidi ya miaka miwili ni kuwanyima
nafasi ya kufanya maamuzi kwa wakati wakihofia nafasi zao na kwamba
ipo haja kwa suala hilo kurekebishwa.

Mrema alisema ili kuisadia serikali kusimamia halmashauri kuwa na
nidhamu ya matumizi ya fedha za umma,wahisani na wananchi kwa ujumla
ipo haja kwa taasisi hizo kutekeleza wajibu wake kwa wakati ili
kuwatendea haki wanaotuhumiwa.

Mwenyekiti huyo alitolea mfano halmashauri za wilaya ya Monduli ambayo
kuna nafasi 12 za wakuu wa idara muhimu ambazo zinaendeshwa na makaimu
huku pia halmashauri ya jiji nayo ikiwa na nafasi 6 zinazokaimiwa.

Kamati hiyo iliiomba serikali kuhakikisha taasisi zake hizo zinakuwa
mstari wa mbele katika kusukuma halmashauri kutekeleza wajibu wake
jambo ambalo litachochea maendeleo ya haraka katika sekta mbalimbali.

Kwa upande wao wajumbe wa kamati mbunge wa bahi,Bw Omary Badwel na
mbunge wa mtwara mjini ,Bw Hasnain Murji waliomba TAMISEMI kujaza
nafasi zinazokaimiwa katika halmashauri ya Monduli na jiji la Arusha.

Nao mbunge wa viti maalum mkoani Morogoro,bi Suzan Kiwanga na mbunge
wa mbozi mashariki bw godfrey Zambi walisema kuna uzembe wa wakuu wa
idara katika usimamizi wa miradi ya maendeleo.
 
Habari na Dixon Busagaga,Arusha,

No comments:

Post a Comment