Sunday, April 28, 2013

SUALA LA USAFI WA MOSHI LISICHUKULIWE KISIASA...



round about iliyopo Mjini hapa.ambapo watu mbalimbali wanaodondosha uchafu wanakamatwa na kutozwa faini huku kukuwepo na malalamiko ya kunynyaswa kwa kutozwa shilingi 50,000.

baadhi ya wafanyabisshara wadogo maarufu kama machinga wakiwa wamepanga bidhaa zao chini wakisubiri wateja.
baadhi ya soko lilipo nje ya Kata za katikati ya Mji.


Suala la usafi Moshi lizingatiwe

Rodrick Mushi

MANISPAA ya Moshi ni miongoni mwa manispaa zinazoongoza kwa usafi, lakini hivi sasa suala hilo la usafi wa mazingira linakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo ya itikadi za kisiasa.
Kwa upande wa Tanzania, Manispaa ya Moshi ni miongoni mwa manispaa ambazo zimekuwa zikiwavutia wengi, wakiwamo madiwani, wageni mbalimbali kutoka nje na ndani ya nchi kufika na kujifunza jinsi ya kuweka manispaa zao kuwa safi kama Moshi.
Zipo sheria ndogondogo ambazo hutungwa na manispaa ya mji kwa ajili ya kuhakikisha usafi unaendelea kuwapo na watu ambao wamekuwa wakichafua mazingira wanachukuliwa hatua za kisheria pamoja na kutozwa faini.
Kila mgeni anayefika mjini hapa kama ameambatana na mwenzake basi utasikia akimwambia mwenzake, angalia usije ukatupa takataka, ikiwa ni vocha, kichungi cha sigara au kutema mate, kwani utatozwa faini na watu wanaosimamia usafi.
Katika mji huu kuna mawakala wanne ambao ndio waliopewa jukumu la kusimamia usafi wa mazingira, ila kinachonishangaza ni kwamba usafi unaosimamiwa ni Kata ya Kiusa, Kata ya Mawenzi kuzunguka Stendi Kuu, Soko la Kati, Barabara ya Ghala, Barabara ya Mawenzi, maeneo ya Mtaa wa Dar es Salaam, Mawenzi na Posta.
Madiwani wanasema mawakala waliopewa jukumu hilo kwa sasa wamegeuka kuwa magaidi kwani wamekuwa wakiwakamata wananchi na kuwapeleka pasipojulikana na hata wakati mwingine kuwatoza kiasi kikubwa cha pesa kuliko zile zilizowekwa.
Lakini ukweli ni kwamba mawakala waliopewa jukumu la kusimamia usafi wa mazingira wamegeuka miungu watu, kwani hata baada ya baraza kupunguza kiwango cha faini kutoka sh 50,000 hadi sh 10,000 bado waliendelea kutoza kiwango cha sh 50,000 na kudiriki kutoa hata risiti bila woga.
Hivyo kinachochukuliwa na wanasiasa hivi sasa ni kitendo cha baraza la madiwani kuwaondoa mawakala waliokuwa wanasimamia zoezi hilo la usafi wa mazingira na kurudisha manispaa.
Meya wa Manispaa ya Moshi, Japhary Michael, akizungumza kwenye moja ya kikao cha baraza anasema wameamua kuwaondoa mawakala kwa sababu wanawatesa sana wananchi, kibaya zaidi wanawateka wananchi na kuwatoza kiwango kikubwa cha pesa.
Anasema mawakala hao mkataba wao utakwisha Juni 30, lakini hivyo ni vema wakasubiri kwisha kwa mkataba wao ili wasije kuiingiza halmashauri kwenye hasara ya kuwalipa gharama kwa kusitisha mkataba.
Mmoja wa madiwani, Hawa Mushi, anasema kuwa ushahidi upo wa risiti kwa mawakala hao kuwatoza faini kubwa wananchi na kuwapora wananchi mali zao na malalamiko hayo walikwisha kuyafikisha kwa mkurugenzi lakini yanashindwa kufanyiwa kazi kutokana na kampuni hizo za usafi kumilikiwa na  baadhi ya watumishi wa halmashauri.
Kwa mtazamo wangu, ni wakati mwafaka sasa viongozi wa Manispaa ya Moshi kushirikiana kwa pamoja kusimamia usafi wa mazingira ili kuendelea kubakiza heshima ya mji wa Moshi kama ulivyokwisha kujengeka tangu awali badala ya kulaumiana.
Michael anasema kuwa kwa sasa kuna magari yanayozunguka kwenye kata za Manispaa ya Moshi kwa ajili ya kuchukua taka, pamoja na utaratibu uliokwisha kuanzishwa wa madiwani na wenyeviti wa mitaa kufanya usafi kwenye maeneo yao kila mwishoni mwa wiki.
Anasema licha ya jitihada hizo, bado kuna dhana tayari imekwisha kujengeka kuwa mji wa Moshi ni mchafu, na hiyo imetokana na CHADEMA, lengo likiwa ni kuwachonganisha ili wananchi waone kuwa CHADEMA ndiyo chanzo cha mji wao kuwa mchafu.
Kwa mtazamo wangu, lengo la madiwani wa CHADEMA ni kuwanusuru wananchi, kwani tayari kampuni zinazosimamia zoezi hilo zinadaiwa kuwa za vigogo, hivyo ni bora wakatumika askari wa manispaa na mgambo ili amani iendelee kubaki kwa wananchi.

No comments:

Post a Comment