Sunday, June 3, 2012

Lema Amlima JK

*Atoboa siri ya kikao kabla ya Uchaguzi Mkuu(tanzania daima).





                                             
 MBUNGE wa zamani wa Arusha Mjini, Godbless Lema (CHADEMA), amemwandikia Rais Jakaya Kikwete waraka mzito, akimshambulia waziwazi kwamba alihusika kwa namna zote na maamuzi ya Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, yaliyomvua ubunge.

 Katika waraka huo wenye maneno makali na mazito, Lema amemshambulia Rais Kikwete akimtuhumu kutoa maneno aliyoyaita ya kebehi na yaliyodhihirisha jinsi Ikulu ilivyoingilia hukumu ya kesi yake ya ubunge, akidai kuwa ni kumkomoa baada ya kukataa kukubaliana na maombi yake katika kikao cha wawili hao, Oysterbay, jijini Dar es Salaam, siku chache kabla ya uchaguzi mkuu wa 2010.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, akiwa jijini Arusha, Rais Kikwete alikaririwa katika mkutano wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB), akidai kuwa asingekubali kuruhusu mkutano mzito kama huo kufanyika katika jiji hilo miaka miwili nyuma kutokana na kukosekana kwa utulivu.
Hata hivyo, tamko hilo la Rais Kikwete limechukuliwa na mbunge huyo kama lililomlenga yeye, na kumhusisha na fujo, hatua iliyomfanya kumwandikia waraka mzito uliosambazwa katika vyombo vya habari.
Lema amedai kwamba tamko hilo la rais, ni ushahidi mwingine wa waziwazi wa jinsi mamlaka zilivyoweka mkono wake, pamoja na kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo aliyoitoa wakati akiwaapisha wakuu wa wilaya ya kumshukuru jaji aliyetoa hukumu ya kesi yake.
“Natambua wewe ni rais na unayo mamlaka makubwa katika taifa hili lakini vile vile nataka utambue kuwa huna mamlaka makubwa dhidi ya haki, utu na ukweli.
“Umefurahia sana mkutano uliokupa fursa ya kutoa maneno ya kebehi na kudhihirisha hila iliyofanywa na serikali yako… hata hivyo wakati huu kuna mambo ya msingi ya kushughulikia zaidi ya kebehi na hadaa, 
 uchumi wa nchi umeyumba, huduma za msingi za jamii zimepuuzwa, mpasuko katika suala la Muungano na vururugu zinazoendelea Zanzibar, mfumuko wa bei, hizi ni sababu chache ambazo haziwezi kuruhusu wakati huu kuwa wakati wa kebehi na mizaha isipokuwa kazi,” amesema Lema katika waraka huo.
Lema amedai kuwa, Mama Theresa, Nelson Mandela, Martin Luther Jr na Malcom X hawakuwa wabunge walipokuwa wakipigania haki za nchi zao na watu wao, hivyo, na yeye hahitaji ubunge kupigania ukweli, haki na utu.
“Nahitaji dhamira safi, nia njema na huu utakuwa wajibu wangu mpaka nakwenda kaburini. Nitakapomaliza mbio hizi najua nitapata fursa ya kutazama nyuma yangu nione nini nilifanya; ukweli nisingependa kuona vituo vya mafuta, maghorofa, magari na viwanja vingi kila kona ya nchi bali haki, usawa na utu vikiwa kama nguzo ya imani ya watawala wetu watakaokuwepo,” alisema na kuongeza:
“Pengine sitaishi miaka mingi sana kama utachukizwa sana na waraka wangu huu, kwani Polisi, Usalama wa Taifa na Jeshi la Wananchi wanakutii wewe, hata hivyo siogopi kufa kwani nisipokufa kesho, nitakufa siku moja ambayo siijui, napenda kuishi maisha marefu nimwone mke wa mtoto wangu kama itawezekana, lakini kuliko iwezekane kwa kuishi kwa hofu ni bora ishindikane.”
Lema amedai kuwa huenda bado Rais Kikwete ana hasira alizodai zinaweza kuwa zimetokana hasa na mkutano; “tuliokaa Oysterbay Dar mimi na wewe kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, hata hivyo, sikupuuza maongezi yetu isipokuwa nilichagua kufuata dhamira yangu na wito wangu wa utumishi wa kweli katika jimbo langu na nchi yangu,” amesema.
     

No comments:

Post a Comment