MAHAKAMA KUU KANDA YA ARUSHA YAAMURU WAKILI MWALE AREJESHEWE MAGARI YAKE.

Akisoma hukumu hiyo kwa zaidi ya
saa 1,Jaji wa mahakama kuu kanda ya Arusha, Kakusulo Sambo alisema kuwa
mahakama imetafakari kwa kina hoja za pande zote mbili na kubaini kuwa
kimsingi rufaa iliyokuwa imefunguliwa na upande wa serikali ikiongozwa na
mawakili wake,Neema Ringo na Fredrick Manyanda walikurupuka kwani hawakuwa
wamesoma vipengele vya sheria ipasavyo
ili kujiridhisha kabla ya kufungua
rufaa hiyo.
Jaji Sambo alisema kuwa kati ya
mapingamizi manne yaliyowekwa na wakili Mwale,pingamizi la pili lilidai
kwamba ,maombi yaliyowasilishwa mahakamani na serikali ,hayana sifa ya
kuwepo kwa kuwa yameletwa chini ya kifungu ambacho sicho na hakipo chini ya
sheria zilizotungwa na bunge la jamhuri ya muungano Tanzania.
Alisema pingamizi hilo pekee
lilitosha kutoa maamuzi madogo katika rufaa ya serikali,kwani lilibeba
mapingamizi mengine yaliyobaki kutokana na uzito wa kipekee uliochukuliwa
na mahakama .
Awali alisema kuwa,maombi yaliyowasilishwa
mahakamani hapo na mawakili wa serikali,Fredrick Manyanda na Neema Ringo
juu ya kupinga maamuzi ya hakimu Charles Magesa wa mahakama ya hakimu
mfawidhi,Arusha hayakuwa sahihi na yalijaa upungufu wa baadhi ya
viambatanisho vinavyoweza kuishawishi mahakama .
Jaji sambo alisisitiza kwa kuwataka
mawakili wa serikali kusoma zaidi na kuvipitia mara kwa mara vifungu vya
sheria na kuacha kukurupuka na kudai kuwa mawakili hao wamekuwa wakifanya
makosa kama hilo mara kwa mara ,na mara nyingi amekuwa akiwasihi kupitia
upya vifungu vya sheria kabla ya kuwasilisha shauri mahakamani.
Hata hivyo Jaji Sambo alitumia
muda mwingi kutoa elimu kwa mawakili wa serikali,Neema Ringo na Fredrick
Manyanga kuwa kifungu cha sheria namba 372 walichotumia kupeleka shauri
hilo mahakama kuu ,hawakuwa wamekipitia na kukisoma vizuri ,kwani katika
utetezi wao walidai kuwa kifungu hicho ni sahihi na kilihitaji madogo
madogo.
Alisema kitendo cha mawakili hao
wa serikali kudai kuwa kifungu hicho kilikosewa katika hatua ya uchapishaji
ni hatari sana katika mwenendo mzima wa kesi,na hivyo mahakama haiwezi
kutoa unafuu wowote kwa kutumia
kigezo hicho.
Jaji sambo baada ya hukumu hiyo aliamuru jalada hilo
kurudishwa mara moja katika mahakama ya hakimu mkazi ili kuendelea na kesi
ya msingi inayomkabili wakili Mwale.
Awali mawakili hao
wa serikali walikata rufaa Mahakama Kuu wakitaka ipitie upya maamuzi yaliyofanywa na
mahakama hiyo iliyotoa maamuzi ya magari hayo kukabidhiwa wakili Mwale.
Uamuzi huo
ulitolewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi Magesa, ambaye alisema baada
ya kupitia ushahidi wa pande zote, mahakama yake imeridhika kuwa mamlaka
hizo zilikamata magari hayo kinyume cha sheria ya matunda ya uhalifu
(Proceeds Crimes Act) pamoja na vifungu namba 41 na 44 vya sheria ya
mwenendo wa kesi za jinai.
Magari
yaliyoamriwa na mahakama kurejeshwa kwa Mwale ni T 690 BEW aina ya Range
Rover, T 643 BTS Land Rover Discovery, T 907 BTS BMW, T 118 BRS Cadillac
Escalade, T 499 APX Land Cruiser, T 520 BBJ BMW, ambayo yalichukuliwa
Novemba mosi, pamoja na gari T 660 BCG Toyota Chaser lililokamatwa
Desemba 8, mwaka jana.
No comments:
Post a Comment