Sunday, March 25, 2012

Panga la Serikali kuvishukia vyuo, shule


 Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo Stadi nchini, Philiph Mulugo.


Serikali imesema, itazifunga shule na vyuo vyote ambavyo havijasajiliwa na vile ambavyo havijakidhi vigezo na viwango vya kutoa elimu hapa nchini, ili kulinda hadhi ya elimu ya Tanzania iliyovamiwa na soko holela.

Hayo yamebainishwa na wakati wa akihitimisha kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Mamlaka Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) yaliyofanyika kitaifa kwenye viwanja vya Tangamano jijini Tanga.

Huku akizungumza kwa ukali, Mhe. Mulugo amesema “sekta ya elimu haiwezi kuachwa hivi hivi kama haina mwenyewe, haiwezekani tukawa tunaendesha elimu kwa mfumo holela, hadi kufikia mwanafunzi kuingia sekondari huku hajui kusoma na kuandika”.

Naibu Waziri amesema siku hizi kuna matangazo mengi ya shule na vyuo kwenye vyombo vya habari ambavyo havijasajiliwa, hivyo ameiagiza VETA, kufanya ukaguzi na kuvibaini vyuo hole na kuvifunga ili kulinda hadhi ya elimu yetu.

Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya VETA, Prof. Idrissa Mshoro,  aliwatanga Watanzania kubadili mtizamo wao kuhusu vyuo vya VETA, wakidhani ni kwa ajili ya wale waliofeli darasa la saba au kidato cha nne, VETA  ya sasa inatoa mafunzo kwa wote, na kuna fani mpya ambazo zinahitaji wahitimu walipasi vizuri kuweza kuzimudu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Mhandisi Zebadia Moshi, amewataka wadau wa elimu kujitokeza zaidi katika kuwekeza kwenye kujenga vyuo vya ufundi na kueleza ndilo suluhisho pekee la tatizo la ajira kwa vijana, kwa sababu vijana wakipatiwa elimu ya ufundi, na kuwezeshwa kwa vifaa,  wataweza kujiajiri wenyewe mara tuu wamalizapo chuo.


Maadhimisho hayo ya  wiki moja, yamehusisha maonyesho ya kazi mbalimbali zinazofanywa na vyuo vya VETA nchini na kuhusisha wajasiliamali wadogo wadogo waliowezeshwa na VETA, na yamehitimishwa kwa maandamano maalum ya wadau wa VETA katika viwanja vya Mkwakwani mjini Tanga.

Habari na Mwandishi wetu, Tanga

No comments:

Post a Comment