Sunday, March 25, 2012

IGP Said Mwema.
Wakuu wa Jeshi la Polisi katika nchi wananchama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wameunga mkono juhudi za kuanza Kituo cha Uchunguzi cha Rufaa cha Kanda kwa Masuala ya Uhalifu (RRFC).
‘’ Tunapaswa kufanyakazi kwa kushirikiana kwa manufaa ya wote hapo baadaye,’’ Fabien Ndayishimiye, Mkurugenzi Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Burundi aliwaambia wataalamu wa EAC mjini Bujumbura waliokuwa wanakagua miundo mbinu ya uchunguzi ya jeshi hilo kuona kama inafaa kukiweka kituo hicho cha RRFC nchini humo.
Katika taarifa iliyotolewa na Sekretariati ya EAC, Mkuu wa huyo wa Jeshi la Polisi alisema kwamba kanda ya Afrika Mashariki ni familia moja na kwamba uhalifu wowote unaofanywa katika nchi moja unagusa nchi nyingine.
Kamati ya wataalamu nane wa masuala ya uchunguzi wa uhalifu katika jeshi la Polisi katika kanda  ya Afrika Mashariki ilianza kukagua miundombinu hiyo ya kanda kuanza Machi 8, 2012.
Nchini Rwanda, Mkuu wa Jeshi la Polisi la nchi hiyo (IGP), Emmanuel Gasana aliunga mkono juhusi za EAC za kutaka kuanzisha kituo hicho na kwamba nchi yake inaunga mkono juhudi hizo.
‘’Tunasubiri kwa hamu kuanzishwa kwa kituo bora zaidi ili kudhibiti uhalifu unaojitokeza,’’ alisema katika taarifa yake.
Wakati huohuo IGP wa Tanzania, Saidi Mwema alisema kwamba Tanzania imeshapitisha na kufanya mabadiliko katika jeshi la Polisi, ikiwa ni pamoja na kuweka mitambo ya kisasa ya miundombinu yake ya uchunguzi katika jeshi hilo.
‘’Tunataka kuona watu katika Afrika Mashariki yenye mtangamano wanapata manufaa na kujivunia huduma  zenye weledi za majeshi yao ya polisi,’’ Mwema alisisitiza na kuongeza kwamba ‘’mambo hayo yote yanaungwa mkono kwa dhati na serikali ya Tanzania.’’
 Mwandishi wetu,Arusha.

No comments:

Post a Comment