Viongozi wa muungano CORD wamelalamikia namna matokeo ya kura
yanavyotolewa, huku waangalizi kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki na wa
Soko la Pamoja la COMESA wakitoa ripoti zao za awali.
Huku matokeo ya uchaguzi yakizidi kutiririka kutoka katika kituo cha
kuhesabia kura jijini Nairobi, viongozi wa muungano wa CORD wamelalamika
kwamba utaratibu unaotumiwa kutangaza matokeo hayo unatia shaka.
Kulingana na taarifa iliyosomwa na Kalonzo Musyoka, mgombea mwenza wa
Raila Odinga, viongozi kutoka vyama vinavyounda muungano huo wameowaomba
wafuasi wao kuwa watulivu wakati matokeo yote yanavyosubiriwa.
Kalonzo alisema kuwa bado wana uhakika wa kushinda katika uchaguzi na
akaongeza kuwa endapo watashindwa wako tayari kusalimu amri.
Kauli ya CORD yanakuja wakati ambapo kinara wa mrengo wa Jubilee, Uhuru
Kenyatta, anaonekana kuongoza katika matokeo ya awali yaliyotolewa na
Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).
Hata hivyo, Kenyatta na mpinzani wake wa karibu Odinga wanamenyana
vilivyo huku kila mmoja wao akiwa ametimiza zaidi ya kura milioni mbili.
Katika mkutano na waandishi wa habari, mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi
Bw. Isaack Hassan amewaomba wanasiasa wawe watulivu wakati huu wa
kuhesabiwa kwa kura na akakiri kuwa kulikuwa na hitilafu Fulani za
kimitambo ambazo zilichangia kucheleweshwa kwa matokeo.
Hata hivyo, mgombea mwenza wa muungano wa Jubilee, William Ruto,
alisiifu IEBC kwa kuendeleza shughuli za uchaguzi kwa utaratibu unaofaa.
Ruto amewashukuru Wakenya kwa kujitokeza kwa wingi ili kupiga kura siku
ya Jumatatu.
No comments:
Post a Comment