Picha kwa Hisani ya Maktaba. |
SERIKALI ya Tanzania inahusishwa na vitendo vya ujangili na
uuzaji wa meno ya tembo nje ya nchi.
Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Khamisi Kagasheki
akiongea na waandishi wa habari mara baada ya kumaliza mkutano wake na wadau wa
sekta ya utalii kwenye ukumbi wa hoteli ya Mount Meru jijini Arusha alisema
tatizo hilo limeichafua nchi.
Alisema kwa nchi za Marekani na barani Asia sifa ya Tanzania
kwa suala la ujangili ni mbaya kwa kuwa inahusishwa na vitendo hivyo
vinavyodaiwa kufanywa na baadhi ya watu wa ndani na nje ya nchi.
“Hatuwezi kukubali kubeba sifa mbaya hiyo.. wanatusema sana
wenzetu huko nje…hata wadau wa sekta ya utalii kwenye kikao wamesema…wakihusisha
baadhi ya watendaji wa serikali na mtandao huo”alisema.
Kagasheki alisema mtandao wa ujangili ni mkubwa tena unatumia
silaha za kivita ambazo zinatishia uhai wa askari wa hifadhi hizo na kuwa
tayari mkakati wa kuunganisha nguvu za pamoja umekamilika ili kuhakikisha
wanatokomeza mtandao huo.
“Ni mtandao mkubwa lakini hautatushinda lazima utokomezwe
maana tusipofanya hivyo sifa tulizopata kwa vivutio vyetu kushinda kwenye
mashindano ya vivutio bora vya asili Afrika hautakuwa na maana …lazima tulinde
raslimali hizi zinazochangia pato kuwa kwa taifa”alibainisha.
Aliwaonya baadhi ya watumishi wanaoshirikiana na wahujumu
uchumi kuwa hatua kali zitachukuliwa kwao,huku akisisitiza kuwa wanakusudia
kurekebisha sheria ili ziwe kali kwa wanaokamatwa kwenye makosa hayo.
Kuhusu suala la silaha zinazotumiwa na majangili alisema
zinatishia usalama wan chi kwa kuwa wanatumia silaha kali za kivita ambazo
zinatakiwa kudhibitiwa.
Alikwenda mbali zaidi na kudai kuwa idara yake imejipanga
kusafisha watendaji wasiokuwa waadilifu kwa kuwa baadhi ya wadau wa sekta ya
utalii wameishapoteza imani na idara hiyo kutokana na urasimu wa watendaji
kitendo alichosema atakikomesha mara moja.
Februari 11 mwaka huu Vivutio vya Mlima Kilimanjaro,Bonde la
Ngorongoro na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti zilitangazwa kuwa washindi kwa
vivutio vya maajabu saba ya asili.
Mbali na hivyo pia mto Nile kwa Uganda,maporomoko ya
Zambia,Jangwa la Sahara vilikuwa miongoni mwa vilivyoshinda ,mashindano
yaliyoandaliwa na shirika la Seven Natural Wonders of Afrika la Taxes Nchini
Marekani ,ambapo Waziri Mkuu Mizengo Pinda alikabidhi tuzo kwa washindi.
Na Anthony Mayunga-Arusha.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment