Monday, February 18, 2013

CHADEMA KUITIKISA ARUSHA LEO


CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), leo kinafanya mkutano mkubwa wa hadhara Arusha,ambao pia utatumika kuzindua utekelezaji wa sera yake ya utawala wa majimbo kwa kuzindua Jimbo la Kaskazini.
Katibu wa Muda wa Kamati ya Uratibu Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa alisema mkutano huo utafanyika katika Viwanja vya Shule ya Msingi Ngarenaro na utahudhuriwa na wabunge wote wa Chadema kutoka mikoa ya Kanda ya Kaskazini na kuhutubiwa na Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe. Kwa mujibu wa Golugwa, Kanda ya Kaskazini inajumuisha mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro na Tanga.
“Tunazindua Kanda ya Kaskazini kutekeleza uamuzi wa Baraza Kuu lililoagiza mfumo na shughuli za uendeshaji wa chama ushuke hadi ngazi ya majimbo ambayo ndiyo sera ya Chadema,” alisema Golugwa.
Kabla ya mkutano wa leo, viongozi zaidi ya 200 wa Chadema kutoka mikoa na majimbo 30 ya Kanda ya Kaskazini wakiwamo wabunge, wenyeviti, makatibu, wenyeviti na mameya wa Halmashauri zinazoongozwa na Chadema,walifanya vikao vya ndani kuweka mikakati na mfumo wa utendaji kikanda. Kwa mujibu wa Golugwa, ambaye pia ni Katibu wa Chadema wa Mkoa wa Arusha, kikao cha ndani pia kilihudhuriwa na mwasisi na Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho, Mzee Edwin Mtei.
Mbowe ambaye ni mmoja wa wajumbe waliohudhuria vikao vya ndani, ndiye atakuwa mgeni rasmi na mzungumzaji mkuu kwenye mkutano wa hadhara ambao pia utatumika kuwatambulisha wajumbe wa timu ya uratibu ya Kanda ya Kaskazini.
Mkutano huo ni wa pili kwa Chadema ndani ya wiki mbili zilizopita baada ya kufanya mkutano mkubwa Dar es Salaam uliotumika kuueleza umma udhaifu wa mhimili wa Bunge na ukandamizaji  unaodaiwa kufanywa dhidi ya wabunge wa chama hicho na uongozi wa mhimili huo wa dola.
Katika mkutano huo, viongozi wa Chadema waliutangazia umma namba za simu za Spika Anne Makinda na Naibu wake, Job Ndugai ili wananchi wawapigie au kuwatumia ujumbe mfupi kuwashinikiza kufuata Katiba, Sheria na Kanuni za bunge katika uendeshaji na maamuzi ya chombo hicho.

No comments:

Post a Comment