SIMBA YAINGIZA MIL 134/-, AZAM MIL 34/-
PAMBANO la Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya
Simba na Libolo FC ya Angola lililofanyika jana (Februari 17 mwaka huu)
limeingiza sh. 133,795,000 wakati lile la Kombe la Shirikisho kati ya
Azam na El Nasir ya Sudan Kusini lililochezwa juzi (Februari 16 mwaka
huu) limeingiza sh. 34,046,000.
Watazamaji 22,469 walikata tiketi
kushuhudia mechi ya Simba kwa viingilio vya sh. 5,000, sh. 10,000, sh.
15,000, sh. 20,000 na sh. 30,000. Simba ilipoteza pambano hilo kwa bao
1-0.
Mgawo wa mechi hiyo ulikuwa kama
ifuatavyo; gharama za waamuzi sh. 24,926,500, gharama za tiketi sh.
7,410,000, asilimia 15 ya uwanja baada ya kuondoa gharama za waamuzi na
tiketi ilikuwa sh. 15,218,775, asilimia 10 ya Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF) na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) sh.
10,145,850 na asilimia 75 iliyokwenda klabu ya Simba ni sh. 76,093,875.
Mechi ya Azam iliyomalizika kwa
wenyeji kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 ilishuhudiwa na watazamaji
13,431 kwa viingilio vya sh. 2,000, sh. 5,000, sh. 10,000 na sh. 20,000.
Mgawo katika mechi hiyo ulikuwa kama ifuatavyo;
Gharama za tiketi sh. 4,779,000,
asilimia 15 ya uwanja baada ya kuondoa gharama za tiketi ilikuwa sh.
4,390,050, asilimia 10 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) sh. 2,926,700 na asilimia 75
iliyokwenda Prime Time Promotions (Azam) ni sh. 29,267,00.
PONGEZI KWA UONGOZI MPYA SPUTANZA, FRAT
Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) linatoa pongezi kwa uongozi mpya wa Chama cha Wachezaji
Mpira wa Miguu Tanzania (SPUTANZA) na wa Chama cha Waamuzi wa Mpira wa
Miguu Tanzania (FRAT) uliochaguliwa wiki iliyopita.
Uongozi wa FRAT ulichaguliwa
Februari 13 mwaka huu mjini Morogoro wakati wa SPUTANZA ulichaguliwa
jana (Februari 17 mwaka huu) katika uchaguzi uliofanyika Kigamboni, Dar
es Salaam.
Waliochaguliwa kuongoza SPUTANZA
na hawakuwa na wapinzani ni Musa Kissoky (Mwenyekiti) na Said George
(Katibu Mkuu) wakati Ali Mayai aliwashinda Isaac Mwakatika na Hakim
Byemba katika nafasi ya mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF.
Kusianga Kiata na Charles Mngodo
walichaguliwa kuwa wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya SPUTANZA. Katika
uchaguzi huo uliohudhuriwa na wapiga kura 17, Mhazini na nafasi moja ya
mjumbe wa Kamati ya Utendaji zitajazwa baadaye kutokana na kukosa
wagombea.
Kwa upande wa FRAT viongozi
waliochaguliwa ni Said Nassoro (Mwenyekiti), Charles Ndagala (Katibu
Mkuu) na Kamwanga Tambwe (mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF).
Ushindi waliopata viongozi
waliochaguliwa kuongoza vyama hivyo unaonesha jinsi wapiga kura walivyo
na imani kubwa kwao, na TFF inaahidi kuendeleza ushirikiano wake kwa
Kamati ya Utendaji ya FRAT na SPUTANZA.
Uongozi huo mpya una changamoto
nyingi, kubwa ikiwa ni kuhakikisha unaendesha shughuli za mpira wa miguu
kwa kuzingatia katiba zao pamoja na vyombo vya mpira wa miguu vilivyo
juu yao.
Pia tunatoa pongezi kwa kamati za
uchaguzi za FRAT na SPUTANZA na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa
kuhakikisha uchaguzi umeendeshwa kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za
Wanachama wa TFF.
No comments:
Post a Comment