msanii wa filamu Elizabeth Michael maarufu kama lulu akiwa kwenye pozi.
Msanii wa kike wa filamu Tanzania Elizabeth Michael Kimemeta maarufu
kama Lulu,amefikishwa mahakamani akikabiliwa na mashtaka ya mauaji ya
msanii mwingine wa filamu Marehemu Steven Kanumba.
Amefikishwa
mahakamani ikiwa ni siku nne, tangu alipokamatwa mara baada ya kifo cha
msanii huyo ambaye inaaminika kuwa walikuwa na uhusiano wa Kimapenzi.
Mbele
ya Hakimu mfawidhi wa Mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salaam,Bi
Augustina Mbando,Elizabeth Michael Kimemeta ajulikanaye kama Lulu kwa
jina la Usanii,aliwasili mahakamani hapo akiwa chini ya Ulinzi mkali wa
askari Polisi waliokuwa wamevaa kiraia na wengine wakiwa wamejihami kwa
silaha.
Mara baada ya Kufikishwa mahakamani,upande wa mashtaka
ukiongozwa na Wakili wa serikali Bi Elizabeth Kaganda ulimsomea shtaka
moja ambalo ni la mauaji, kosa ambalo ni kinyume cha sheria ya kanuni ya
adhabu kifungu cha 196.
Wakili huyo wa
serikali Bi Elizabeth Kaganda,alidai mbele ya mahakama kuwa mnamo tarehe
07 mwezi April mwaka 2012,katika eneo la Sinza Vatican,msanii Elizabeth
alimuua msanii Steven Kanumba.
Akiwa amevalia gauni kubwa
lijulikanalo kama dera lenye rangi ya Njano mtandio wa rangi ya waridi
na kandambili nyekundu mshtakiwa alionekana kutokuwa na wasi wasi pamoja
uzito wa tuhuma za mauaji anayokabiliwa nayo huku akijibu maswali
kadhaa kuhusu wasifu wake.
Msanii huyo alikanusha kuwa na umri wa
miaka 18 baada ya kuulizwa ,ambapo yeye amesisitiza kuwa ana umri wa
miaka 17, hii ikiwa ni tofauti na habari ambazo zimekuwa zikiripotiwa
kuhusu umri wa msanii huyo ambaye sasa anatambulika kama mshtakiwa.
Kesi hii ya mauaji inatajwa kwa mara ya kwanza na mshtakiwa hakutakiwa kukiri wala kukana mashtaka.
Upande wa mashtaka umeieleza mahakama kuwa kesi bado iko kwenye upelelezi ambapo inatarajiwa kutajwa tena April 23 mwaka huu.
Mshtakiwa amepelekwa rumande hadi siku hiyo wakati kesi hii itakapotajwa tena.
Kwa
upande mwingine tukio la kufikishwa mahakamani kwa mtuhumiwa huyo
kumefanywa kwa usiri mkubwa na kufanya waandishi wa habari wengi
wameshindwa kufuatilia kwa karibu tukio lenyewe.
Kufikishwa
mahakamani kwa msanii huyo na kusomewa shtaka la mauaji ya Kanumba
kumetokea siku moja baada na Marehemu Steven Kanumba kuzikwa katika
makaburi ya Kinondoni.
Mazishi yake yalichukua sura ya kitaifa
kutokana na umaarufu aliojijengea msani huyo katika jamii ya watanzania
na hata nchi za nje
|
No comments:
Post a Comment