Tuesday, June 19, 2012

          M4C yavua magamba wanaccm 70 arumeru Magharibi

HARAKATI za mabadiliko zinazoendeshwa na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kupitia kauli mbiu ‘Vua Gamba Vaa Gwanda’ imezidi kushika kasi mkoani Arusha baada ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) 70 wilayani Arumeru kuamua kukikimbia chama hicho.

Katibu wa Chadema mkoani hapa, Amani Golugwa 
Wanachama hao walipokelewa june 16, mwaka huu na katibu wa Chadema mkoani hapa, Amani Golugwa kwenye ofisi zao za mkoa zilizopo maeneo ya Ngarenaro ambapo viongozi mbalimbali wa mkoa walishiriki akiwemo Mwenyekiti wa BAVICHA , Ephata Nanyaro, Mwenyekiti wa BAWACHA, Ceccilian Ndossi na Mwenyekiti wa Chadema, Arumeru Magharibi.



 Wanachama hao walipatiwa kadi za uanachama huku kiongozi wao, Vivian Lebulu akikabidhiwa katiba ya Chadema, bendera ambapo mwenyekiti wa Bawacha alivisha skafu yenye rangi za chama hicho.


Akiongea kwa niaba ya wenzake, Lebulu alisema kuwa wameamua kuachana na CCM baada ya kuona kwa kipindi kirefu imekuwa madarakani huku ikishindwa kutatua kero za wananchi huku akitolea mfano kwenye jimbo hilo asilimia 35 ya wanafunzi wa shule za msingi hukaa chini kwa kukosa madawati.
Alisema kuwa waliamua kujiunga Chadema ili kushiriki kikamilifu harakati ya kuking’oa madarakani chama hicho kupitia sanduku la kura mwaka 2015 kutokana na imani kubwa waliyonayo kuwa chama hicho makini kina sera nzuri za kuwakomboa wanyonge.



Kwa upande wake katibu wa Chadema mkoa, kabla na baada ya kuwapatia Wanachama hao kadi aliwasomea haki na wajibu alionao mwanachadema popote alipo huku akiweka msisitizo umuhimu wa kupinga uonevu na kupigania haki na kulinda utu wa watu wote kwa gharama yoyote.
Aidha alisema kuwa operesheni hiyo itahamia rasmi wilayani Monduli Juni 24, mwaka huu wanapotarajia kuvuna wanachama wengi hasa kutokana na maombi ya muda mrefu ya wananchi wa maeneo hayo ambao wamekuwa wakiwaomba waende ili waweze kurudisha kadi za CCM na wachukue za Chadema.
Golugwa alisema kuwa wakati wa operesheni hiyo wanatazamia kuzindua mashina ya wakereketwa, ofisi za chama na kufanya mikutano ya hadhara ambapo harakati hizo zitaongozwa na viongozi wa mkoa na wilaya.
Kwa upande wao wenyeviti wa mkoa wa BAVICHA, Nanyaro  na BAWACHA, Ndossi waliwataka wanachama hao wapya kujiunga na mabaraza hayo ambayo ni haki ya kila mwachadema kwani yatawawezesha kushiriki kikamilifu katika  harakati za kuleta mabadiko hapa nchini.
Habari na Grace macha.


No comments:

Post a Comment