Tuesday, September 4, 2012

RIPOTI YA MGOMO WA WALIMU NCHINI KENYA PAMOJA NA KAULI YA SERIKALI

Ripoti iliyoandaliwa na BBC imesema Serikali ya Kenya imekiri kwamba haiwezi kutimiza matakwa ya walimu wa shule za misingi wanaogoma nchini humo huku mgomo huo ukiingia siku ya tatu. Waziri wa elimu Mutula Kilonzo amesema wanachotaka walimu yani kuongezwa asilimia miatatu ya mishahara yao hakiwezekani, kwa sababu pesa hizo hazikujumuishwa kwenye makadirio ya bajeti ya mwaka huu. Maelfu ya walimu nchini Kenya walianza mgomo wao juzi (September 3) wakidai kuwa serikali imekuwa ikipuuza kilio chao kuongezwa mishahara yao kwa miaka mingi ambapo walimu hao ni wa shule za misingi na zile za upili. Walimu hao wamekiuka agizo la mahakama lililoharamisha mgomo huo huku shule nyingi katika miji mikubwa kama Mombasa, Nairobi na Nakuru zilisalia kufungwa, walimu wa shule za upili pamoja na wahadhiri wa vyuo vikuu wamesema watajiunga na mgomo huo baadaee wiki hii ingawa tayari wameanza kususia kazi. Mgomo huu umetokea wakati shule zikifungua kwa muhula wa tatu kitu ambacho walimu hao wanasema sio hoja kwani wamekuwa wakigoma kila muhula wa tatu unapofungua kwa zaidi ya miaka kumi iliyopita wakidai hiyo nyongeza. Wanasema kuwa serikali haina usawa katika mishahara kwa wafanyakazi wa sekta ya umma kwani ni hivi juzi tu wauguzi na wafanyakazi wengine wa umma waliongezwa mishara baada ya kugoma lakini walimu wamepuuzwa. Huu mgomo umeonekana kufanikiwa kwasababu shule nyingi zimesalia kuwa bila walimu na wanafunzi wengi wamebaki majumbani.

No comments:

Post a Comment