Tuesday, May 29, 2012

MADIWANI MOSHI VIJIJINI WAMTUHUMU MBUNGE WA MOSHI VIJIJINI CYRIL CHAMI.

Mbunge wa Moshi Vijijini Cyril Chami(katikati)akifuatilia hoja kwenye baraza la madiwani.

Diwani akitoa hoja kwenye kiako hicho cha baraza kilichofanyika leo.  


BARAZA la madiwai wa halmashauri ya wilaya ya Moshi, mkoani
Kilimanjaro, limeelezwa kuwa wabunge wanaopaswa kuhudhuria kwenye
vikao vya baraza hilo, wanaongoza kwa utoro hivyo kutokuwa na
uwakilishi wa kutosha katika vikao hivyo.

Hoja hiyo ilitolewa jana na diwani wa kata ya Arusha-chini (TPC),

Rojas Mmari, alipokuwa akitoa hoja za maswali 10, aliyowasilisha
kwenye kikao cha baraza la madiwani kilikutana jana katika ukumbi wa
halmashauri hiyo wilayani hapa.

Wabunge waliotajwa ni pamoja na Dk. Cyrill Chami wa Moshi vijijini,

Dk. Augustine Mrema wa Vunjo na mbunge wa viti maalum mkoani
Kilimanjaro Betty Machangu, ambao kwa mujibu wa diwani huyo wamepata
kuhudhuria vikao vichache katika kipindi cha miaka miwili tangu
uchaguzi wa mwaka 2010.

Akizungumzia hilo diwani Mmari alisema ni vyema baraza lijulishwe

sababu za wabunge hao kushindwa kuhudhuria kwenye vikao vya baraza
hilo kuliko hali ilivyo, na kusema kuwa jambo hilo ni moja ya
ukiukwaji wa taratibu na kanuni za baraza zinazozungumzia mahudhurio
ya wajumbe wake kwenye vikao hivyo.

Mbali na hilo Mmari alirusha tuhuma kwa mbunge wa jimbo la Moshi

vijijini Dk. Chami, ya kwamba amekuwa aitumia magari ya halmashauri
kwa ajili ya ziara ya kutembelea wapigakura wake kwenye jimbo,
akitolea mfano wa ziara yake ya mwisho ambapo alitumia gari la
mkurugenzi wa halmashauri hiyo.

Hoja hiyo ilipingwa vikali na Dk. Chami, ambaye alitaka baraza hilo

kuunda tume ya kuchunguza tuhuma zilizotolewa na diwani huyo dhidi
yake ili kuweka wazi kile kinacholalamikiwa dhidi yake.

“Mh. Mwenyekiti naomba tume iundwe ili ukweli ubainike maana hakuna

siku hata moja niliyotumia gari la halmashauri kwa ajili ya ziara
zangu kwenye kata, lakini mtoa hoja atueleze ni hatua gani zichukuliwe
pale diwani anaposema uongo mbele ya baraza hili”, alisema Dk. Chami.

“Mwenyekiti naomba kukanusha sijawahi kutumia gari la halmashauri

kutembelea kwenye kata zangu”, alisema Dk. Chami, ambaye alifanya
ziara ya mwisho jimboni humo mwezi mmoja kabla ya kuvuliwa madaraka ya
uwaziri katika mabadiliko yaliyofanywa hivi karibuni na rais Kikwete
kwa kuzingatia ripoti ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za
serikali iliyobaini dosari mbali mbali katika shirika la viwango
nchini (TBS), lililoko chini ya wizara hiyo.

Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Moshi Moris Makoi, wakati

akihitimisha hoja hiyo, alisema kuwa ni kweli kuwa gari la mkurugenzi
wa halmashauri hiyo, lilitumika kwenye ziara ya mwisho ya mbunge huyo,
lakini liliwabeba baadhi ya watumishi wa halmashauri na sio mbunge
kama ilivyodaiwa na diwani huyo.

Hata hivyo alisema hoja hiyo haipaswi kuendelezwa kwenye kikao hicho

kwa tahadhari ya kuibua mvutano na malumbano yanayoweza kukwamisha
mijadala mingine kulingana na ratiba ya kikao hicho.

Katika hatua nyingine kikao hicho cha madiwani kilielezwa kuwa ofisi

ya mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo na eneo la mapumziko na
vikao vya madiwani haijakamilika kutokana na chumba kilichotengwa
kuendelea kutumika kuhifadhi masanduku ya kupigia kura.

Hoja hiyo ni sehemu ya zile zilizotolewa na diwani Mmari, ambaye

alisema mpaka sasa madiwani wameonekana wakishinda kwenye korido za
jengo la halmashauri hiyo bila kuwa na eneo maalum la kuendesha
shughuli zao, ikiwemo mipango mbali mbali inayopaswa kusimamiwa na
madiwani hao.

Katika hoja yake hiyo Mmari alipendekeza ofisi hiyo ya mwenyekiti

kukarabatiwa na kuwa na vitendeakazi vya kisasa kwa kutambua uzito wa
kiongozi huyo kwenye halmashauri hiyo.

No comments:

Post a Comment