Wednesday, March 6, 2013

WAHINDI WADAIWA KUIWEKA SERIKALI MFUKONI.


*Kiwanda cha nondo chaua watanzania/chajeruhi kwa uji uji wa chuma

*Waandishi watakiwa kwenda na kibali cha serikali ili kuhojiana na uongozi

*Waliojeruhiwa watelekezwa!
 Lucas Mtoka (30) aliyekuwa mfanyakazi wakiwanda hicho cha Sayona Steel Ltd kama anavyoonekana na majeraha yaliyotokana na kulipukiwa na ujiuji na moto ndani ya kiwanda hicho huku mwenzao mmoja akipoteza maisha...

NA MWANDISHI WETU,
ALIYEKUWA MWANZA

KIWANDA kinachotengeneza Nondo kijulikanacho kwa jina la Sayona Steel Ltd kilichopo eneo la Nyang’omango kata ya Usagala wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza kinadaiwa kuua watanzania na wengine kujeruhiwa na kutelekezwa bila msaada wowote. Imebainika.

Kiwanda hicho kinachomilikiwa na wawekezaji wenye asili ya India, kinadaiwa kutokuwa katika hali ya usalama na pindi viongozi wa serikali wakienda huishia kukifunga na baada ya siku moja kinafunguliwa.

Hivi karibuni, baadhi ya wafanyakazi wa kiwanda hicho wamekufa baada ya kuungua miili yao vibaya na ujiuji wa chuma unaotengenezewa nondo ndani ya kiwanda hicho huku wengine wakijeruhiwa vibaya.

Mmoja wa majerui ambaye alijeruhiwa hivi karibuni mwezi Februari mwaka huu na anajulikana kwa jina la Barui na wenzake wanne akiwemo marehemu Joseph ambaye alienda kuzikwa katika kijiji cha Mwalungwabagole.

Baadhi ya wafanyakazi waliohojiwa na mwandishi wa habari hizi kwa makubaliano ya kutoandka majina yao na vitengo wanavyofanyia kazi, walitoboa siri hiyo na kuomba Ikulu kuingilia kati na kuchunguza ubora wa kiwanda hicho.

Walisema kuwa wafanyakazi wengi wa kiwanda hicho hawana mikataba ya ajira hivyo pamoja na hatari wanazokumbana nazo baadhi wanalipwa Tsh. 9,800 kwa siku wengine Sh. 7,000.

‘’Humo ndani kazi ni ngumu, hatuna mikataba, malipo ni kidogo na tukifungiwa ndani hewa haitoshi na wenzetu wamekufa wengine wameungua vibaya lakini hakuna anayejali na serikali wakija wanafunga kiwanda lakini baada ya siku moja utaona kinafunguliwa’’ walisema kwa nyakati tofauti wafanyakzi hao.

Walikitaja kitengo ambacho ni hatari zaidi kuwa ni kitengo cha finance ambacho ndiko wengi wao wamekufa na kujeruhiwa.

Mmoja wa majeruhi wa ujiuji huo wa nondo ambaye anatakiwa kufanyiwa upasuaji ni Lucas Mtoka (30) mwenye watoto wawili Emmanuel (3) na Stephen(1) ambaye aliungua na wenzaken nane April 18, 2012.

Mtoka alisema kuwa siku hiyo ilikuwa ni jioni ya saa kumi na mbili ambapo akiwa na wenzake ndipo alipolipukiwa huku moto ukiwa umetanda kwenye chumba hico kisha akapelekwa katika hospitali ya Seketule.

‘’Tuliumia vibaya kisha tkapelekwa Seketule ambako nililazwa kwa wiki mbili mimi na wenzangu akiwemo Simon Maiko, Renatus Lubinza, Joseph, Kulwa, Willium Mhangwa na huyu mwingine alikuwa mgeni alifariki hospitali baada ya miezi miwili’’ alisema Mtoka.

Alioulizwa kuwa amejipangaje kumudu gharama za upasuaji anaotaiwa kufanyiwa sehemu za shingoni na maeneo ya mwili wake alimoungua vibaya, alisema kuwa hajui hatima yake na sasa hawezi kurudi kazini tena.

Uongozi wa kiwanda ulipotakiwa kuelezea hali hiyo ulisema kuwa haupo tayari mpaka hapo mwandishi wa habari atakaotoka na kibali serikalini kwa ajili ya kuhoji udhaifu uliopo kiwandani hapo.

‘’Nenda kalete kibali cha serikali ili uweze kuhoji mambo ya hapa kiwandani’’ aisema mmoja wa viongozi wa kiwanda hicho aliyejitambulisha kwa jina moja la Mehul mwenye simu namba 0754 442142.

No comments:

Post a Comment