Sunday, March 10, 2013

SIMBA BADO TUPO..


Wachezaji wa Simba, Abdallah Seseme, Amri Kiemba na Mrisho Ngassa wakimpongeza Haruna Chanongo (6) kufunga bao la pili katika mchezo wa leo.

Na Mahmoud Zubeiry
WEKUNDU wa Msimbazi, Simba SC wamezinduka leo katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na kufufua matumaini ya kutetea ubingwa wao, kufuatia ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Coastal Union ya Tanga, Uwanjwa Taifa, Dar es Salaam.
Ushindi huo, unaifanya Simba SC itimize pointi 34, baada ya kucheza mechi 19, ikiendelea kubaki nafasi ya tatu, nyuma ya Azam FC yenye pointi 37, wakati wapinzani wao wa jadi, Yanga SC wapo kileleni kwa pointi zao 45.  
Hadi mapumziko, tayari Simba SC walikuwa mbele kwa mabao 2-0 yaliyopatikana ndani ya dakika tatu za muda wa nyongeza baada ya kutimu kwa dakika 45 za kipindi hicho.
Coastal ndio waliuanza vema mchezo huo, wakisukuma mashambulizi mfululizo langoni mwa Simba na kama si uimara wa kipa Mganda, Abbel Dhaira wangeweza kupata bao la mapema.
Ndani ya dakika tatu, kipa huyo namba wa Uganda aliokoa michomo miwili ya hatari, mmoja wa chini na mwingine wa juu na kuwafanya mashabiki wa Simba warukwe kwa shangvwe, wakiamini wamepata kipa bora.
Ikumbukwe hii ilikuwa mechi ya kwanza kwa Dhaira kudaka katika Uwanja wa Taifa tangu asajiliwe Simba SC dirisha dogo akitokea Iceland nay a pili katika ardhi ya Tanzania, baada ya Simba na Bandari Kombe la Mapinduzi.
Kiulainiii; Mrisho Ngassa akiifungia Simba SC bao la kwanza leo. Kipa Shaaban Kado amekwishapotea mabode kulia, langoni yupo beki Philip Mugenzi, ambaye hakuwa na la kufanya.
Zaidi ya hapo, Dhaira alidaka dakika 45 kila mechi katika mechi mbili za kirafiki nchini Oman na dakika zote 90, wakati Simba ikilala 4-0 mbele ya Recreativo de Libolo nchini Angola wiki iliyopita.     
Mrisho Khalfan Ngassa alikuwa wa kwanza kuwainua vitini wana Simba dakika ya kwanza ya muda wa nyongeza, baada ya kumchambua kipa Shaaban Kado, akimalizia gonga safi zilizosababisha kizazaa langoni mwa Wagosi wa Kaya.
Haruna Athumani Chanongo alipigilia msumari wa pili kwenye ‘jeneza’ la Coastal hii leo dakika ya tatu wa muda nyonegza akimalizia kazi nzuri ya Ngassa, kufuatia shambulizi la kushitukiza. 
Kipindi cha pili, Coastal walikianza tena kwa kasi na kufanikiwa na kupata bao la kufutia machozi dakika ya 49 na ushei, lililofungwa na kiungo Razack Khalfan aliyeunganisha krosi ya Twaha Shekuwe.
Baada ya hapo, timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu na hadi kipyenga cha refa Martin Sanya kutoka Morogoro kinapulizwa kuhitimisha mchezo huo, Wekundu wa Msimbazi waliibuka kidedea.
Simba SC ilichelewa kuingia uwanjani hii leo na kukosa hata muda wa kupasha misuli moto, kutokana na matatizo ya kufungiwa hotelini.  
Katika mchezo huo, kikosi cha Simba SC kilikuwa; Abbel Dhaira, Nassor Masoud ‘Chollo’, Miraj Adam, Hassan Hatibu, Shomary Kapombe, Jonas Mkude, Amri Kiemba, Rashid Ismail/Saim Kinje, Abdallah Seseme, Haruna Chanongo na Mrisho Ngassa/Ramadhan Singano ‘Messi’.
Coastal Union; Shaaban Kado, Hamad Hamisi, Abdi Banda, Mbwana Hamisi, Philip Mugenzi, Razack Khalfan, Daniel Lyanga/Twaha Shekuwe, Mohamed Athumani, Deangelis da Silva, Suleiman Kassim ‘Selembe’ na Joseph Mahundi/Castory Mumbara. 

No comments:

Post a Comment