Zitto Kabwe
MATOKEO ya Kidato cha Nne ya namna hii (zaidi ya nusu ya
wahitimu kupata sifuri) na takriban asilimia 90 kufeli kwa kupata daraja
la nne na daraja
la sifuri sasa ni mwaka wa tatu mfululizo.
Matokeo yakitoka tunasema weeee mpaka povu linatoka. Baada ya wiki tumeshasahau na hakuna hatua yeyote.
Lazima Uwajibikaji utokee. kwanza Waziri Shukuru Kawambwa lazima awajibike na Naibu wake na Katibu Mkuu na Kamishna.
Najua kuwa haina uhusiano wa moja kwa moja maana matatizo ya elimu ni
makubwa sana nchini.
Lakini ni lazima kitu fulani kitokee ili kufanya mabadiliko.
Uwajibikaji ni njia mojawapo inayoleta nidhamu na uharaka katika utendaji kazi.
Tumwambie Rais aichukue Wizara ya Elimu, yaani Waziri wa Elimu awe yeye (kuwe na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Elimu).
Tumwambie matokeo yakibaki
hivi mwakani na yeye atatoka. Najua wa mwakani ndio wako kidato cha nne
sasa na wana msingi mbaya tayari lakini sio jukumu letu kujipa majibu bali
ni jukumu letu kuiambia serikali hapana. Tuipe masharti. Vinginevyo haya yatakwisha na mwakani yatarudia tena.
Hawa watoto wanakwenda wapi? Mwaka jana tulisema mpango wa kujenga vyuo vya
ufundi kila halmashauri ya wilaya uanze mara moja.
Katika Bajeti Kivuli
mwaka 2011 tulipiga hesabu kwamba tunahitaji sh 720 bilioni katika
kipindi cha miaka mitano ijayo kujenga vyuo vya ufundi vya VETA kila
wilaya.
Tukawaambia badala ya kukopa kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii kulipana
posho ni vema tukope kuwekeza kwenye elimu maana elimu ni hifadhi ya jamii.
Elimu yetu ya sasa inazalisha matabaka kwenye jamii na ni hatari sana kwa
uhai wa taifa.
Tunaweza kujidai kujenga madaraja na miji mipya. Tunaweza kujidai
kujenga mabomba ya gesi na kusambaza umeme kila kijiji mpaka kwenye
vyoo.
Kama hakuna elimu haya yote ni bure kabisa. Hata kukosa uvumilivu wa
kiimani sasa hali itakuwa mbaya zaidi unapokuwa na taifa la mbumbumbu.
Waziri Kawambwa na wenzake watoke na watoke sasa.
SOUURCE Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment