Thursday, December 20, 2012

POLISI WANAODAIWA KUGAWA FEDHA ZILIZOPORWA WAPEWA SIKU SABA KUJISALIMISHA.

 

JESHI la Polisi limetoa siku saba kwa baadhi ya askari kuzisalimisha  fedha zipatazo sh milioni 150 wanazodaiwa kuiba, ambazo zilizoporwa na majambazi Mtaa wa Mahiwa na Livingston jijini Dar es Salaam juzi.

 
Akizungumza na waandishi wa habari jijini, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum, Suleiman Kova, alisema kutokana na tuhuma hizo jeshi hilo limeunda Jopo la wapelelezi ili kujua ukweli wa madai hayo.

Alisema Jopo hilo litaundwa na watu watano, likiongozwa na Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum, Ahmed Msangi, atakayehakikisha kwamba muda mfupi inavyowezekana, ukweli upatikane ili wananchi wajulishwe matokeo.

Kamanda Kova alisema jeshi hilo lina mfumo wake wa kuchunguza askari wake inapotokea amejihusisha katika matukio yanayokwenda kinyume na maadili ya kazi yake.

Alisema tukio hilo halikubaliki hivyo kila aliyepewa jukumu la kulifuatilia ni lazima ahakikishe kuwa anafanya kazi kwa ufasaha ili majibu yapatikane haraka kuondoa shaka shaka kwa wanachi.

Kova alimtahadharisha Msangi kuwa, endapo atashindwa kutoa majibu ya kuridhisha basi atambue hata yeye itabidi awajibike ambapo alisema vitu kama hivi vikiachwa viendelee vinaliletea jeshi hilo sifa mbaya na kupoteza imani kwa wananchi.

“Pamoja na kumkabidhi kazi hiyo Msangi lakini hata mimi sitakaa kimya bali nitalifuatilia kwa karibu ili mradi tuwapatie wananchi ukweli”alisema Kova.

Alibainisha kuwa hawezi kupinga kama askari wanaweza kushiriki katika vitendo hivyo viovu bali suala hilo bado linahitaji ushahidi zaidi hivyo, ni vema wananchi wenye ushahidi wakatoa ushirikiano utakaosaidia kupatikana fedha hizo.

Aidha, Kova alilitaka jeshi la polisi kufanya kazi zake kwa nidhamu, uaminifu na ueledi kwani endapo ofisa au askari atakiuka maadili ya kazi yake, basi  hatua madhubuti zitachukuliwa dhidi yake bila kuchelewa.

Hata hivyo, katika hali ya kushangaza jopo hilo linaundwa na polisi wenyewe bila kushirikisha wadau wengine kwa madai kuwa, eti lifanya kazi kwa kutii sheria zote bila kwenda kinyume.

No comments:

Post a Comment