Tuesday, August 7, 2012

Wabunge waridhia hoja ya marekebisho mafao‏

 Dodoma:
WABUNGE wameridhia hoja ya kutaka yafanyike marekebisho ya Sheria namba 5 ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya mwaka 2012 baada ya Mbunge wa Kisarawe, Selemani Jafo (CCM) kuiwasilisha bungeni jana.

Katika hoja hiyo iliyoungwa mkono na wabunge, Mbunge huyo ametaka Serikali katika Mkutano ujao wa Bunge, iwasilishe muswada wa sheria kwa hati ya dharura kwa ajili ya kuweka vifungu vya sheria vinavyoweka fao la kujitoa katika mifuko hiyo kwa wafanyakazi wanaoacha kazi kwa sababu wafanyakazi wana haki ya kuacha au kuendelea na kazi.

“Wakati tunasubiri kuleta muswada Serikali itoe waraka wa maelekezo kwa mifuko ya jamii kuendelea kuwalipa mafao watumishi walioachishwa kazi au walioacha kazi,” alisema Mbunge huyo.

Ametaka pia katika muswada huo, Serikali iondoe vifungu vinavyomtaka mtumishi kuwasilisha maombi ya  kupata msamaha kwa fao la kujitoa.

Aidha, ametaka Serikali iagize kampuni za madini kutosimamisha wafanyakazi waliohoji kwa kina juu ya mafao yao baada ya kupata mshituko wa taarifa ya kutoruhusiwa kuchukua mafao.

Aliitaka Serikali iangalie kanuni inayotumika kukokotoa mafao ya wafanyakazi na kutaka watumishi wote wanaolipa kodi kupitia mishahara yao wapewe TIN namba wajulikane ni walipa kodi halali.
Mbunge huyo alisema Serikali isipowasilisha muswada huo wa marekebisho ya sheria, atawasilisha muswada binafsi ili wabunge wote walete marekebisho hayo kama alivyoyapendekeza.

Kwa mujibu wa Mbunge huyo, wanachama walifaidika na kujitoa na kulipwa mafao kwa kuwa uliwawezesha kupata kianzio cha maisha yao baada ya kuacha kazi ikizingatiwa kwamba wafanyakazi nchini wanaishi maisha ya kuungaunga.

Alisema kutokuwapo kifungu hicho cha sheria kutaleta athari kwa watumishi wanaoachishwa kazi kabla ya umri wa kustaafu kwa kushindwa kuendesha maisha.
Alisema jambo hilo limekuwa tete na kuathiri uzalishaji katika sekta hususan katika madini ambako katika baadhi ya migodi, baadhi ya wafanyakazi walitishia kuandamana.

Spika Anne Makinda alisema leo Waziri wa Kazi na Ajira huenda akazungumzia suala hilo katika hotuba yake, lakini akataka Kamati ya Uongozi kuangalia upya muswada huo kabla ya kuwasilishwa kama hati ya dharura.

No comments:

Post a Comment