Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa
Jakaya Mrisho Kikwete ametuma salamu za rambirambi kwa Waziri wa Habari,
Vijana, Utamaduni na Michezo, Mheshimiwa Fenella Mukangara kuomboleza
kifo cha Mhariri Mtendaji wa Gazeti la JamboLeo, Ndugu Willy Edward
Ogunde kilitokea usiku wa kuamkia jana, Jumapili, Juni 17, 2012
mjini Morogoro.
Katika salamu zake za rambirambi, Mheshimiwa Rais
Kikwete amesema kuwa ameshtushwa na kusikitishwa na kifo cha ghafla
cha Ndugu Willy Edward Ogunde ambaye amepoteza maisha akiwa bado kijana
ingawa tayari alikuwa amekwishakutoa mchango mkubwa katika maendeleo
ya tasnia ya habari kutokana na umakini wake, uzingatiaji wa weledi
kikamilifu na misingi mingine mikuu ya uandishi wa habari.
“Nimepokea kwa mshtuko mkubwa na huzuni nyingi
kifo cha ghafla cha Ndugu Willy Edward Ogunde ambaye nimejulishwa kuwa
kilitokea usiku wa kuamkia jana, Jumapili, huko Morogoro ambako alikuwa
amekwenda kikazi. Ndugu Willy Edward Ogunde amepoteza maisha akiwa bado
kijana sana hata kama ni kweli katika muda mfupi wa maisha ametokea
kuwa mfano wa kuigwa katika tasnia ya habari kwa mchango wake wa kudumisha
weledi na misingi mingine mikuu ya uandishi wa habari.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Nakutumia wewe Mheshimiwa
Waziri salamu za dhati ya moyo wangu za rambirambi kuomboleza kifo cha
kijana huyu wetu na mwanataaluma wako. Aidha, kupitia kwako nakuomba
uniwasilishie salamu zangu kwa wanataaluma wote wa tasnia ya habari
nchini kwa kuondokewa na mwenzao. Lakini zaidi, nakuomba unifikishe
salamu zangu nyingi kwa wanafamilia, ndugu na jamaa wa Marehemu Willy
Edward Ogunde.”
“Wajulishe kuwa niko nao katika msiba huu mkubwa
kwa sababu msiba wao ni msiba wangu pia. Naelewa machungu yao katika
kipindi hiki kigumu cha kufiwa na mpendwa wao. Nawaombea subira na uvulivu.
Aidha, wajulishe kuwa naungana nao katika kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi
wa Rehema, aiweke pema peponi roho ya Marehemu Will Edward Ogunde. Amina,”
amesisitiza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
IMETOLEWA NA:
KURUGENZI YA MAWASILIANO YA
RAIS IKULU
18 Juni, 2012
DAR ES SALAAM
No comments:
Post a Comment