TGNP YAITAKA SERIKALI KUWAWAJIBISHA MAWAZIRI WANAODAIWA KUFUJA FEDHA ZA UMMA.
MTANDAO wa Jinsia Tanzania (TGNP) imeitaka
Serikali kuwawajibisha mara moja mawaziri, manaibu waziri na watendaji wakuu wa
Serikali na mashirika ya umma ambao wametajwa kuhusika na matumizi mabaya ya
fedha za umma ama kushindwa kusimamia rasilimali za taifa.
Kauli
hiyo imetolewa leo jijini Dar es
Salaam na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Anna
Kikwa katika taarifa yake aliyoisambaza kwa vyombo vya habari. Aidha amemtaka mkuu
wa nchi awafute kazi watendaji wanaotumia vibaya fedha za umma na kuwaongezea
wananchi umasikini, ili iwe fundisho kwa watendaji wa Serikali wenye tabia kama hiyo na wachukuliwe hatua za kisheria.
Hata hivyo TGNP imeishauri Serikali kuboresha
mifumo ya kusimamia rasilimali za nchi yetu ili wananchi wote waweze kufaidi
keki ya taifa kwa sababu mara zote Serikali imekuwa ikisema Tanzania hatuna
rasilimali lakini hali halisi ni kwamba rasilimali za taifa zinaliwa na
mafisadi wachache wa ndani na nje ya nchi.
Katika hatua nyingine, mtandao huo umetoa pongezi
kwa wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge za Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC),
Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Kamati ya Hesabu za Serikali Kuu, Ardhi
Maliasili na Utalii kwa kusimamia vema na kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za
serikali zinazotokana na walipa kodi na kuwasilisha ripoti zao Bungeni ambazo
zimeibua uozo mkubwa na kujenga mjadala mpana unaotaka uwajibikaji kwa
wanaohusika.
“Tunawapongeza pia baadhi ya wabunge walioshiriki katika mijadala kwa kuzijadili ripoti hizo kwa undani bila
kujali urafiki, itikadi za kisiasa, hasa ile ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa
Hesabu za Serikali (CAG) kwa kuibua uozo uliojificha na kusimamia maslahi ya Taifa.”
amesema Bi. Kikwa katika taarifa hiyo.
“Tumeshuhudia mara kadhaa kupitia vyombo vya
habari wabunge wakiacha itikadi zao za
kisiasa na kusimamia kwa dhati dhana ya kushinikiza uwajibikaji katika vyombo
vinavyohusika kutokana na ufisadi kama Richmond,
Dowans nk. Hata hivyo, TGNP kwa muda mrefu tumekuwa tukipinga ubadhirifu wa
fedha za umma na kudai haki ili
kutokomeza ufisadi uliokithiri, lakini bado ufisadi umezidi kushamiri hasa
katika Wizara na taasisi za umma.
“Sisi kama wanaharakati tunasema kuendelea kwa
ufisadi ni aibu kwa serikali iliyoko madarakani, TGNP tuko mstari wa mbele kushinikiza rasilimali za taifa ziwanufaishe
wananchi wote, hasa walioko pembezoni, kamwe hatutanyamazia aina yoyote ya
ubadhirifu na matumizi mabaya ya fedha za miradi ya wananchi zilizotengwa kwa
ajili ya maendeleo ya wananchi.” Imesema taarifa hiyo.
"Tumeshuhudia wanawake na wasichana wakiendelea
kuwa maskini na kukumbana na mifumo kandamizi kwa kukosa haki za kufikia huduma
za msingi kama vile maji, barabara, afya, elimu, kilimo, utawala bora n.k.
Fedha zinazopotea zinatokana na kodi za wananchi na jamii ina haki ya kuhoji
uwajibikaji na wahusika wanatakiwa kuchukuliwa hatua za kisheria," imeongeza taarifa hiyo kwa vyombo vya habari.
Vilevile tunawapongeza wabunge wote walioshiriki kwa dhati
katika zoezi la kusaini kusudio la kutaka viongozi waliotajwa/kutuhumiwa kwenye ripoti hizo kuwajibika. Ili kuonesha dhana ya
uwajibikaji na utawala bora unaozingatia misingi ya haki za binadamu.Na mwandishi wetu.
No comments:
Post a Comment