Sunday, June 3, 2012


MAKAMU WA RAISI ASISITIZA  JAMII KUSHIRIKISHWA KWENYE KUBORESHA NA UTUNZAJI WA MAZINGIRA.
Makamu wa Raais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akitoa hotuba yake kwenye uzinduzi wa wiki ya mazingira inayoadhimishwa kitaifa Mjini Moshi mkoani Kilimanjaro.
Wanafunzi walikuwepo kwenye maadhimisho hayo ya wiki ya mazingira,iliyoazimishwa Kitaifa Mkoani Kilimanjaro.


Burududani mbalimbali zilipamba siku ya wiki ya Mazingira.
                                                                    
TAASISI za Serikali na zisizo za Kiserikali zimepewa jukumu la kueleimisha jamii juu ya umuhimu wa utunzaji mazingira kwa kutumia  maudhui ya siku ya maadhimisho  ya wiki ya  mazingira Nchini inayosema hifadhi mazingira jikite kwenye uzalishaji endelevu, hatua ambayo itasaidia kulinusuru taifa na majanga yatokanayo na uharibifu wa mazingira ikiwemo vimbunga

Rai hiyo ilitolewa na makamu wa Raais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal, wakati akizindua wiki ya mazingira inayoadhimishwa kitaifa Mjini Moshi mkoani Kilimanjaro ambapo alisema ni vema serikali kwa kushirikiana na mashirika binafsi wakatoa elimu na uhamasishaji kwa wananchi kujikita katika uzalishaji endelevu kwa kuepuka uchafuzi wa mazingira.

Alisema katika siku ya mazingira ambayo huadhimishwa kila mwaka kuanzia Juni Mosi hadi juni tano wananchi waelimishwe ipasavyo juu ya utunzaji,usimamizi na usafi wa mazingira ili kupata uelewa zaidi wa masuala  hayo na changamoto zake.

“Suala la kupata uelewa na jukumu la uhifadhi na usafi wa mazingira ni letu sote,wazee kwa vijana,wake kwa waume na hata watoto hivyo tutumie vema wiki hii kuhakikisha suala la utunzaji wa mazingira linaeleweka ipasavyo kwa wananchi na kila mmoja anatimiza wajibu wake”alisema Bilal.

Aidha ailisema  maadhimisho hayo yamezingatia historia ya mkoa wa Kilimanjaro ambao una mfano hai wa upoteaji wa bionuai uliosababishwa na uharibifu wa vyanzo vya maji  na mfano mzuri ni katika ziwa jipe lililoko wilayani Mwanga ambalo limemezwa na magugu maji yanayohatarisha uwepo wa ziwa hilo.

Alisema mkoa wa Kilimanjaro  unakabiliwa changamoto kubwa ya  uchomaji moto na uharibifu wa mazingira kwenye mlima Kilimanjaro  ambao ni urithi wa dunia hali ambayo inapaswa kushughulikiwa kabla haijaleta madhara makubwa.

Awali akizungumza katika maadhimisho hayo mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro  Leonidas Gama alisema  katika kukabiliana na tatizo la uharibifu wa mazingira mkoa unakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kuwepo kwa uvamizi wa maeneo ya hifadhi ya maliasili unaoambatana na ujangili wa rasilimali za asili,ukataji wa miti ya asili pampja na matumizi ya ardhi yasiyozingatia kanuni za kitaalamu.

Gama alisema katika kukabiliana na changamoto ya uharibifu wa mazingira mkoa umejipanga kuanzisha program maalumu ya upandaji miti, ya asili mfululizo katika kipindi cha miaka mitano,utakaolenga kuurejeshea mlima Kilimanjaro uoto wake wa asili .

Alisema katika kipindi cha mwaka huu mkoa umepanga kupanda miti Mil. 8.259 lakini kutokana na mkoa huo kukabiliwa na tatizo la ukame na upungufu wa miche ya miti hadi sasa wamepanda miti  Mil. 5.604 .

Maadhimisho ya wiki ya mazingira mwaka huu ambayo yanatarajiwa kufungwa Juni tano mjini Moshi na Rais wa jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete,yataambatana na utoaji wa Tuzo ya Rais ya kuhifadhi  vyanzo vya maji,kupanda na kutunza miti.

No comments:

Post a Comment