Thursday, November 22, 2012



                         *Ukame pigo lingine kwa wakulima Wilayani Hai.


Na Rodrick Mushi,Hai.
Sekta ya Kilimo ni miongoni mwa sekta muhimu nchini,ambapo mbali na kutoa ajira kwa zaidi ya asilimia 70 hutegemewa kama chanzo kikuu cha chakula nchini lakini imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali.

Kwa mwaka ambao mvua zimenyesha za kutosha na wakulima kupata mazao sekta ya kilimo inatoa asilimia 95 ya chakula chote kinachotumika nchini.

Zipo changamozo ambazo zimekuwa kikwazo kikubwa kwa wakulima  na zinafanana karibia nchi nzima,na ukikutana na kila mkulima na kuzungumza naye  hususani ni maeneo ya vijijini basi utaweza kuwaonea huruma wakulima hawa.

Mbali na mchango mkubwa wa ajira,na kuhudumia nchi yetu chakula pamoja na kusaidia kwenye mchango wa pato la taifa lakini sera nyingi zinazohusu kilimo hakuna mkulima anayehusishwa,na badala yake zimebaki kwenye makaratasi huku mkulima akiendelea kutaabika.

Ukizungumza na wakulima wengi wanalalamikia upatikanaji wa vocha za pembejeo,ulanguzi wa bei ya kuuzia,kutokuwa na elimu ya kilimo kutoka kwa maafisa ugani,migogoro kati yao na wafugaji,ushuru mkubwa pamoja na ukame.

Nilitembelea Wakulima Wilayani Hai ambao wanalima zaidi mahindi, maharage, ufuta, hususani ni ukanda wa tambarare, wanasema kuwa ukame umekuwa kikwazo kikubwa kwao kuendelea kuwa maskini.

Wakati ukame ukiendelea kuwarudisha wakulima nyumba kwa mazao yao kukauka yakiwa mashambani,viongozi wengi wamebaki kusema kuwa hali hiyo inatokana na mabadiliko ya hali ya hewa bila kutafuta njia mbadala kutatua suala hilo.

Ukame unavyowatesa wakulima
Issa Sadiki mkazi wa kijiji cha kwa sadala Kata ya Masama Kusini Wilayani Hai anasema kuwa badala ya kilimo kuwa mkombozi  wao kimekuwa  adhabu kwao kwani kimekuwa hakitimiza malengo na matarajio yao.

Anasema kuwa kwa Wilaya hiyo wananchi wana miaka mitatu sasa wakiadhiriwa na ukame,wakipanda mazao na kukauka kutokana na mvua kutonyesha.

 Sadiki anasema kuwa mwaka huu alikuwa amelima shamba la hekari 10 ambapo garama aliyotumia kuanzia kulima,mbegu hadi kuhudumia shamba ni zaidi ya shilingi million 4 lakini hajaambulia kitu.

Anasema kulima shamba heka moja ni shilingi 30,000 mbolea ni shilingi 70,000 kilo 50 mbegu ambayo mfuko wa kilo 2 unauzwa  7500 hivyo utaona ni jinsi gani mkulima amekuwa akiumia katika kilimo.

Kwa mahesabu ya kawaida mkulima Issa anasema bado hujazungumzia mkulima mbaye hana shamba kama yeye aliyekodisha shamba heka 10 ambapo ni 500,000 garama za kulima heka 10 ni shilingi 400,000 lakini mvua zinashindwa kunyesha na mazao kukauka yakiwa shambani.

Ni dhahiri kuwa Mkulima amekua ni mtu wa kupata hasara kwani licha ya kuwepo kwa ruzuku za pembejeo lakini bado pembejeo za kilimo zimekuwa zikiuzwa gali kwa mkulima anapohitaji.

Issa anasema kuwa ni bora ingekuwa mkulima anatumia garama na kupata faida lakini badala yake imekuwa hasara kwa wakulima na taifa.

Wapo wakulima wanaokodisha mashamba,wapo wanaokopa fedha benki wakilima wakiwa na malengo ya kuwekeza kwenye kilimo,hawa ndio wamekuwa wakiuziwa hata mali zao au kuuza mali ili kuweza kulipa deni ambalo wanakuwa wamekopa.

Willy nyari yeye anasema kuwa ukame umemfanya kuendelea kuwa maskini kwani huu ni mwaka wa tatu sasa mwaka huu angevuna ila ukame wa mvua moja  pekee ya kumalizia mazao kukomaa ndiyo iliyomkosesha mazao.

Anasema kuwa alichoambulia kwenye hekari tatu alizokuwa amelima ni magunia 5 ambapo mvua zingenyesha angeweza kuvuna hadi magunia 80 kwenye hekari hizo.

Anasema kuwa Mkulima ni mtu wa kuvumilia hali yoyote ile lakini Serikali imekuwa haifanyi jitihada za kumfanya mkulima kuweza kufurahia kilimo ambacho kimekuwa kikitoa jira kubwa nchini.

Nyari anasema kuwa Wilayani humo,kuna maji ya kutosha na yapo mashamba makubwa ambayo yamepewa wawekezaji na wanatumia maji yaliyopo kwa kumwagilia mazao yao ambayo yamekuwa yakistawi muda wote.

Anasema kuwa wananchi hawana elimu juu ya kilimo cha umwagiliaji au ya kulima mazao ya muda mfupi ili kuweza kuwasaidia wakulima kuondokana na adha hiyo ya kukaukiwa na mazao kila mwaka.

Wakati wakulima wakiendelea kupata hasara,wapo wanaohoji juu ya uwepo wa maafisa ugani ambao wanatakiwa kutoa elimu kwa wakulima,lakini badala yake wamekuwa wakikaa maofisi na kuendelea kulipwa mishahara.

 Hali halisi ya tatizo la ukame.
Wilaya ya Hai ina misimu miwili ya kilimo yaani masika na vuli,kwa kipindi cha mwaka 2011 ambacho nacho kilikuwa na tatizo la ukame mvua ya milimita 37.8 ilinyesha mwezi januari na milimita 59.2 mwezi februari mvua ambazo zilileta matumaini kwa wakulima kulima na hatimaye mvua kutoweka na mazao kukauka.

Kwa mwaka huu msimu wa kilimo ulianza april 3,kwa kuwepo kwa mvua za mtawanyiko ndani ya mwezi moja na kufanya mazao yaliyokuwa mashambani kustawi,ambapo mvua za mwisho zilinyesha may 5 na hazikuwepo mvua nyingine zilizofuatia.

Kwa mujibu wa taarifa ya hali ya kilimo iliyoandaliwa na Halmashauri ya Hai,mwaka huu wa 2012 kwa Wilaya ya hiyo asilia 70 ya mahindi yaliyokuwa yameoteshwa yamekauka na wakulima kukosa kabisa mazao kutokana na ukame.

Kutokana na hali hiyo ya ukame watu 2224,850 ambao walikuwa wanategemea kilimo watu 63,982 wanakabiliwa na upungufu wa chakula kutokana na mazao yao kukauka yakiwa mashambani.

Tatizo la ukame linaonekana kuwa kubwa na madhara makubwa kwani kwa mwaka 2012 hadi julai 14 mahindi yaliyokuwa yamelimwa hekta 22,300 ziliweza kunyauka hekta 16,725 ambapo hekta 5575 pekee ndizo walizoweza kuvuna.

Ni dhahiri kuwa wakulima wa Hai hawazalishi chakula kwa ajili ya watu wa hai pekee bali kinasaidia nchi nzima,hivyo kuwepo kwa ukame Hai na maeneo mengine ni matokeo ya kuendelea kuwepo kwa hali mbaya ya chakula na umaskini nchini.

Diwani wa Kata ya Masama Kusini Issa Kisanga anasema kuwa wakulima wengi wanategemea kilimo pekee kuweza kuendesha maisha yao ya kila siku,ambapo kwa sasa Wilaya ipo hatarini kukumbwa na baa la njaa kutokana ukame wa mazao wa muda mrefu.

Nini Kifanyike?
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Leonidas Gama anasema kuwa mabadiliko ya hali ya hewa kwa kiasi kikubwa yanachangiwa na uharibu wa mazingira ambao umekuwa ukifanywa na wananchi wenyewe.

Anasema kuwa kutokana na hali mbaya ya ukame ndio maana Mkoa umeamua kupambana na udhibiti wa uharibifu wa mazingira ili kusaidia kuondokana na hali ya kukosekana kwa mvua.

Wananchi wengi wanasema kuwa ni wakati wa Serikali kubadili kilimo cha kutegemea mvua hadi kutengeneza miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji pamoja na mazao yanayostahimili ukame.

“Serikali iweke utaratibu wa wakulima kuuza mazao yao kwa Serikali tofauti na sasa wafanyabiashara  wananunua kwa bei wanazotaka,ndio maana wakati wa mavuno gunia linafika hadi shilingi 6000 la kilo 100 huku debe likinunua hadi 2000 ambayo haijafika hata mfuko wa mbolea’anasema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Hai Clement Kwayu,anasema kuwa jitihada mbalimbali zinahitaji kwa Serikali kuwatengenezea wakulima miundombinu yakilimo cha umwagiliaji ili kuepukana na adha wanayoipata kila mwaka.

Anasema kuwa Serikali inaweza kutoa elimu kupitia kwa maafisa ugani wake ili wakulima kuweza kulima kilimo cha kisasa cha umwagiliaji ambacho kinategema maji kidogo tofauti na kilimo cha umwagiliaji cha kumwagilia kwa kutumia mfumo wa mafuriko ambao unapoteza maji mengi.

Kutokana na mvua kutonyesha mara kwa mara wakulima wanatakiwa kupewa elimu na kuwezeshwa juu ya kulima mazao yanayotahimili ukame,ili kuepukana na hasara wanayoipata.

Kiwango cha ukuaji katika shughuli za kiuchumi za kilimo kilikuwa asilimia 3.6 mwaka 2011 ikilinganishwa na asilimia 4.2 mwaka 2010,upungufu huu ulitokana na kuchelewa kwa mvua za msimu kwa mwaka 2009/10 ambazo ziliathiri uzalishaji wa mazao.

Kwa upande wa kiwango cha ukuaji katika shughuli ndogo za uzalishaji mazao kilishuka hadi kufikia asilimia 3.5 mwaka 2011 kutoka asilimia 4.4 mwaka 2010 kutokana na kupungua kwa uzalishaji kufuatia kuwepo kwa hali mbaya ya hewa katika msimu wa 2009/10.

Mwisho

No comments:

Post a Comment