Sunday, June 17, 2012

ziara ya ngawaiya na viongozi wengine wa chama cha mapinduzi ccm katika wilaya ya moshi vijijini.
katika ziara hiyo ngawaiya alitembelea na kukagua ujenzi wa mradi wa kusambaza maji katika kijiji cha kilototoni, kilichopo kata ya kilema kusini, ambapo pia alishiriki kweye zoezi la kufukia mabomba ya maji.

                                       
MIRADI ya maendeleo inayotekelezwa sehemu mbali mbali mkoani Kilimanjaro, inashindwa kukamilika kwa wakati uliopangwa kwa kile kinachoelezwa ni baada ya wananchi kuacha kujitolea kutokana na
itikadi za kisiasa.

Hayo yalibainika mwishoni mwa wiki, wakati wa ziara ya viongozi wa chama cha mapinduzi (CCM), katika kijiji cha Kilototoni kilichopo wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro, ambapo walitembelea mradi wa wa
maji ambao unawashirikisha wananchi katika utekelezaji wake.

Akiongoza msafara wa viongozi hao wa CCM mwenyekiti wa jumuiya ya wazazi mkoani Kilimanjaro, Thomas Ngawaiya alielezwa kuwa licha hatua mbali mbali kufikiwa kwenye mraddi huo, mwamko wa wananchi wanaochangia nguvukazi ni mdogo hivyo kushindwa kukamilika kwa wakati.

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara kijijini hapo Ngawaiya aliwaeleza wananchi hao kuwa serikali pamoja na wahisani wanatekeleza miradi mbali mbali ya kijamii, ambayo pia inahitaji mchango wa
wananchi wanaojitolea nguvukazi katika kuikamilisha.

Hata hivyo alisema mipango hiyo imekuwa na dosari baada ya wananchi kutoshiriki kikamilifu, ambapo sababu kubwa iliyobainika ni kuwepo siasa za chuki dhidi ya CCM na serikali yake.

“Napenda kuwaambieni kwamba maendeleo yanaanzia kwa wananchi wenyewe, tuanze kujipanga tujiulize tutawategemea wafadhuli mpaka lini, jitoleeni kufanya kazi hizi za kijamii kwa sababu ya itikadi za kisiasa”, alisema.

Aliongeza kuwa mfumo wa vyama vingi nchini ulilenga kuongeza kasi ya maendeleo, lakini hali hiyo imekuwa tofauti miongoni mwa wanachi ambao wamekuwa na chuki za wazi miongoni mwao, huku wakiyasahau malengo hayo yaliyokusudiwa.

“Vyama hivi vilianzishwa ili vilete maendeleo, tatizo vingine vimesahau malengo yale na kuanza kuwavuruga wananchi kwa kuwapandikizia chuki, sisi huku chini tunachukiana lakini naomba
mtambue kwamba viongozi wetu huko juu wanakaa na kuzungumza lazima tujifunze”, alisema.

Ngawaiya aliwataka viongozi wa dini nao kushiriki kikamilifu kukemea hali hiyo ambayo inaweza kuvuruga utulivu na amani iliyopo hapa nchini, baada ya chuki hizo za kisiasa kuendelea kukua miongoni mwa wananchi hao.

Kwa upande wao wananchi kijijini hapo walitoa ombi kwa mwenyekiti huyo kuwatatulia kero kubwa ya ukosefu wa huduma ya maji licha ya eneo hilo kuwa na maji yaliyochimbwa ardhini.

Wakizungumza kwenye mkutano huo wananchi hao walidai kuwa eneo la Kilototoni lina kisima cha maji ambacho kilichimbwa kwa madhumuni ya kusambaza maji kwa wakazi wake, lakini huduma hiyo ilisitishwa huku wananchi wakiendelea kuteseka bila kuwa na ufumbuzi.

Mwenyekiti wa kijiji hicho Robert Mosha, alitoa ombi kwa CCM kusaidia urejeshwaji wa huduma za maji kwa wakazi waishio maeneo hayo yaliyopo jirani na kituo kidogo cha mabasi cha Njia-panda.

Mosha alisema sababu za kusitishwa kwa huduma hiyo ni baada ya halmashauri ya wilaya ya Moshi inayohusika kukusanya fedha za mauzo ya maji kutoka kwenye kisima hicho kushindwa kulipa gharama za umeme unaotumika kwenye pampu ya kuvuta maji hayo kwa muda mrefu sasa.

Kutokana na hali hiyo Ngawaiya aliahidi wananchi hao kuwa suala hilo litafanyiwa kazi ambapo alimwagiza mwenyekiti wa kijiji hicho kuambatana naye kwenda kwenye ofisi za halmashauri ya wilaya ya Moshi ili kufahamu ukweli na kupata ufumbuzi wa tatizo hilo.

Hata hivyo Ngawaiya alisema changamoto kama hizo zimekuwa zikijitokeza katika maeneo mbali mbali wilayani Moshi zikiwemo zile za ukosefu wa vyoo kwenye masoko, hali ambayo pia alisema inachangiwa kwa kiasi kikubwa na uzembe wa baadhi ya watendaji wa halmashauri wasiotambua wajibu wao wa kazi.

No comments:

Post a Comment