MBUNGE wa zamani wa Arusha Mjini, Godbless Lema (CHADEMA),
amemwandikia Rais Jakaya Kikwete waraka mzito, akimshambulia waziwazi
kwamba alihusika kwa namna zote na maamuzi ya Mahakama Kuu Kanda ya
Arusha, yaliyomvua ubunge.
Katika waraka huo wenye maneno makali na mazito, Lema amemshambulia
Rais Kikwete akimtuhumu kutoa maneno aliyoyaita ya kebehi na
yaliyodhihirisha jinsi Ikulu ilivyoingilia hukumu ya kesi yake ya
ubunge, akidai kuwa ni kumkomoa baada ya kukataa kukubaliana na maombi
yake katika kikao cha wawili hao, Oysterbay, jijini Dar es Salaam, siku
chache kabla ya uchaguzi mkuu wa 2010.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, akiwa jijini Arusha, Rais Kikwete
alikaririwa katika mkutano wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB),
akidai kuwa asingekubali kuruhusu mkutano mzito kama huo kufanyika
katika jiji hilo miaka miwili nyuma kutokana na kukosekana kwa utulivu.
Hata hivyo, tamko hilo la Rais Kikwete limechukuliwa na mbunge huyo
kama lililomlenga yeye, na kumhusisha na fujo, hatua iliyomfanya
kumwandikia waraka mzito uliosambazwa katika vyombo vya habari.
Lema amedai kwamba tamko hilo la rais, ni ushahidi mwingine wa
waziwazi wa jinsi mamlaka zilivyoweka mkono wake, pamoja na kauli ya
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo aliyoitoa wakati akiwaapisha
wakuu wa wilaya ya kumshukuru jaji aliyetoa hukumu ya kesi yake.
“Natambua wewe ni rais na unayo mamlaka makubwa katika taifa hili
lakini vile vile nataka utambue kuwa huna mamlaka makubwa dhidi ya haki,
utu na ukweli.
“Umefurahia sana mkutano uliokupa fursa ya kutoa maneno ya kebehi na
kudhihirisha hila iliyofanywa na serikali yako… hata hivyo wakati huu
kuna mambo ya msingi ya kushughulikia zaidi ya kebehi na hadaa,
uchumi
wa nchi umeyumba, huduma za msingi za jamii zimepuuzwa, mpasuko katika
suala la Muungano na vururugu zinazoendelea Zanzibar, mfumuko wa bei,
hizi ni sababu chache ambazo haziwezi kuruhusu wakati huu kuwa wakati
wa kebehi na mizaha isipokuwa kazi,” amesema Lema katika waraka huo.
Lema amedai kuwa, Mama Theresa, Nelson Mandela, Martin Luther Jr na
Malcom X hawakuwa wabunge walipokuwa wakipigania haki za nchi zao na
watu wao, hivyo, na yeye hahitaji ubunge kupigania ukweli, haki na utu.
“Nahitaji dhamira safi, nia njema na huu utakuwa wajibu wangu mpaka
nakwenda kaburini. Nitakapomaliza mbio hizi najua nitapata fursa ya
kutazama nyuma yangu nione nini nilifanya; ukweli nisingependa kuona
vituo vya mafuta, maghorofa, magari na viwanja vingi kila kona ya nchi
bali haki, usawa na utu vikiwa kama nguzo ya imani ya watawala wetu
watakaokuwepo,” alisema na kuongeza:
“Pengine sitaishi miaka mingi sana kama utachukizwa sana na waraka
wangu huu, kwani Polisi, Usalama wa Taifa na Jeshi la Wananchi wanakutii
wewe, hata hivyo siogopi kufa kwani nisipokufa kesho, nitakufa siku
moja ambayo siijui, napenda kuishi maisha marefu nimwone mke wa mtoto
wangu kama itawezekana, lakini kuliko iwezekane kwa kuishi kwa hofu ni
bora ishindikane.”
Lema amedai kuwa huenda bado Rais Kikwete ana hasira alizodai zinaweza
kuwa zimetokana hasa na mkutano; “tuliokaa Oysterbay Dar mimi na wewe
kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, hata hivyo, sikupuuza maongezi
yetu isipokuwa nilichagua kufuata dhamira yangu na wito wangu wa
utumishi wa kweli katika jimbo langu na nchi yangu,” amesema.
No comments:
Post a Comment