Thursday, December 20, 2012

UJENZI WA SOKO LA LOKOLOVO MWAROBAINI WA BIASHARA ZA MAGENDO KUPITIA NJIA ZA PANYA KILIMANJARO.

 

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Katikati Leonidas Gama,akizungumza na viongozi wa kamati ya Usalama Wilaya ya Rombo,aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hiyo,Peter Toima baada ya kukamatwa kwa gari ambalo lilikuwa likisafirisha mazao aina ya mahindi kwenye Kenye kwa kupitia njia za Panya.
 Rodrick Mushi,Moshi
MWAROBAINI wa tatizo la usafirishaji wa mazao ya biashara na chakula  nchini umepatikana baada ya Serikali kupitisha mradi  wa ujenzi wa soko la kimataifa la bidhaa za mazao .
Ujenzi wa Soko hilo unatarajiwa kufanyika katika eneo la Himo Wilaya ya Moshi Mkoani Kilimanajaro,ambalo linakadiriwa kugarimu zaidi ya shilingi billion 5,mpaka kukamilika kwake.
Mpango wa ujenzi huo umekuja baada ya kuwepo kwa wimbi kubwa la usafirishaji wa mazao ya bidhaa kwenda nje ya nchi kwa kupitia njia za panya.
Hatua za kwanza baada ya kupatikana kwa eneo la ujenzi wa soko hilo,tayari Serikali Mkoani Kilimanjaro imeshatiliana saini na benki ya Uwekezaji (TIB) kupitia kwa Meneja wake Allan Magoma kwa ajili ya kupatiwa fedha za ujenzi wa soko hilo la kimataifa.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Leonidas Gama anasema kuwa ujenzi wa soko hilo ulikuja kwenye kikao cha Mkoa kilichofanyika mwezi wa tatu mwaka huu,baada kilio cha wafanyabiashara pamoja na kushamiri kwa biashara ya magendo.
Lakini anasema kuwa jitihada za Serikali siyo  kujenga soko la bidhaa za mazao bali pia kwenye mkataba walioingia na benki ya uwekezaji walipewa kiasi cha shilingi billion 10  kwa ajili ya ujenzi wa soko la mbogamboga eneo la njia panda.
Anasema kuwa ujenzi wa soko hilo unaweza kuchukua zaidi ya miaka miwili endapo shughuli za ujenzi na mkandarasi atakayeshinda tenda ya ujenzi wa soko hilo litafanya kwa wakati.
“Mwazo soko hilo lilikuwa lijengwe eneo la njia panda lakini eneo likawa dogo hivyo kulazinmika kulitumia kujenga soko la mbogamboga ukubwa wake ni hekari 9 na kwenda na eneo la Lokolova  lina ukubwa wa hekari 140”Alisema Gama.
Eneo ambalo soko hilo linajengwa linajulikana kama Lokolova ambalo lilikuwa eneo la ushirika wa wafugaji,hivyo Serikali kufanya mazungumzo nao kwa ajili kujenga soko eneo hilo.
Gama anasema Ugumu wa ujenzi wa soko hilo ulikuwa ni jinsi ya kupata fedha kwa ajili ya ujenzi,lakini baada ya hatua za awali za jinsi soko hilo linatakiwa kukamilika na kupitishwa imekuwa rahisi kuingia mkataba na benki ya uwekezaji.
“Kinachotakiwa  hivi sasa ni kutengenezwa kwa  garama halisi ya ujenzi wa soko (bill of quantity)ambapo baada ya kujua garama halisi itakayotumika  ni kutangaza tenda kwa ajili ya kumpata mkandarasi.”Alisema Gama.
Utaratibu wa soko hilo utakuwa unahusisha wafanyabishara kutoka mikoa yote nchini  kununua bidhaa za mazao sehemu mbalimbali na kuleta kwenye soko hilo la lokolova kwa ajili ya kuwauzia wateja kutoa ndani na nje ya nchi.
Mazao ya bidhaa za nafaka ambayo yatakuwa yanauzwa  kwenye soko la Lokolova ni pamoja na mahindi,mpunga mchele,mahindi maharage,Ulezi,uwele na mazao mengine ambapo yamekuwa yakisafirishwa kwa wingi kwa njia za panya kwenda nje ya nchi.
Ujenzi wa soko hilo utatoa fursa kwa wafanyabishara kutoka nchi za Afrika Mashariki na nyinginezo kuingia nchini hadi kwenye soko hilo na kununua bidhaa mbalimbali za mazao ambayo yanapatikana nchini.
Faida za ujenzi wa soko la lokolova.
Usafirishaji wa bidhaa za mazao kwenda nje ya nchi kwa njia ya panya ulikuwa ukikosesha Serikali mapato ambayo yangetokana na kodi ambayo ingetakiwa kutozwa kwenye mazao yanayoenda nje.
Lakini mbali na kuikosesha Serikali mapato pia ilikuwa inachangia kukosekana kwa takwimu sahihi ya mazao ambayo yameuzwa nje ya nchi kutokana na kutokuwepo kwa rekodi ya mazao yanayotoroshwa kwa njia za panya.
Hili la kukosekana kwa Takwimu, Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika Christopher Chiza anakiri kuwa Serikali imekuwa ikikosa takwimu muhimu hususani za Mazao yaliyouzwa nje,kutokana na biashara ya magendo.
Wakati akiwa ziarani Mkoani hapa alisema kuwa hali hiyo imekuwa ikichangia pia baadhi ya bidhaa na mazao yanayozalishwa nchini kuonekana nchi jirani ndio zinazalisha zaidi ilihali zinatoka nchini.
Serikali  kuzuia biashara ya usafirisha wa bidhaa za mazao bila kuweka utaaratibu wa wananchi kufanya biashara ilitoa mianya kwa mamlaka zilizokuwa zimepewa jukumu la kuzuia zoezi hilo ikiwemo polisi na mamlaka ya mapato (TRA) kulalamikiwa kuwepo kwa vitendo vya  kupokea rushwa kwa wafanyabiashara wa mazao.
Hali ya usafirishaji wa mazao ya bidhaa nje ya nchi yalikuwa yakiongezeka kutokana na mahitaji ya mazao hayo,pamoja na bei ambayo ilikuwa inatoa faida kubwa kwa wafanyabisahara.
Mbali na wafanyabiashara pia soko hili litatoa fursa kwa wakulima wa mazao ya chakula kuuza mazao yao moja kwa moja katika soko hili,na kuepuka kulanguliwa na wafanyabiashara.
Mmoja wa wakulima wa Mahindi,John Malisa,anasema kuwa Serikali imekuwa ikiwaonea wakulima kwa kuwapangia masoko ya kuuza mazao yao,ikiwemo la kuuzuiwa kuuza nje ya nchi.
Lakini kutokana na ujenzi wa soko hilo anasema kuwa atatumia fursa hiyo kufikisha mazao yake kwenye soko hilo kutokana na kuwa na wateja kutoka sehemu mbalimbali nje na ndani hivyo kupata bei nzuri.
Wakati Serikali ikitangaza kuruhusu biashara ya usafirishaji wa mazao nje ya nchi tayari ilitenga soko la muda eneo la Himo ambalo wafanyabiashara  kutoka nchi za Afrika Mashariki kuiingia nchini na kununua mazao kwa kufuata taratibu zilizowekwa.
Utaratibu huo ulianza mwezi marchi mwaka huu,hadi mwezi  julai ambapo hali hiyo imesaidia Serikali kujua takwimu ya mazao yaliyouzwa nje kwa kipindi hicho kifupi tofauti na hapo awali ambapo ilikuwa vigumu kupata takwimu kutokana na mazao kutoroshwa kwa njia za panya.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Leonidas Gama anasema kuwa kwa kipindi cha mwezi marchi hadi julai mwaka huu kiasi cha mahindi yaliyouzwa nje kwa wafanyabiashara kuingia nchini ni zaidi ya tani 26,588.
Lakini kwa upande wa mazao mengine kama Mikunde maharage zaidi ya tani tani 131 zilizwa nje na kusaidia kupatikana kwa mapato kwenye vijiji halmashauri za Wilaya husika ambapo biashara hiyo ilikuwa ikiufanyika.
Kwa Kijiji cha himo pekee ambapo ndipo soko hilo la muda lilipo kiliweza kupata mapato ya zaidi ya shilingi million 25,Huku Wilaya ya Rombo ikipata shilingi million 21,171,000 tangu kuanza kwa soko hilo la muda mfupi.
Halmasahuri ya Wilaya ya moshi vijijina nayo iliweza kupata mapato ya shilingi million 80 ,huku kukiwepo na zaidi ya shilingi 48,000,000 zilizopatikana kutokana na tozo ya magari yalikuwa yanatoka nje ya nchi kuingia nchini kununua mazao.
Hivyo kwa takwimu hiyo utaona ni jinsi gani Serikali ilikuwa ikikosa mapato kutokana na kutokuwepo kwa utaratibu na jinsi ya kuweza kutoza kodi,pamoja na kushamiri kwa biashara ya kusafirisha mazao kwa njia za panya.
Wafanyabiashara mbalimbali wanaofanya biashara ya mazao wanasema kuwa ujenzi wa soko hilo utakuwa mkombozi kwao,kwani hapo awali walikuwa wakikamatiwa bidhaa zao na wakati mwingine kutaifishwa wakiwa nchini.
Juma Hamisi anasema kuwa ujenzi wa soko hilo ni mwisho wa uonevu kwa wafanyabiashara kwani soko hilo litatoa fursa ya kufanya biashara kwa uhuru tofauti na ilivyokuwa hapo awali.
Lakini pia uwepo wa soko utatoa ajira kwa vijana na wananchi wengine kama lilivyotoa soko la muda pamoja na wajasiriamali wengine kama mama ntilie,kujipatia kipato kupitia wafanyabiashara na wegeni wengine watakaoukuwa waningia nchini.
Waziri wa Afrika Mashariki Samweli Sitta anasema kuwa ujenzi wa soko hilo ni moja wapo ya njia za kuendelea kuimarisha mahusiano baina ya nchi ambazo zilizopo kwenye soko la pamoja la Afrika Mashariki.
Anasema kuwa soko hilo litatoa chachu kwa wageni na majirani tuliopakana nao kuingia nchi kwa utaratibu uliowekwa na kuwezesha nchi kupata mapato pamoja na kumaliza biashara ya magendo.
Mwanzoni mwa mwaka huu kwenye mwezi Januari hadi marchi kulikuwepo na wimbi kubwa la usafirishaji wa mazao ya nafaka kwenda nje ya nchi,licha ya Serikali kupiga marufuku usafirishaji wa bidhaa hizo za mazao nje ya nchi.
Mwisho 

No comments:

Post a Comment