Tuesday, October 9, 2012

Kipi kinakwaza udhibiti bei ya sukari Kilimanjaro?


Rodrick Mushi


Sukari inavyoonekana kwa wingi kwenye godauni la kiwanda cha sukari TPC.


 

WANANCHI mkoani Kilimanjaro wamelalamikia serikali kushindwa kudhibiti upandaji wa bei kwa bidhaa ya sukari kiholela, licha ya kiwanda kinachotengeneza bidhaa hiyo ya sukari cha Tanganyika Sugarcane Plantation (TPC) kuwepo mkoani hapa.

Zaidi ya hilo, wananchi wanasema licha ya viongozi mbalimbali kutoa matamko juu ya kuhakikisha kuwa bidhaa hiyo haiuzwi zaidi ya shilingi 1,800 kwa kilo, bado bidhaa hiyo imekuwa ikiuzwa kwa bei ya juu, hivyo kuwaumiza wananchi.

Juma Rajab ambaye ni mkazi wa Kata ya Mamsera, wilayani Rombo, anasema wananchi wanashangazwa na kitendo cha kupuuzwa kwa agizo la Serikali kwa wananchi kuendelea kuuziwa sukari kwa bei kati ya shilingi 2,000 hadi sh 2,500 kwa kilo.

“Kama unavyojua, gharama za maisha zimepanda kila kitu tunanunua kwa bei ya juu kutokana na mfumuko wa bei, lakini hata bidhaa ambayo inazalishwa hapa mkoani kwetu tunauziwa kwa bei ghali kwa nini?” anahoji mwananchi huyo.

Anasema mbali ya sukari kupatikana kwa bei kubwa, kuna maeneo bidhaa hiyo imekuwa ikipatikana kwa shida au kiasi cha kwenda dukani siku mbili ukiambiwa hakuna na ikipatikana, unakuta unauziwa bei tofauti na uliyonunua siku ya jana yake.

Rajabu anasema wananchi walitarajia kuwepo kwa mabadiliko tangu alipofika waziri mkuu na kukaa na uongozi wa mkoani hapa kwa ajili ya ufumbuzi wa tatizo hilo ambaye alitoa maagizo ya bidhaa hiyo kuuzwa kwa shilingi 1700, lakini hakuna utekelezaji hadi sasa.

Bei hiyo ya sukari inayouzwa vijijini na Mjini ni tofauti kwani vijijini wamekuwa wakipandisha bei kulingana na umbali wa eneo lenyewe na kuiuza hadi shilingi 3000 kwa kilo huku maeneo ya mjini wakiuza shilingi 2000-2500.

Naye Amina Abasi, amesema hali hiyo moja kwa moja inachangiwa na serikali kushindwa kuwadhibiti wafanyabiashara wakubwa ambao wamekuwa wakihusika kwenye usambazaji wa bidhaa hiyo.

Wafanyabiashara wa rejareja wanasema kuwa, wakati mwingine wanalazimika kuamua kupandisha bei kutokana na bei ambayo wamekuwa wakinunua kwa wasambazaji wakubwa, hivyo kama hao wangedhibitiwa, bei ya rejareja ingetulia.

Mfanyabiashara wa rejareja Amos Tarimo wa Wilaya ya Moshi Vijijini anasema kuwa wakati mwingine wauzaji wa jumla (Wholesale), wanawapandishia bei bidhaa hiyo kwa kuwauzia mfuko wa kilogramu 50 kwa shilingi 9,5000 hadi 10,000 badala ya shilingi 75,000.

“Kuna wafanyabiashara wanaouza sukari katika nchi za Kenya na Uganda kwa kupitia katika njia za panya, badala ya kuwauzia wananchi waliopo vijijini na kusababisha kuwepo kwa uhaba wa sukari kwa baadhi ya maeneo,” anasema Tarimo.

Maeneo mbalimbali mkoani hapa, ikiwamo Wilaya ya Rombo, Moshi Vijijini, Hai na Siha, kumekuwepo na usumbufu mkubwa kwa bidhaa hiyo kutokana na kuwepo mianya ya njia za panya za kuisafirisha kwenda nje ya nchi.

Tatizo la kupanda kwa bei ya sukari, halijaanza mwaka huu 2012 bali lilikuwepo tangu mwaka jana kwenye miezi ya Aprili, Mei, Julai hadi Septemba, tatizo lililoonekana kuwa kubwa na kutaka kuwa sugu kwenye mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro.

Wakati kukitokea ongezeko hilo la bei, mwaka jana sukari iliuzwa hadi shilingi 4,500 kwa kilo kwenye maeneo ya kata za Mamsera, Tarakea wilayani Rombo, wilaya za Hai, Siha, Mwanga na sehemu nyingine wakikosa kabisa bidhaa hiyo.

Wakati bei ya sukari ilipopanda na kufika hadi shilingi 4,500 hadi 5,000 kwa kilo, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alitoa tamko akitaka bidhaa hiyo isiuzwe zaidi ya shilingi 1,800 na kuwaagiza maofisa biashara kutembelea maduka ya wafanyabiashara ambao wamekuwa wanauza tofauti na bei hiyo na kuchukuliwa hatua.

Uongozi wa kiwanda unasema kuwa haukubaliani na bei ya bidhaa hiyo inayouzwa na wafanyabiashara kwa wananchi kwa shilingi 2000 hadi 2,500, kwani bei wanayouza wao wangepaswa kuiza shilingi 1,800 kwa wateja.

Ofisa utendaji na utawala wa Kiwanda cha TPC, Japhary Ally, alisema kuwa mfumo mzima wa usambazaji wa sukari una matatizo na Serikali inapaswa kuliangalia suala hilo kwa makini kutokana na anayeumia kwa upandishwaji ni mlaji wa kawaida.

Anasema kuwa kunahitajika uangalizi wa hali ya juu kutokana na bidhaa hiyo kuendelea kuuzwa ghali huku akisema kuwa bei ambayo sukari inauzwa mpaka hivi sasa ya shilingi 2,000 hadi 2,500, uongizi wa kiwanda hicho haukubaliani nayo.

Ally anasema, kulingana na bei ambayo wamekuwa wakiwauzia wauzaji wa jumla, kwa mfuko wa kilogramu 50 kwa shilingi 76,000, wafanyabiashara wasingepaswa kuuza bei hiyo wanayouza kwa sasa.

“Serikali isipoangalia kwa umakini suala la wafanyabiashara kuendelea kuwalangua wananchi, lawama zimekuwa zikielekezwa kwa wazalishaji kuwa sisi ndio tunauza bidhaa hiyo ghali, lakini kwa bei wanayouza wao sisi tungepaswa kuuza mfuko shilingi 100,000,” anasema Ally.

Hata hivyo, anawatupia lawama wafanyabiashara wakubwa akisema wanaagiza sukari kutoka nje ya nchi na kuuza kwanza walioagiza nje huku wakiendelea kuihodhi inayotoka kiwandani hapo.

Anasema, mfumo wa usambazaji ambao ni wauzaji wa jumla, wakati na rejareja kuwa ndio wenye matatazo na ndiyo wanapaswa kuangaliwa ili kuacha kuuza sukari kwa bei ghali.

Japhary anasema kiwanda hicho kilikuwa kinauza kati ya tani 400 hadi 450, lakini kwa sasa wanauza kati ya tani 200 hadi 220 kwa siku kutokana na kasumba ya wafanyabiashara kuuza kwanza sukari ya nje wakisubiri ya TPC ikosekane sokoni kwa lengo la kuuza kwa bei kubwa.

“Sisi kama kiwanda tunaangalia mahitaji ya wananchi usambazaji na masoko ili kupanga bei ambayo haitakiwi kuwa chini sana, kwani itachangia sukari yetu kuuzwa nje ya nchi,” anasema Ally.

Anagusia pia kupanda kwa bei ya sukari mwaka jana na kusema kuwa, haikutokana na gharama za uzalishaji, bali ni nchi zinazopakana na Tanzania kuwa na uhaba wa bidhaa hiyo, hivyo sukari kwenda katika nchi hizo.

Anafafanua kuwa, nchi zilizokuwa na uhaba wa sukari ni Ruanda, Burundi, Uganda, Kongo huku Kenya ambayo nayo inazalisha sukari kwa wingi ikiwa na uhaba mkubwa hivyo nchini humo kuuzwa kati ya shilingi 4,000 hadi sh 4,500 ya humo.

“Nakumbuka wakati sakata la sukari kukosekana kabisa kwa walaji kutokana na wafanyabiashara wengi kudaiwa kuuza nje ya nchi, serikali pia ilitoa nafasi kwa Chama Kikuu cha Ushirika (KNCU) kusambaza sukari hiyo kwa wananchi vijijini,” anasema Ally.

Ally anasema kwa matatizo hayo, serikali bado ina jukumu la kuhakikisha wauzaji wa bidhaa hiyo ya wanapunguza bei ili kuwapunguzia wananchi wa kawaida gharama za maisha badala ya wao kutaka kujinufaisha.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kilimanajaro, Leonidas Gama alisema kuwa ni kweli tatizo la kuendelea kupandishwa bei kwa sukari kiholela linaendelea, huku akisema kuwa linachangiwa na wafanyabiashara wasio waaminifu.

Gama anasema kuwa tayari uongozi wa mkoa umeshapata malalamiko hayo ya kupandishwa kwa bei, huku ikiwapo taarifa za wafanyabiashara kuisafirisha bidhaa hiyo nchi jirani ya Kenya.

Anasema kuwa wameanza kujipanga kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi ili kudhibiti usafirishwaji huo wa sukari kinyemela kwenye nje ya nchi ambao umekuwa chanzo cha wafanyabiashara kupandisha bei ya sukari.

Hata hivyo, anasema kuwa tayari wamekwishakutana na uongozi wa kiwanda cha TPC ili kuangalia jinsi ya kurekebisha upandaji huo wa bidhaa ya sukari kiholela, pamoja na kupanga kukutana na wafanyabiashara wanaosambaza bidhaa hiyo.

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alipofanya ziara kwenye kiwanda cha TPC Aprili, 2011, alisema hakuna sababu yeyote ya msingi wananchi kuuziwa sukari kwa bei ya juu kama shilingi 1,700 hadi 2,000, wakati bidhaa hiyo inapatikana ndani ya mkoa wao.

Pinda anasema kuwa, bei ya sukari kiwandani ni ya kawaida na hata katika viwanda alivyopita lakini wafanyabiashara ndio wanawanyonya wananchi kwa kuwapandishia bei ya sukari.

No comments:

Post a Comment