Saturday, October 6, 2012

ADHARI NA SABABU ZA KUSHUKA KWA KILIMO CHA KAHAWA KIUCHUMI.

Wadau mbalimbali,kulia Venance Mallel akiangalia moja ya miche ya kwanza kupandwa na Missionary Mkoani Kilimanjaro.

Mche wa kahawa ambao una miaka mingi. 

Vicky Swai (40) mkazi wa kijiji cha Mbeera Kata ya Machame Uroki Wilayani Hai ambaye ni mjane na mama wa watoto watano kwa muda mrefu alitegemea kilimo cha kahawa,lakini baada ya kushuka kwa uzalishaji  kumeathiri kwa kiwango kikubwa maendeleo yake kiuchumi. 

Wakati wa uhai wa mume wake ambaye amefariki mwaka 2004 walikuwa wakivuna hadi kilo 900 kwenye  shamba la hekta 2  ambapo waliuza na kupata kipato kilichowatosha kutumia mpaka kipindi cha kuvuna tena kahawa.
Anasema kuwa hali ya maisha kwa sasa ni tofauti kwani amelazimika kuwa mfanyabisha  mdogo(machinga)baada ya kilimo hicho kukosa muelekeo.

Vicky anasema kuwa kilichomkatisha tamaa ya kutoendelea  na kulima zao hilo ni pamoja na kutumia garama kubwa kwenye uzalishaji lakini kuuza kwa bei ya chini.
Anasema kuwa kilimo cha kahawa kwa miaka ya 1998 walikuwa wakilima na kupata hadi tani 1000 kwa hekta mbili walizokuwa wakilima, ,tofauti na miaka ya 2000 kuendelea ambayo wamekuwa wakipata tani 200 kwenye hekta hizo.

 “Mimi mume wangu alikuwa akilima zao la Kahawa na alikuwa akipata magunia mengi,na hata baada ya kufariki mwaka 2004 kahawa tulizokuwa tunazitegema zilianza kutoa kahawa kidogo,huku zikishambuliwa na wadudu hatimaye kushindwa kuzihudumia kutokana na kuhitaji garama kubwa”Alisema.

Hata hivyo kupitia kilimo hicho anasema kuwa waliweza kuwasomesha watoto,kujenga na majukumu mengine,lakini maisha anayoshi kwa sasa ni yatofauti kidogo baada ya kufa kwa zao la kahawa.
Kilimo cha zao la kahawa kinategemewa na wananchi kwenye  Wilaya zaidi ya nne zilizopo Mkoani hapa,ambazo ni Wilaya ya Hai,Siha, Moshi, na Rombo,ambzao maendeleo yao yanategemea kilimo cha kahawa.

Katika kushuka kwa uzalishaji wa zao la Kahawa hakujamuadhiri Vicky peke yake bali wapo wakulima wengine ambao nao wameamua kujitafutia shughuli nyingine,baada ya kujiondoa kwenye kilimo cha kahawa.

Bashiri Andrew (45)ambaye ameamua kuikata mibuni ya kahawa na kulima mazao ya muda mfupi aina ya nyanya,yeye anasema kuwa mazao aliyolima yamekuwa na soko la uhakika,pamoja na kutochukua garama kama ilivyo kahawa.

Bashiri anasema kuwa Serikali imejitoa katika kuwahudumia wakulima wa kahawa pembejeo,tofauti na ilivyokuwa ikifanya kipindi cha nyuma,hivyo kuchangia pia wakulima wengi kukata tamaa.

“Mimi nilikuwa mkulima mzuri wa kilimo cha kahawa lakini ikafika wakati kilimo hicho kikawa ni hasara kwetu,kutokana na kupanda kwa garama za uzalishaji,huku bei ikishuka kwenye soko la dunia”Alisema Andrew.

Anasema kuwa wananchi wamekuwa wakilima zao hilo kila mwaka huku mafanikio yakiwa ni madogo kutokana na pembejeo za kilimo kuuzwa ghali,na upatikanaji wa miche kuwa wa shida na gharama kubwa.
Alex Munuo (50) mkazi Wilayani Rombo yeye  anasema kuwa maisha ambayo walikuwa wakiishi kwa kutegemea kilimo cha kahawa na ilivyo sasa ni tofauti,kutokana na kilimo hicho kuwa kama uti wa mgongo wa uchumi wa familia.
Anasema kuwa mafaniko waliyonayo ikiwemo nyumba wanayoishi walijenga kwa kilimo hicho,kuanzisha miradi mbalimbali pamoja nakuwapia watoto elimu na mahitaji mengine ya familia.
Uzalishaji wa zao la kahawa ulikuwa umejigawa katika makundi mbalimbali ikiwemo mashamba ya wawekezaji,yale ya vyama vya ushirika,pamoja mashamba ya watu binafsi.
Hali ya kilimo cha kahawa kukosa muelekeo  anasema kuwa imesababisha wanachi wengi kuyatelekeza mashamba yao,na kuamua kujiingiza kwenye biashara nyingine ili kuweza kumudu maisha yao.
Miongoni mwa changamoto ambayo ilionekana kuwa kubwa na kuelezwa na kila mkulima kwenye Wilaya za Hai,Siha,Rombo na Moshi wakulima wengi walieleza kukatishwa tamaa kukosekana kwa soko la uhakiki,pamoja na bei ndogo.

Wakulima wanasema kuwa ilifika wakati kahawa ikashuka bei kutoka shs. 1500 kwa kilo mwaka 1997/98 hadi shs. 500 kwa kilo mwaka 2002/03, wakati gharama ya uzalishaji kilo moja ya kahawa ikiwa shs. 800 mpaka 1200,hapo kukapelekea wakulima wengi kuacha kabisa kulima kahawa

Madhara ya kushuka kwa uzalishaji wa zao la Kahawa Mkoani Kilimanjaro.
Wakulima ambao walikua wakilima zao hilo la kahawa wanasema kuwa baada ya uzalishaji wa kahawa kushuka,wazazi wengi walishindwa kuwasomesha watoto shule pamoja na vijana wengi kuamua kujiingiza kwenye biashara ndondogo maarufu kama machinga na kupanda mlima kama wabeba mzigo.

“Zao la kahawa lilisaidia kwa kiasi kikubwa kwenye maendeleo ya  familia  walizokuwa wanalima zao hilo kwani wakati wa uzalishaji ulivyokuwa mzuri maisha yao yalikuwa mazuri,tofauti na yalivyo sasa uzalishai uliposhuka”Alisema Hamisi Juma mmoja wa wakulima.
Gift Matious ni miongoni mwa mwananchi,mkazi Mwika Wilaya ya Moshi Vijijini ambaye anasema kusuasua kwa uzalishaji wa zalo hilo kumekuwa na madhara kwa  wananchi wa Mkoa wa Kilimanajaro kwa ujumla.

Anakumbushia kipindi cha nyuma wakati uzalishaji wa kahawa ukiwa mzuri,pia kulikuwepo na huduma muhimu ambazo zilikuwa zikitolewa kwa jamii kupitia vyama vyake vya ushirika,ambavyo vilikuwa vikiundwa na wakulima wa zao hilo.

Anasema vyama vya ushirika vilikuwa na maduka ya ushirika ambayo yalikuwa yakiuza bidhaa mbalimbali,kwa wananchi,na wakati mwingine kupatiwa huduma hata kama  hawana fedha taslimu na kulipa kwa kukatwa kwenye malipo wanapouza kahawa.
Pia vyama hivyo vilikuwa vikitoa pembejeo za kilimo kwa wakulima,hali ambayo baada ya kusitishwa kwa pembejeo kumewafanya wananchi wengi kushindwa kununua pembejeo hizo kutokana na kuuzwa gali.

 “Baada ya kufa kwa uzalishaji wa zao la kahawa kuna baadhi maeneo vyama vya ushirika navyo vimekufa,majengo yake yamebomoka,hivyo wananchi hawapati huduma iliyokuwa ikitolewa na ushirika pamoja na wengine kupoteza ajira”Alisema Mongi.
Katika uuzwaji wa kahawa kwa vyama vikuu pia kulikuwapo na fedha za akiba ambazo alikuwa akilipwa kila mkulima mara baada ya kuuza kahawa kulingana na bei ambayo ingeuzwa kwenye soko la dunia.
“Wakati wa uzalishaji wa zao la kahawa ukiwa mzuri Umoja wa wakulima wa zao hilo kupitia chama Kikuu cha ushirika pia waliweza kuwa na miradi kama mahoteli,Benki,ambazo zilikuwa zikitoa huduma ,hivyo zao hilo lingekuwa linaendelea vizuri huenda wangekuwa na miradi mingi zaidi kama mashule na hata Vyuo vya elimu ya juu.”Alisema Mongi 

Mwenyekiti wa KNCU Mynard Swai anakiri kufa kwa baadhi ya maduka hayo ya ushirika ambayo anasema pia yalikuwa yakiuza vifaa mbalimbali,ikiwemo vya ujenzi na zana za kilimo.
Hivyo anasema kuwa kushindwa kufanya kazi kwa maduka hayo kutokana na madhara ya kushuka kwa uzalishaji kumechangia wananchi kukosa huduma muhimu.
“Maduka ya ushirika yalikuwa hayaendeshwi kibiashara kwa lengo la kupata faida kubwa,yalikuwepo kwa ajili ya kutoa huduma kwa wakulima,hivyo yaliweza kuuza vifaa mbalimbali ikiwemo vya ujenzi na kusaidia wakulima wengi kuwa na nyumba bora”Alisema.
 Kwa upende wake Mkurugenzi wa Manispaa ya moshi Bernadette Kinabo anasema kuwa kushuka kwa uzalishaji wa kahawa,kumechangia kwa kiasi kikubwa kufa kwa viwanda vya Moshi.
Anasema viwanda vilikuwa vinategemea kutoa huduma kwa kuwepo kwa mahitaji kwa wakazi wa mkoa wa Kilimanajaro,lakini baada ya kushuka kwa zao wa kahawa,kulipelekea viwanda zaidi ya 15 kushindwa kufanya kazi.

Mbali na viwanda kufa,lakini pia anasema hali ya kufa kwa zao hilo kumechangia kuwepo kwa wimbi kubwa la wafanyabiashara wadogo maarufu kama machinga ambao walikuwa wakitegemea kilimo pamoja na kufanya kazi kwenye mashamba ya wakulima.

Mbali na kufa kwa viwanda lakini uchumi wa wakazi wengi wa moshi akamaanisha kipato cha wananchi kimepungua,huku wengine wakiwa hawana kazi,pamoja na kushindwa kuchangia kazi mbalimbali za maendeleo.
“Kilimo cha kahawa kilikuwa muhimu kwa wananchi Mkoani hapa,na baada ya zao hili kukosa muelekeo basi hata maendeleo ya wananchi na Mkoa yamekuwa nyuma,ndio maana Serikali inafanya juhudi mbalimbali kufufuza zao la kahawa”Alisema Kinabo.
Sababu za kushuka kwa uzalishaji
Wakulima wengi kwenye Wilaya Hai,Siha,Rombo na Moshi Vijijini ambao mwandishi wa makala hii aliweza kuzungumza nao walieleza kuwa sababu ambazo zimepelekea kushuka kwa zao hilo kuwa ni pamoja na kushuka kwa bei,na kupanda kwa garama za uzalishaji.
Pia wanasema kuwa Serikali kutotoa ruzuku ya pemebejeo kwa wakulima,licha ya kuwepo kwa garama kubwa za uzalishaji nako kukachangia wakulima wengi kukata tamaa kabisa ya uzalisha na kuamua kulima mazao mengine.
Mwenyekiti wa chama kikuu cha ushirika Mkoani Kilimanjaro,(KNCU) Mynard Swai anakiri kushuka kwa uzalishaji wa zao hilo,na kusema kuna sababu mbalimbali zilizopelekea kushuka kwa uzalishaji.
Anasema kuwa kilimo hicho kilipanda miaka ya 1997/98 kwa Mkoa wa Kilimanjaro kuweza kuzalisha hadi tani  11325 lakini ulishuka tena kwenye miaka ya 2007/8 na kufika tani 3495,kutokana na changamoto mbalimbali.
Miongoni mwa changamoto iliyopeleka uzalishaji kushuka ni pamoja na Mibuni mingi ya zao la kahawa inayotunzwa na zaidi ya asilimia 60 inamiaka zaidi ya 40.

Mibuni kuwa na umri mkubwa inasababisha uzalishajikushuka kwa mkulima kupata  kilo 200 badala ya zaidi ya kilo 500 kwa hekta zinazoweza kuzalishwa katika shamba lenye mibuni mipya.

Sababu nyingine ya kushuka kwa uzalishaji ni pamoja na  mashambulizi ya magonjwa ya chulebuni (CBD) na kutu ya majani (CLR) kusababisha hasara kubwa ya mazao toka shambani pamoja na kuharibu ubora wake.

“Pembejeo za kilimo kama madawa zimekuwa zikipatikana kwa garama kubwa,hivyo mkulima kushindwa kumudu garama hizo,hususani ni pale mibuni inapokuwa inashambuliwa na magonjwa kutokana na hali ya hewa”Alisema Swai.

Huduma duni za ugani na ukosefu wa vitendea kazi hasa vyombo vya usafiri kwa Maafisa Ugani pamoja na ukosefu wa mafunzo ya mara kwa mara na uhaba wa wataalamu pamoja na kupungua kwa maeneo ya kulima kahawa kutokana na maeneo hayo kutumika katika ujenzi wa makazi ya watu.

Hali ya uzalishaji kwa sasa
Mkurugenzi Mkuu wa bodi ya Kahawa,injinia Adolph Kumburu akizungumza na mwandishi wa makala hii kuhusiana na uzalishaji wa kahawa kwa kipindi cha miaka 5  anasema uzalisjaji umekuwa wa wastani wa tani 50,000 za kahawa safi ambayo imekuwa ikizalishwa nchini.
Uzalishaji huo kwa kipindi cha miaka mitano nchini  umekuwa wa kupanda na kushuka, kutokana na msimu na hali ya hewa,ambapo mwaka jana 2011/12 uzalishaji ulishuka hadi tani 33,000 za kahawa safi toka tani 54,000 mwaka  2010/11.
 Anasema kuwa kwa mwaka huu 2012/2013 uzalishaji huo unatarajiwa kupanda na kufikia tani 55,000 angalau kuweza kufikia uzalishaji wa mwaka 2010/2011 ambao uzalishaji wake wa kahawa ulikuwa tani 54,000 kwa Tanzania nzima.
Anasema kuwa Mkoa wa Kilimanjaro,kwa sasa unazalisha kiasi cha tani 4,000 tu za kahawa safi ambayo ni sawa na asilimia 8 tu ya kahawa yote nchini.
Hapa ndipo uzalishaji wa zao la kahawa unajidhirisha kushuka,kutokana na ukweli kuwa  kipindi cha nyuma kwenye miaka ya 1997 Mkoa wa Kilimanjaro pekee ulikuwa ukizalisha zaidi ya asilimia 30-36 ya kahawa yoye iliyokuwa ikizalishwa nchini.
“Kwa kipindi cha miaka mitano uzalishaji wa zao la kahawa kama hali ikiwa nzuri kwa Mkoa wa Kilimanjaro umekuwa ukichezea kwenye kati ya tani 3,000 hadi 9,000 kulingana na hali ya hewa”Alisema Kumburu.
Soko la Kahawa likoje?.
Kahawa inayozalishwa nchini inategemea zaidi soko la nje,kutokana na asilimia 95 ya kahawainayozalishwa nchini kuuzwa nje ya nchi na asilimia  5 ndiyo inayouzwa kwenye soko la ndani.
Kutokana na hali hiyo ni dhahiri kuwa bei itakuwa inategemea zaidi soko la dunia na aina ya kahawa,mbaya zaidi ni pale nchi ambazo zinanunua kahawa kwa wingi zinapokumbwa na mdororo wa uchumi,wakulima wa kahawa huwa na kilio zaidi.
Adolph Kumburu anasema kahawa huuzwa nje ya nchi ikiwa safi (clean) na ikiwa katika madaraja,huku masoko ya kahawa aina ya Arabika yakiwa Marekani na kahawa za Robusta yakiwa Uingereza.
Bei ya Kahawa kwenye soko la dunia kwa msimu huu wastani wa bei kwa kahawa za Arabica ni shilingi 5000 za kitanzania na kwa kahawa za robusta ni shilingi 3200.
Kuhusu upatikanaji wa soko la uhakika,Kumburu anasema kuwa zao hilo kwa sasa lina soko la uhakika na siyo kama kipindi cha nyuma,ila cha kuzingatia ni kuzalisha kahawa yenye ubora ili kupata bei nzuri.
Jitihada za kuimarisha  Kilimo cha Kahawa.
Kutokana na soko la kahawa kutegemea zaidi masoko nje ya nchi, kama Japan, Ujerumani, Marekani, Uholanzi, Italia na Ubelgiji,jitihada mbalimbali zinahitajika kuimarisha soko letu la ndani ili kutotegemea kwa kiasi kikubwa kupangiwa bei na soko la dunia.
Kumburu anasema kuwa zipo jitihada mbalimbali ambazo zinafanywa na bodi hiyo ya kahawa katika kuhakikisha soko la ndani linakuwa zaidi ya asilimia 5 iliyopo kwa sasa.
Miongoni mwa mikakati ni pamoja na Kuhamasisha wananchi kunywa kahawa yao na kupata manufaa ya kunywa kahawa kiafya licha ya kupata kiburudisho tu,na wakati mwingine kuitumia kama tiba ya kiafya.
Pia kufanywa kwa uhamasishaji katika taasisi za serikali na katika maonyesho mbali mbali kama vile nanenane na sabasaba kuhusu unywaji wa kahawa,ikiambatana na faida za kunywa kahawa.
Lakini pia zipo jitihada mbalimbali ambazo zinafanywa na uongozi wa Mkoa wa Kilimanjaro,kutokana na umuhimu wa zao la kahawa kwa uchumi wa mkoa,kwa kushirikiana na chama kikuu cha Uhsirika Mkoani Kilimanjaro(KNCU).
Miongini mwa jitihada hizo ni pamoja na taasisi ya Serikali ya utafiti wa kahawa(TaCri)kwa kushirikisha vikundi vya wakulima kuanzisha bustani za miche kwenye maeneo yao wakulima ili kurahisisha upatinaji wa miche bora ya kahawa,
Kujenga na kufufua viwanda vya kumenya kahawa (central pulperies)ambavyo vilikuwa vimekufa, baadhi ya vikundi/watu binafsi kuruhusiwa kuuza kahawa yao ya ubora wa juu moja kwa moja nje na kupata bei nzuri
Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Mnard Swai anasema kuwa chama hicho kwa kushirikiana na taasisi ya utafiti ya zao la kahawa,(Tacri)wameweza kusambaza miche mipya zaidi ya 500,000 kwa wakulima wa kahawa miche ambayo ni ya kisasa.
Pia anasema kuwa chama hicho kumewaajiri maafisa ugani,hivyo kusaidia kuongeza idadi ya maafisa ugani kutoka 8 hadi 29 ambao wamekuwa wakifanya kazi kwa ukaribu na wakulima na kugaramiwa vifaa vya kazi na KNCU.
Anasema lengo ni kuongeza tija katika uzalishaji kutoka kilo 200 kwa hekta hadi kilo 600-1000 kwa kupanda aina bora za kahawa zilizozaliswa na TACRI ambazo zinauwezo wa kuzuia magonjwa pamoja na kuwa na uzalishaji mzuri.
“Kilimo cha kahawa kinategemea bei kutoka nje ya nchi na ndio wanapanga bei ya zao hilo,hivyo KNCU kwa kushirikiana na wadau wa kahawa tunajiahidi kuhakikisha kuwa kahawa inayozalishwa inauzwa asilimia 40 nchini”Alisema Swai.
Tanzania inazalisha kahawa namba 1 (clear)kwa wastani wa tani 50,000 na hii ni sawa na asilimia 0.8 ya uzalishaji wote wa dunia.
Miongoni mwa Mikoa inayoongoza katika uzalishaji ni pamoja na Kagera ambao uzalisha  wake ni asilimia 30 hadi 40% ya kahawa yote inayozalishwa Nchini.
Kwa upande wa pato la taifa kahawa huchangia asilimia 15 ya sehemu ya kilimo (agricultural GDP)ambapo jumla ya mchango wa sekta ya Kilimo kwenye pato la taifa ni asilimia  24.7 .


No comments:

Post a Comment