RAISKIKWETE ATOA RAMBIRAMBI KWA KIFO CHA RAIS WA MALAWI HAYATI BINGU WA MUTHARIKA.
Hayati Bingu wa Mutharika
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Makamu wa Rais wa Malawi, Mheshimiwa Joyce Banda kuomboleza kifo cha kiongozi wa nchi hiyo, Mheshimiwa Rais Bingu wa Mutharika.
Katika salamu zake hizo, Rais Kikwete amemwambia Mheshimiwa Banda
kuwa Tanzania imepokea kwa mshtuko na majonzi makubwa taarifa za kifo
cha Rais Bingu wa Mutharika ambaye Rais Kikwete amemwelezea kama
kiongozi wa karibu na rafiki mkubwa wa Tanzania.
Amesema Rais Kikwete katika salamu hizo, “Sisi katika
Tanzania tumepokea taarifa za kifo cha Rais Bingu wa Mutharika kwa
mshtuko na majonzi. Alikuwa kiongozi na rafiki wa karibu wa Tanzania na
rafiki yangu. Alikuwa kiongozi wa kutumainiwa miongoni mwa nchi
wanachama wa Jumuia ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) na Bara la
Afrika lote.”
Ameongeza Rais Kikwete: “ Kwa hakika, Afrika imempoteza
kiongozi imara, aliyeamini katika maslahi ya Bara letu na watu wake.
Siku zote tutamkumbuka kwa dhamira yake na moyo wake katika kupigania
umoja, amani, utulivu na ustawi wa mataifa yetu mawili na Afrika nzima.”
“Kwa niaba ya Serikali na Wananchi wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania na kwa niaba yangu mwenyewe, nakutumia wewe Mheshimiwa,
familia ya marehemu na wananchi wote wa Malawi salamu za rambirambi za
dhati ya mioyo yetu kufuatia kifo cha ghafla cha Mheshimiwa Rais Bingu
wa Mutharika,” amesema Rais Kikwete katika salamu zake.
Mwisho.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
No comments:
Post a Comment