MANISPAA ya Moshi ni miongoni mwa manispaa zinazoongoza kwa
usafi, lakini hivi sasa suala hilo la usafi wa mazingira linakabiliwa
na changamoto mbalimbali ikiwamo ya itikadi za kisiasa.
Kwa upande wa Tanzania, Manispaa ya Moshi ni miongoni mwa manispaa
ambazo zimekuwa zikiwavutia wengi, wakiwamo madiwani, wageni mbalimbali
kutoka nje na ndani ya nchi kufika na kujifunza jinsi ya kuweka
manispaa zao kuwa safi kama Moshi.
Zipo sheria ndogondogo ambazo hutungwa na manispaa ya mji kwa ajili
ya kuhakikisha usafi unaendelea kuwapo na watu ambao wamekuwa
wakichafua mazingira wanachukuliwa hatua za kisheria pamoja na kutozwa
faini.
Kila mgeni anayefika mjini hapa kama ameambatana na mwenzake basi
utasikia akimwambia mwenzake, angalia usije ukatupa takataka, ikiwa ni
vocha, kichungi cha sigara au kutema mate, kwani utatozwa faini na watu
wanaosimamia usafi.
Katika mji huu kuna mawakala wanne ambao ndio waliopewa jukumu la
kusimamia usafi wa mazingira, ila kinachonishangaza ni kwamba usafi
unaosimamiwa ni Kata ya Kiusa, Kata ya Mawenzi kuzunguka Stendi Kuu,
Soko la Kati, Barabara ya Ghala, Barabara ya Mawenzi, maeneo ya Mtaa wa
Dar es Salaam, Mawenzi na Posta.
Madiwani wanasema mawakala waliopewa jukumu hilo kwa sasa wamegeuka
kuwa magaidi kwani wamekuwa wakiwakamata wananchi na kuwapeleka
pasipojulikana na hata wakati mwingine kuwatoza kiasi kikubwa cha pesa
kuliko zile zilizowekwa.
Lakini ukweli ni kwamba mawakala waliopewa jukumu la kusimamia usafi
wa mazingira wamegeuka miungu watu, kwani hata baada ya baraza
kupunguza kiwango cha faini kutoka sh 50,000 hadi sh 10,000 bado
waliendelea kutoza kiwango cha sh 50,000 na kudiriki kutoa hata risiti
bila woga.
Hivyo kinachochukuliwa na wanasiasa hivi sasa ni kitendo cha baraza
la madiwani kuwaondoa mawakala waliokuwa wanasimamia zoezi hilo la
usafi wa mazingira na kurudisha manispaa.
Meya wa Manispaa ya Moshi, Japhary Michael, akizungumza kwenye moja
ya kikao cha baraza anasema wameamua kuwaondoa mawakala kwa sababu
wanawatesa sana wananchi, kibaya zaidi wanawateka wananchi na kuwatoza
kiwango kikubwa cha pesa.
Anasema mawakala hao mkataba wao utakwisha Juni 30, lakini hivyo ni
vema wakasubiri kwisha kwa mkataba wao ili wasije kuiingiza halmashauri
kwenye hasara ya kuwalipa gharama kwa kusitisha mkataba.
Mmoja wa madiwani, Hawa Mushi, anasema kuwa ushahidi upo wa risiti
kwa mawakala hao kuwatoza faini kubwa wananchi na kuwapora wananchi
mali zao na malalamiko hayo walikwisha kuyafikisha kwa mkurugenzi
lakini yanashindwa kufanyiwa kazi kutokana na kampuni hizo za usafi
kumilikiwa na baadhi ya watumishi wa halmashauri.
Kwa mtazamo wangu, ni wakati mwafaka sasa viongozi wa Manispaa ya
Moshi kushirikiana kwa pamoja kusimamia usafi wa mazingira ili
kuendelea kubakiza heshima ya mji wa Moshi kama ulivyokwisha kujengeka
tangu awali badala ya kulaumiana.
Michael anasema kuwa kwa sasa kuna magari yanayozunguka kwenye kata za Manispaa
ya Moshi kwa ajili ya kuchukua taka, pamoja na utaratibu uliokwisha
kuanzishwa wa madiwani na wenyeviti wa mitaa kufanya usafi kwenye
maeneo yao kila mwishoni mwa wiki.
Anasema licha ya jitihada hizo, bado kuna dhana tayari imekwisha
kujengeka kuwa mji wa Moshi ni mchafu, na hiyo imetokana na CHADEMA,
lengo likiwa ni kuwachonganisha ili wananchi waone kuwa CHADEMA ndiyo
chanzo cha mji wao kuwa mchafu.
Kwa mtazamo wangu, lengo la madiwani wa CHADEMA ni kuwanusuru
wananchi, kwani tayari kampuni zinazosimamia zoezi hilo zinadaiwa kuwa
za vigogo, hivyo ni bora wakatumika askari wa manispaa na mgambo ili
amani iendelee kubaki kwa wananchi.
No comments:
Post a Comment