Sunday, October 21, 2012

                             UCHAGUZI UWT...VIGOGO NJEEEEEEE.....

NI DK HUVISA, RITHA MLAKI, MLATA WALIKUWA WAKIWANIA UWAKILISHI UWT, MWANGUNGA AREJEA KWA KISHINDO, MADAI YA RUSHWA YATAWALA
BAADHI ya vigogo akiwamo waziri mmoja na wabunge waliokuwa wakiwania nafasi za mbalimbali za uwakilishi kupitia Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) katika uchaguzi uliofanyika juzi mjini hapa, wameangukia pua baada ya kushindwa katika kinyang’anyiro hicho.

Vigogo hao ni pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Dk Terezya Huvisa, Mbunge wa Viti Maalumu, Ritha Mlaki na Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Angela Kizigha ambao walianguka katika kuwania nafasi ya ujumbe wa Baraza Kuu la UWT kutoka Tanzania Bara. Dk Maua Daftari alijitoa muda mfupi kabla ya kura kupigwa, kwa upande wa Zanzibar.

Upepo ulianza kuvuma vibaya kwa Mlata ambaye awali, alishindwa katika nafasi ya uwakilishi wa UWT katika Jumuiya ya Wazazi. Alibwagwa na Mbunge mwenzake, Namelok Sokoine aliyepata kura 740. Namelok hakuwapo kwenye mkutano huo. Mlata ambaye alikuwa akitetea nafasi yake, alipata kura 337.

Matokeo hayo yanamfanya Mlata kuwa na wakati mgumu katika kinyang’anyiro cha uongozi wa Jumuiya ya Wazazi ambako anawania uwenyekiti akichuana na Abdalah Bulembo na Kapteni Mstaafu John Barongo katika uchaguzi ulipangwa kufanyika Jumamosi ijayo.

Wengine walioanguka ni Wabunge wa Viti Maalumu, Halima Mamuya na Purdenciana Kikwembe pamoja na Naibu Waziri wa Afya wa zamani, Dk Aisha Kigoda na aliyewahi kuwa Mbunge wa Kibaha Vijijini, Dk Zainabu Gama ambao walikuwa wakigombea ujumbe wa Nec kupitia UWT.
Wakati baadhi ya vigogo wakianguka, Waziri wa zamani wa Maliasili na Utalii, Shamsa Mwangunga alirejea kwa kishindo baada ya kushinda nafasi mbili ambazo ni ujumbe wa Nec na ule wa Baraza Kuu la UWT.

Uchaguzi huo ulisimamiwa na vigogo watatu wa CCM, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Tanzania Bara, Pius Msekwa, kada wake wa siku nyingi, Abdulrahaman Kinana na Mbunge wa Uzini, Muhammad Seif Khatib na mkutano wa uchaguzi ulifanyika chini ya uenyekiti wa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Profesa Anna Tibaijuka, kuwa nwenyekiti wake wa muda.

Wabunge wang’ara
Wabunge walioshinda nafasi za ujumbe wa Nec ni pamoja na Naibu Waziri wa Fedha, Janeth Mbene, Mbunge wa Ukonga, Eugen Mwaiposa, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, Pindi Chana, Wabunge wa Viti Maalumu Diana Chilolo, Zainabu Kawawa, Betty Machangu, Mary Mwanjelwa na Subira Mgalu.

Kutoka Tanzania Visiwani walioshinda nafasi za Nec ni Panya Ali Abdallah, Fatma Said Ali, Maudline Castico, Amina Andrew Clement, Waride Bakari Jabu na Tauhida Nyimbo.

Kwa upande wa nafasi za ujumbe wa Baraza Kuu la UWT, walioshinda kutoka Bara ni Halima Dendego, Amina Masenza, Juliana Manyerere, Shamsa na Mbunge wa Nkenge, Asumpta Mshama.
Kwa upande wa Zanzibar, walioshinda ni Zainab Khamis Shomari, Khadija Hassan Aboud, Mwanajuma Majid Abdallah, Catherine Nao na Elizabeth Mayala.

Kwa upande wake, Esther Mambali alichaguliwa kuwa mwakilishi wa UWT katika Jumuiya ya Vijana (UVCCM) na kwa mujibu wa ratiba, kesho ataanza kuitumikia nafasi yake hiyo atakaposhiriki Mkutano Mkuu wa UVCCM unaoanza kesho mjini hapa.

Vituko vya uchaguzi
Zomeazomea na majigambo vilitawala katika Viwanja vya Chuo cha Mipango ulikofanyika uchaguzi huo, wakati wajumbe wa mkutano huo mkuu wa nane wa UWT.Hali hiyo ilisababishwa na wapambe wa wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya UWT lakini kwa sehemu kubwa, ile ya uenyekiti.


Kambi za Sophia Simba na Anna Kilango Malecela zilikuwa zikitambiana na kurushiana vijembe vya hapa na pale. Kambi ya Simba ilikuwa imesheheni vijana wa kiume kutoka nje ya Dodoma na hivyo ilionekana kuwa na nguvu katika vita hiyo ya maneno.

Utulivu pekee ulikuwa kwa mgombea wa tatu, Maryrose Majinge ambaye wakati wote alionekana kuwa ni mtu asiyekuwa na kundi.

Baada ya kukurukakara za kutwa nzima, hatimaye Kinana alitangaza matokeo ya uchaguzi huo saa 5:45 usiku na Simba kuibuka kidedea kwa kumwacha kwa mbali Malecela kwa tofauti ya kura 405.
Wakati wa kuahirisha mkutano huo, Kilango hakuwapo kwa taarifa kwamba alifiwa na kaka yake, hivyo alilazimika kusafiri kwenda msibani Same, Kilimanjaro.

Kwa upande wake, Simba kabla ya kuahirisha mkutano huo usiku saa 7:27 alikiri kwamba licha ya ushindi alioupata, “kazi ilikuwa ngumu”.

Hata hivyo, tofauti na wakati wa kujinadi, ambapo alimbatiza jina mmoja wa wagombea wenzake kuwa ni ‘mbwatukaji,’ safari hii alionekana kuwa mtulivu.

Rushwa chooni
Hata hivyo, uchaguzi huo unadaiwa kutawaliwa na vitendo vya rushwa, huku watoaji na wapokeaji wakitumia mbinu za hali ya juu kuwakwepa maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Choo cha wanawake kilichopo nyuma ya Ukumbi wa Mwalimu Julius Nyerere katika Chuo cha Mipango, Dodoma ndicho kinachodaiwa kutumika kugawa rushwa wakati mkutano wa uchaguzi ukiendelea.

Habari zilizopatikana jana mjini hapa zinadai kuwa rushwa ilianza kutolewa Oktoba 18 na kuendelea hadi usiku wa manane wa Oktoba 19, ambao ulikuwa ni wa kuamkia siku ya uchaguzi. Kwa mujibu wa habari hizo, kiasi cha fedha kilichokuwa kikitolewa ni kati ya Sh50,000 na 100,000, na kwamba kwa baadhi ya wajumbe wenye nafasi katika ngazi za wilaya na mikoa kilikuwa kati ya Sh200,000 na 300,000.

Kutumika kwa choo kugawa fedha, kulisababisha foleni kiasi cha kuzua mvutano miongoni mwa wajumbe waliokwenda kujisaidia kutokana na kukaa sana nje wakisubiri. Baadhi ya wajumbe walilazimika kuanza kutumia vyoo vya wanaume vilivyopo mbele ya ukumbi, hali ambayo ilisababisha kuwapo mkanganyiko mkubwa juu ya matumizi ya vyoo hivyo.

Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo alisema katika njia ya kuingia kwenye vyumba vya choo hicho, kulikuwa na msururu wa watu ambao walikuwa wakiingia katika moja ya vyoo hivyo kuchukua fedha zao. “Huu uchaguzi wa ajabu, watu wamejifungia vyooni, ushawahi kuona wapi chumba kimoja cha choo wanaingia watu wawiliwawili kila wakati?”alihoji mmoja wa wajumbe wa mkutano huo kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Kutokana na msongamano wa watu waliokuwa wakisubiri zamu zao za kwenda kuchukua fedha katika chumba kimojawapo cha choo, yalizuka malumbano makali ya maneno miongoni mwa wajumbe, huku kundi moja likilishutumu jingine kwa kujihusisha na rushwa.

“Jamani mbona mnatutesa hivyo, kama ni rushwa zenu kwa nini msitafute sehemu nyingine za kupeana hadi mje huku chooni …,” alinukuliwa mmoja wa wajumbe akilalama.

Kauli hiyo ilisababisha wajumbe wengine kumjibu wakimtaka athibitishe iwapo kulikuwa na ugawaji wa fedha chooni.

Hata hivyo, haikufahamika mara moja ni kundi gani lilikuwa likituhumiwa kugawa fedha hizo. Mbinu nyingine zilizotumika ni pamoja na kuwatumia wauzaji wa nguo na mamalishe.

Waliopaswa kupewa fedha hizo walielekezwa sehemu za kwenda kuchukua mzigo wao na mchakato huo uliendeshwa kwa ustadi mkubwa kiasi kwamba Takukuru hawakuweza kuwagundua wahusika.
SOURCE: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment